Saturday, February 20, 2010

WALIONUSURIKA MAUAJI MUSOMA WASIMULIA

Baadhi ya majeruhi katika tukio la mauaji ya kinyama ya watu 17 katikati ya wiki hii katika Manispaa ya Musoma, mkoani Mara wamesema wauaji walikuwa wamejiandaa na inaonekana walikuwa wanawafahamu kila mmoja.

Aidha wamesema wauaji waliamini hata wao wamekufa.

Moris Mgaya (40), aliyepoteza mke na watoto wake watano katika mauaji hayo, alisema wauaji walikuwa wanamfahamu vizuri.

Akizungumza kwa shida kitandani katika moja ya wodi za Hospitali ya Mkoa wa Mara mjini hapa, Mgaya alisema wauaji walikuwa wakimjua vizuri kwa kuwa walimtaja kwa majina yake likiwemo lile lisilojulikana na wengi la Susi (kunguni) wakati wakifanya mauaji hayo nyumbani kwake.

Katika tukio hilo mke na watoto wa Mgaya waliuawa kwa kucharangwa mapanga huku yeye mwenyewe akiachwa na majeraha makali, kutoka kiunoni hadi miguuni.

Mgaya alisimulia kuwa wauaji hao ambao alishindwa kuwatambua kutokana na kuvalia makoti makubwa na kutumia tochi waliyoitumia kuwamulika, walimtaka atoe pesa na aliposema hana walimtaja kwa jila lake la Susi na kumwambia kuwa watamuua endapo hatatoa pesa hizo. Alisema kuwa wauaji hao walichukua fedha taslimu Sh. 200,000 alizokuwa amezihifadhi sandukuni na zingine Sh. 50,000 alizoweka katika suruali yake aliyokuwa ameitundika katika kamba kabla ya kulala.

Akizungumzia kuhusu taarifa za mkewe na mtoto wake waliokuwa katika chumba kimoja, Mgaya alisema kuwa hadi sasa bado hajaambiwa kama mkewe na mtoto wake walifariki dunia katika tukio hilo la mauaji lililohusisha jumla ya nyumba tatu za wana ndugu wa ukoo mmoja.

"Hadi sasa sijaambiwa kama mke na mtoto wangu walifariki dunia katika tukio hilo, bado wamenificha ingawa mimi nahisi kuwa walishakufa," alisema Mgaya huku akifuta machozi kwa kutumia kitambaa alichokuwa amekishika mkononi.

Naye majeruhi mwingine, Maximilian Robert (20), ambaye amelazwa wodi moja na Mgaya, alisema kuwa alikatwa mapanga katika nyumba nyingine ambayo alikuwa amelala yeye, bibi yake na mtoto mwingine mdogo.

Robert alisimulia kuwa bibi yake alikatwa mapanga na kuuawa, na kwamba yeye alinusurika baada ya wauaji kumkata mapanga begani na mkononi na kisha kumwacha wakidhani kuwa alikuwa ameshafariki.

Jumla ya watu 17 waliuawa katika tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Jumatatu, mbapo familia zilizokumbwa na tukio hilo na idadi ya watu waliouawa ikiwa katika mabano ni ya Mzee Kinguye (8), Moris Mgaya (6), na familia ya mzee Mgaya Nyarukende (3).

Akizungumza katika Hospitali ya Mkoa wa Mara jana, Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali hiyo, Benadecto Mwijarubi, alisema kuwa majeruhi hao ukiondoa Maria Kawawa, hali zao zinaendelea vizuri.

Mwandishi wa habari hizo alipomtembelea Maria, alishindwa kuongea naye baada ya kumkuta akiwa bado katika maumivu makali kitandani mwake huku akiwa amefungwa bandeji kichwani na sehemu nyingine za mwili pamoja na kufungwa bandeji (pop) katika mkono wake wa kushoto.

Jeshi la Polisi mkoani hapa limesema kuwa tayari linawashikilia watuhumiwa sita kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo, huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurence Masha, aliyefanya ziara ya mkoani hapa juzi kwa ajili ya kufuatilia tukio hilo akisisitiza kuwa wote walioshiriki katika mauaji hayo lazima wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Waziri Masha aliyasema hayo juzi alipowatembelea wafiwa na baadaye majeruhi katika Hospitali ya Mkoa wa Mara mjini hapa.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mstaafu Enos Mfuru, amekuwa akiwahimiza wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Robert Boaz, tangu kutokea kwa mauaji hayo amekuwa akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi limejipanga katika maeneo yote ya mkoa huo kufanya msako wa kuwatia mbaroni watu waliohusika na tukio hilo ambalo limeandika historia mkoani humo.

No comments:

Post a Comment