Friday, February 26, 2010

GHADAFI AITISHA VITA VYA JIHADI DHIDI YA USWIZI

Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi amewataka Waislamu kuanza vita vya Jihad dhidi ya Uswizi.
Kanali Gaddafi anadai kwamba nchi hiyo imeanzisha kampeini ya kuharibu misikiti baada ya kura ya maoni nchini humo mwezi Novemba, kuidhinisha kupigwa marufuku kwa ujenzi wa minara katika misikiti ya Uswizi


Kanali Gaddafi pia ametaka waislam kote duniani kususia bidhaa za Uswizi. Kiongozi huyo wa Libya ameyasema hayo mjini Benghazi wakati wa kuadhinisha siku ya kuzaliwa kwa Mtume Mohamed.

Mwezi Novemba mwaka uliopita, wapiga kura nchini Uswisi waliidhinisha sheria ya kupiga marufuku ujenzi wa minara nchini humo, kupitia kura ya maoni. Uamuzi huo wenye utata unazusha hofu juu ya uwezekano wa kuzuka uhusiano mbaya kati ya Uswisi na jamii ya Kiislamu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Uswisi, Lars Knuchel alikataa kuzungumzia wito huo uliotolewa na Gadhafi wa kuanzishwa vita vitakatifu dhidi ya nchi hiyo.

Kumekuwa na mzozo wa kidiplomasia kati ya Libya na Uswizi tangu mwana wa Kanali Gaddafi pamoja na mkewe kukamatwa nchini humo kwa tuhuma za kumdhulumu mjakazi.

Wiki iliyopita, Libya iliwapiga marufuku raia wa muungano wa Ulaya kupata vibali vya kuzuru nchi hiyo. Hiyo ilifuatia hatua ya Uswizi kutoa orodha iliyowawekea vikwazo raia 188 wa Libya, ikiwa ni pamoja na Kanali huyo na watu wa jamii yake.

No comments:

Post a Comment