Friday, November 6, 2009

WAZANZIBARI TUNATAKA DOLA YETU, SIO HATI YA MUUNGANO

Umoja wa Wazalendo

“Na shikamaneni kwa Dini ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane…”.

Wazee wetu, Ndugu zetu;

Assalaamu Alaaykum,

UMOJA, UHURU, UADILIFU

KUVAMIWA NA KUMEZWA DOLA HURU YA ZANZIBAR

Kwa Rehma za Mwenyezi Mungu na juhudi za Wazalendo, Zanzibar ilipata Uhuru wake, Disemba kumi, 1963 na kujiunga na Umoja wa Mataifa Disemba kuminasita, 1963; ikiwa ni Dola Huru Kaamili yenye Kiti chake na Bendera yake, na kila lake.

Siku 33 baada ya hivi kupata Uhuru wetu, yaani Januari 11, 1964 jeshi la Nyerere liliivamia Zanzibar na kuleta mauwaji ambayo hayajapata kutokea katika historia ya Zanzibar. Mara tu baada ya mavamizi haya, April 24, hiohio 1964, Nyerere alitufanyia Aprilfool Wazanzibari kwa kuleta zile “Articles of Union, 1964”, hivyo kwa kisingizio cha huu wenyekuitwa muungano wakaimeza Nchi yetu kikamilifu. Kutokana na uovu huu, ndipo Waziri Mkuu wa Tanganyika, Mhishimiwa Pinda kutangaza na kusisitiza kwamba “Zanzibar si Nchi”. Tangu sikumosi ya khiyana kuu hii, Tanganyika ilioifanyia jirani yake Zanzibar; Wazalendo wa Kizanzibari wamekikanya kitendo kiovu hiki na kudai kurejea Dola Huru Kaamili ya Zanzibar.

Mara tu baada ya uovu huu, mengi yameandikwa, na mengi yamesemwa na watu mbalimbali; kukhusu “uhalali wa huu wenyekuitwa muungano” (the legality of the union). Wote hao, hapana hata mmoja aliekuwa na nguvu za hoja kuhalalisha haramu hii, haramu ya kuvamiwa Zanzibar na haramu ya kumezwa Dola ya Zanzibar.

Mjadala umeendelea kukhusu kuwepo khati ya muungano iliosainiwa na Mzee Karume pamoja na yeye Mwalimu Nyerere, wawili ambao ndio waliofanya khiyana hii. Mpaka hivijuzi, sirikali ya Zanzibar na sirikali ya Tanganyika wameendelea kukiri kwamba hakuna khati iliosainiwa na mabwana wawili hawa. Hali yenye kushangaza ni hivi ghafla kuona maneno haya yanasemwa na mkoloni mvamizi, Tanganyika:

“SERIKALI imesema mkutano ujao wa bunge itagawa kwa wabunge pamoja na kuweka katika maktaba mbalimbali pamoja na makumbusho Hati ya Muungano kwa kuwa ni haki ya kila mtu kuufahamu mkataba huo……….”.

Wazanzibari, hatuna mjadala kukhusu khati ya muungano, ipo au haipo; au uhalali wa muungano. Kwa Wazanzibari la asili na la hakika ni kwamba hapakuwa na muungano, bali ni kumezwa Dola Huru ya Zanzibar. Kwahivyobasi, Wazanzibari wanachotaka na wataendelea kukiwania mpaka tukipate, ni kurejea Dola Huru Kaamili ya Zanzibar. Irejee kama ilivyokuwa ilipopata Uhuru wake na kujiunga na Umoja wa Mataifa, Disemba, 1963 ikiwa ni Dola Huru Kaamili, yenye Bendera yake na Kiti chake sawa na Dola nyengine yoyote ile katika Umoja huu wa Mataifa.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu, Subhaanahu wa Taáala atujaalie kila la kheri na atuepushe na kila shari; na atujaalie ufunguzi wa karibu, Aamyn Yaa Rabbi.

Wa Billahi Tawfiiq

Umoja wa Wazalendo

Zanzibar,

Ijumaa Novemba 06, 2009

“…. وأمرهم شورى بينهم ……”.

“….., na mambo yao yakawa ni kwa kushauriana baina yao,…..”.

No comments:

Post a Comment