Thursday, February 11, 2010

WAZIRI SMZ ABURUZWA MAHAKAMANI

Waziri wa Maji, Ujenzi Nishati na Ardhi Mansour Yussuf Himid, amefunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Ardhi Zanzibar kwa tuhuma za kuchukua ardhi kinyume na sheria katika kijiji cha Buyu, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Kesi hiyo imefunguliwa na Abdallah Ahmed Abdallah, ambaye anadai shamba lake limevamiwa na waziri huyo kwa malengo ya kujengwa hoteli na nyumba za kulala wageni.

Karani Mkuu katika Mahakama ya Ardhi Zanzibar, Kassim Haji Ali, alisema kesi hiyo tayari imepangwa kuanza kusikilizwa Febuari 18, mwaka huu katika Mahakama ya Ardhi na Naibu Mwenyekiti wa mahakama hiyo, Haroub Shehe Pandu, na kwamba imefunguliwa kwa hati ya ombi la dharura.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo ya madai, Abdallah Ahmed Abdallah, shamba linalodaiwa kuvamiwa na Waziri Mansour ni mali yake aliyorithi kutoka kwa bibi yake, Mwanayamu Kombo likiwa na thamani ya Sh. milioni 12.

Abdallah ameiomba mahakama itoe amri ya kuzuia matumizi ya aina yoyote katika eneo hilo hadi mahakama itakapotoa uamuzi pamoja na kulipa gharama zote za kesi hiyo.

“Kitendo cha kufanya uvamizi na kuharibu mazingira ya shamba langu ni cha unyang’anyi na dhuluma juu yangu na kumenitia simanzi na hasara kubwa na hasa kwa kuzingatia umiliki wangu wa ardhi ni halali,” alilisisitiza katika hati yake ya kiapo ya Januari 22, mwaka huu.

Alidai kuwa shamba hilo limevamiwa na Waziri Mansour upande wa Magharibi eneo ambalo lipo pwani ya Bahari ya Hindi katika eneo la Buyu Wilaya ya Magharibi Unguja.

Alieleza kwamba ameamua kesi hiyo isikilizwe kwa ombi la dharura kwa vile tayari mdaiwa amekwishaanza kufyeka eneo hilo na kujenga ghala la kuhifadhia vifaa kwa ajili ya ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala.

Aidha ameiomba mahakama isibitishe kuwa eneo hilo limevamiwa na mdaiwa kuwa ni eneo lake na itoe amri ya kumtaka ahame na kuondosha kila kinachowekwa katika eneo hilo na kukabidhi kwa muhusika likiwa tupu.

Mdai anaiomba mahakama kuchukua hatua ya kumtaka mdaiwa alipe gharama za mahakama na kutoa amri nyingine ili kuhakikisha haki inatendeka katika kesi hiyo.

Aidha, mdai huyo aliambatanisha na nyaraka za kuthibitisha umiliki wa eneo hilo zilizotolewa na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana baada ya kurithi shamba hilo kutoka kwa bibi yake.

No comments:

Post a Comment