Thursday, March 11, 2010

MGOMO WAKWAMISHA HUDUMA NCHINI UGIRIKI

Huduma mbalimbali za umma zimesimama nchini Ugiriki kutokana na mgomo wa saa 24.

Wafanyakazi katika sekta ya binafsi na watumishi katika sekta ya umma leo wameendelea na mgomo nchini Ugiriki kote na kutokana na hayo huduma za usafarishaji zimesimama, shule zimefungwa na ndege hazikuruka.

Sababu ya mgomo huo ni kupinga mpango wa kubana matumizi uliopitishwa na serikali ya nchi hiyo.

Katika mitaa ya mji mkuu wa Ugiriki, Athens leo vilisikika vipaaza sauti vilivyotangaza vidokezo juu ya kuwataka tajiri wa Ugiriki walipe deni kubwa linaloikabili nchi hiyo. Vipaaza sauti hivyo vilitangaza vidokezo hivyo huku maelfu ya watu wakiandamana kupinga kukatwa kwa mishahara ya watumishi wa serikali, kupinga kupandishwa kodi, kutoongezwa kwa pensheni na kupinga kupandishwa kwa umri wa kustaafu.

Waandamanaji walisema kwa sauti za juu kwamba watu wa Ugiriki hawapo tayari kuwalipia tajiri. Watu wameuliza jee fedha zimeenda wapi?

Kutokana na shinikizo kutoka kwa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya na kutokana na shinikizo la masoko,kuitaka Ugiriki ichukue hatua zaidi ili kuukabili mgogoro wake wa madeni, serikali ya nchi hiyo ilipitisha wiki jana, mpango wa kubana matumizi ili kupata kiasi cha Euro bilioni 4 .8 kwa kukata matumizi na kupandisha kodi.

Serikali ya Ugiriki itautekeleza mpango huo, licha ya mgomo huo mkubwa wa saa 24 unaoongozwa na jumuiya za wafanyakazi zenye wanachama milioni mbili na nusu.

Hatahivyo ingawa Wagiriki wengi wanakubaliana na serikali kwamba hatua ilizochukua ni za lazima, kwa jumla inaaminika kwamba hatua hizo zinawabana wasiokuwa na hatia, katika nchi ambamo rushwa imeshtadi na ukwepaji kodi umetanda.

Maalfu ya wafanyakazi kwenye viwanja vya ndege, na katika sekta nyingine za usafirishaji walishiriki katika mgomo kwa kuandamana.

Palitokea ghasia ambapo polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwakabili waandamaji waliokuwa wanawatupia polisi hao mawe. Watu alfu 50 walishiriki katika maandamano ya leo mjini Athens.

Serikali ya Ugiriki ilitangaza mpango wa kubana matumizi ili kuthibitisha uhakika kwamba ina uwezo wa kulikabili deni lake la Euro bilioni 300.

No comments:

Post a Comment