Friday, February 12, 2010

BABU SEYA SASA KUMALIZIA MAISHA YAKE JELA

Ile nyota iliyoanza kung'ara Desemba 3, mwaka jana wakati Makahama ya Rufaa iliposikiliza sababu 15 za rufaa ya Nguza Viking 'Babu Seya' na wanawe watatu, jana imepotea kabisa baada ya mahakama hiyo kuamuru mwanamuziki huyo na mwanae, Johnson Nguza (Papi Kocha) kuendelea kutumikia kifungo cha maisha.

Mahakama hiyo pia imewaachia huru wanawe wawili, Nguza Mbangu na Francis Nguza ambao pamoja na Baba yao 'Babu Seya' walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela, baada ya mwaka 2004 kukutwa na hatia ya makosa ya kudhalilisha watoto 10 wa kike wa shule ya msingi wenye umri kati ya miaka 6-10.

Wakili wa warufani hao, Bw. Mabere Marando alisema hukumu hiyo ya jopo la majaji Salum Massati, Mbarouk S. Mbarouk na Nathalia Kimaro inafunga kabisa hatua mbadala wanayoweza kuchukua 'Babu Seya' na 'Papi Kocha' ili kuwa huru tena.

"Kesi ikishasikilizwa na jopo la majaji watatu ni sawa na 'Full Bench' hakuna refrence 'rejea' isipokuwa kama rufaa ingesikilizwa na jaji mmoja, ninasikitika kwa hilo, lakini nashukuru kwa kuwa jamii iko upande wetu, pengine iko siku nao watasamehewa na kuachiwa," alisema Bw. Marando.

Hukumu hiyo ya rufaa ya jinai No. 56 ya mwaka 2009 ilizingatia utetezi uliotolewa na Bw. Marando kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pamoja na Mahakama Kuu zilikiuka misingi ya sheria na kupuuza ushahidi wa wateja wake katika mashitaka hayo.

Kwa kuzingatia utetezi huo, mahakama hiyo iliwafutia mashitaka 9 warufani wote, likiwemo kosa la kulawiti kwa pamoja, huku ikiwakuta na hatia ya kubaka na kubaka kwa pamoja, warufani wawili, Babu seya na Papi Kocha, hivyo kuamuru waendelee na adhabu ya awali iliyotolewa na mahakama za chini.

Mahakama hiyo ilitaja sababu za kuwaachia huru Nguza Mbangu na Francis nguza kuwa ni kutokuwepo kwa ushahidi wa kutosha juu ya ushiriki wao katika udhalilishaji huo, na kuwa mahakama za chini hazikuzingatia utetezi wao kuwa hawakuwepo eneo la tukio siku iliyotajwa.

Aidha mahakama hiyo iliukataa utetezi wa 'Babu Seya' kuwa mahakama za chini hazikuleta mashahidi walioshuhudia akifanya vitendo hivyo, na kuwa asingeweza kubaka watoto katika nyumba iliyokuwa na watu wengine muda wote ukitumika kama ukumbi wa mazoezi ya bendi yake ya Achigo.

Mahakama ilisema kutokana na ushahidi wa watoto na wa mazingira ya eneo la tukio ni wazi kuwa 'Babu Seya' asingeshindwa kufanya udhalilishaji huo, na kuwa watoto wote 10 waliomtambua wasingeweza kuongopa kwa kuwa hawakuwa na sababu ya kufanya hivyo.

Ushahidi wa 'Papi kocha' kuwa asingeweza kutenda vitendo hivyo kwa kuwa mara nyingi alikuwa safarini kwa ziara za kimuziki pia ulikataliwa na mahakama zote ikiwamo ya rufaa kwa sababu alikuwa akirejea nyumbani mara ziara hizo zinapolizika.

"Mahakama haipingi kuwepo kwa ushahidi wa safari za muziki na kuwa mrufani wa pili alikuwa akienda mazoezini, lakini hiyo hamaanishi kuwa alikuwa harudi na kukaa nyumbani, wakati alipokuwepo nyumbani asingeshindwa kufanya hivyo," ilidai sehemu ya hukumu hiyo.

Kabla ya hukumu hiyo wanamuziki hao na umma wa Watanzania ulikuwa na matumaini mamkubwa ya kuachiwa huru kwa warufani hao kutokana na hoja za utetezi kushindwa kujibiwa na upande wa mashtaka katika usikilizwaji wa rufaa hiyo.

Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na ile ya mrufani wa kwanza 'Babu Seya' kuiomba mahakama kumpima ugonjwa wa zinaa waliokutwa nao baadhi ya watoto, ambayo ingethibitisha iwapo waliingiliwa naye au na mtu mwingine, jambo ambalo halikufayika.

Baada ya hukumu hiyo baadhi ya wanasheria na wananchi hawakusita kuonesha kutoridhishwa kwao, kwa madai kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha pasipo shaka kuwa warufani ndio hasa walio wadhalilisha watoto hao 10 wa darasa la kwanza shule ya Msingi Mashujaa, Sinza Dar es Salaam.

Aidha wameiomba serikali kuwasaidia vijana walioachiwa, hasa katika suala la elimu ambapo iliwalazimu kuacha shule baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha, kwa kile walichodai walisababishiwa usumbufu na mateso wakati hawakuwa na hatia kama ilivyothibitishwa jana.

No comments:

Post a Comment