Wednesday, January 27, 2010

KICK BOXING BADO NI MARUFUKU ZANZIBAR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesisitiza msimamo wake wa kutoruhusu mchezo wa ngumi za mateke (kick boxing) katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Naibu Waziri wa habari Utamaduni na Michezo Mahmoud Thabit Kombo amewambia wajumbe wa Baraaza la wawakilishi katika kikao kinachoendelea Maisara Mjini Zanzibar kwamba Serikali haijaruhusu mchezo huo hapa nchini .

Mwakilishi wa Jimbo la Chambani (CUF) Abass Juma Muhunzi alisema kwa kuwa vijana wa Zanzibar sasa wanashiriki katika mashindano ya judo na ngumi za mateke ( kick boxing ) ambayo hayana tafauti sana na mchezo wa ngumi za kawaida (boxing ) ni kusema sasa mchezo wa ngumi unaruhusiwa kuchezwa Zanzibar.

Waziri Kombo alisema ipo tafauti kubwa kati ya mchezo wa judo na mchezo wa ngumi kwa kuwa katika mchezo wa judo wachezaji hawapigani ngumi wala mateke isipokuwa wanaoneshana nguvu na mbinu katika kukamatana na kuangushana kwenye kiwanja kilichowekwa maalum matandiko malum ya kuangukia

Mwakilishi wa nafasi za Wawanawake (CUF) Zakia Omar Juma alisema kwa kuwa mchezo wa ngumi za mateke ulipigwa marufuku na mzee Karume ili kulinda wananchi wasipigane kwa wakati huo kwa nini hivi sasa bado suala hilo linaekewa pingamizi na serikali hali ya kuwa baadhi ya Wazanzibar wanashiriki mchezo huo nje ya nchi na kushinda

Naibu Waziri huyo alisema suala la kukatazwa ngumi za mateke lilipingwa marufuku na muasisi wa kwanza wa Taifa la Zanzibar ambaye ni rais wa kwanza wa visiwa hivi marehemu mzee Abeid Amani Karume hivyo marufuku hiyo kwa sasa haiwezi kuondolewa hadi hapo ionekane kuna haja hiyo

Kombo alisema Wazanzibari wanaokwenda kushiriki mchezo huo nje ya nchi hawakatazwi wala hawawezi kuingiliwa uhuruwao huo lakini Serikali haiwasindikizi wanapokwenda katika mashindano wala kuwapokea rasmi kwa kuwa mchezo huo bado ni marufuku kwa Zanzibar.

Hata hivyo alisema iwapo wananchi watataka kuondosha marufuku hiyo ni suala la wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuleta mswada Barazani juu ya suala hilo na wajumbe kwa mamlaka waliyopewa wanaweza wakachangia na wakitaka sheria kufanyiwa marekebisho na haja ya kuuondosha kama itawezekana kufanyika hivyo.

No comments:

Post a Comment