Wednesday, February 24, 2010

PONGEZI KWA SPIKA WA BARAZA LA WAWAKILISHI

Spika BLW Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho

MUWAZA inakutunukia pongezi zake za dhati kwa matamshi yako ya kizalendo ya kutetea uhuru, uwezo na nguvu za BLW kwa kutamka kwamba “Hakuna Mtu au Utawala wowote unaoweza kubadilisha maamuzi ya BLW”.

MUWAZA imefarijika na inatoa pongezi kwa msimamo madhubuti huo ambao umeweka wazi Mamlaka ya BLW na kuondosha tafsiri za migongano zilizotolewa hapo kabla baada ya Mkutano wa NEC wa karibu huko Dodoma.

Kauli hiyo ilio wazi na isio na wasi wasi wowote ya Mh. Spika wa BLW imesaidia kutolewa kwa kauli sahihi ya Rais wa Muungano wa Tanzania Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete huko Uturuki na kufuatiliwa na kauli sahihi za ndugu zetu Waziri wa Mambo ya Kimataifa wa Tanzania Mh. Bernard Membe pamoja na kusahihishwa kwa kauli sahihi ya Katibu Muenezi wa CCM Mh. John Chiligati. MUWAZA imefurahishwa kusikia kauli sahihi na zilizorekibishwa na ndugu zetu hawa wa Bara kwa kuunga mkono maamuzi ya BLW na kuitakia Zanzibar mema.

MUWAZA inamshukuru Spika wa BLW Mh. Pandu Ameir Kificho kuwa ni chachu ya kuondosha wingu la suitafahum baina ya ndugu zetu wa Tanzania Bara na Zanzibar

MUWAZA vile vile inaomba kutumia nafasi kwa kupitia kwa Mh. Pandu Ameir Kificho kuwapongeza Wawakilishi wote wa Baraza la Wawakilishi kwa kuonyesha moyo wa maridhiano, kutetea mustakbal wa Zanzibar kwa pamoja bila ya kujali mirengo ya kisiasa, kusimama kidete kwa sauti moja katika dhamana yao ya kuondosha uhasama baina Wazanzibari na kuchimba misingi ya mashirikiano kwa maslah ya Zanzibar na kuzika uadui ulio wafarakanisha Wazanzibari kwa muda mrefu

MUWAZA vile vile kwa kupitia Spika wa BLW inawapongeza Wawakilishi wote kwa kusimamia utekelezaji wa:

Kusimamisha BENDERA ya Zanzibar,
Kuanzisha NEMBO ya Zanzibar,
Kuanzisha WIMBO WA TAIFA,
Kutetea MAFUTA ya Zanzibar
Kulilinda na kulitukuza BLW
Kulinda, kuitetea, kuihifadhi na kuitengeneza KATIBA ya Zanzibar
MUWAZA kwa kupitia Mh. Spika wa BLW inatuma pongezi zake za dhati kwa Mwanashria Mkuu Mh. Iddi Pandu Hassan pamoja na timu yake ya Wanasheria kwa kutunga kwa haraka Sheria ya Kura ya Maoni Zanzibar, sheria ambayo itaifungulia Zanzibar milango ya kheri siku za usoni.

MUWAZA haitakuwa mwizi wa fadhila kwa kusahau chanzo cha michango ya maraidhiano kwa hivyo papo inachukuwa fursa hii adhiim kuwapongeza tena Rais wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Shariff Hamad kwa ushujaa na ujasiri wao kuiletea maridhiano ya Zanzibar.

Kwa niaba ya MUWAZA
Dr. Yussuf S. Salim Mwenyekiti wa Muda wa MUWAZA

Febuari 24, 2010 Gawanyo Kitaifa

No comments:

Post a Comment