Madereva na makondakta wa daladala jijini Dar es Salaam wametangaza mgomo wa chinichini kuanzia leo.
Taarifa za mgomo huo wa siku mbili zilisambazwa jana na baadhi ya madereva kwa kutumia ujumbe wa maandishi ulioandikwa katika vikaratasi.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mgomo huo utahusisha njia zote za mkoa wa Dar es Salaam, huku madereva hao wakidai mgomo huo una baraka zote za Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (DARCOBOA).
Maderava hao wanadai sababu ya mgomo huo ni maslahi duni, kero za barabarani zinazosababishwa na Kampuni ya Majembe na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, (Trafiki) ambao wamekuwa kikwazo kikubwa.
Madai mengine ni kutopatiwa dhamana, kutaka mazingira bora ya kazi pamoja na mishahara na makato ya mishara kupelekwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na marupurupu mbalimbali.
Tanzania Daima ilishuhudia baadhi ya madereva wakipeana vikaratasi hivyo katika maeneo ya Posta, Gongo la Mboto, Buguruni na Ilala huku kukiripotiwa kuonekana hali kama hiyo maeneo ya Mwenge.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa masharti ya kutotajwa majina, madereva hao walisema wameamua kufanya mgomo huo kutokana na manyanyaso wanayoyapata kutoka kwa Majembe na trafiki pamoja na kudai maslahi yao.
“Tunafanya kazi katika mazingira magumu, huku tukisumbuliwa na Majembe na trafiki na mwisho wa siku hakuna tunachokipata kwani mwajiri naye amekupangia hesabu yake. Kwa kifupi hatuna uhakika na maisha yetu,” alisema dereva mmoja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa DARCOBOA, Sabri Mabruki, alipoulizwa kuhusiana na habari za kuwepo kwa mgomo huo, alisema hana taarifa.
“Mimi sina taarifa ya mgomo huo, ndiyo kwanza nazisikia kwako, hakuna mgomo sisi hawajatuletea taarifa zozote,” alisisitiza Mabruki.
Mabruki aliendelea kusema kuwa madai yao hayo ya kutaka kugoma hayana msingi wowote kwao kwani mikataba ya madereva hao iko wazi na kila siku wanaambiwa kufuata mikataba yao lakini hawajitokezi.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mpaka sasa madereva 2500 baadhi yao wana mikataba huku wengineo wakiombwa kuchukua mikataba yao lakini hawataki kufanya hivyo.
“Sisi kama DARCOBOA, tunasema mgomo huo si halali na wala hatuujui,” alisema Mabruki.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Madereva na Makondakta wa Mabasi ya Abiria Dar es Salaam (UWAMADAR), Shukuru Mlawa, hakuweza kupatikana kuzungumzia ngomo huo.
.
No comments:
Post a Comment