Monday, October 26, 2009

WACHAPWA BAKORA 25 KWA KUANGALIA VIDIO ZA NGONO KWENYE SIMU

Wanaume wawili wa nchini Somalia wamecharazwa bakora 25 mbele ya kadamnasi ya watu na kisha kutupwa jela siku 15 baada ya kukamatwa wakiangalia video za ngono kwa kutumia simu zao za mkononi.

Maafisa wa ulinzi wa kundi la Al shabab waliwafumania vijana hao wakiangalia video za ngono kwa kutumia simu zao siku ya ijumaa na walicharazwa bakora hizo siku ya jumamosi katika mji wa kusini mwa Somalia wa Kismayo unaotawaliwa na Al shabab.

"Vijana hawa wawili walikamatwa wakiangalia video za ngono kwa kutumia simu zao na baada ya kukiri makosa yao wameadhibiwa kwa mujibu wa sharia za kiislamu", alisema Sheikh Omar Mohamed, afisa wa mambo ya dini wa Al shabab alipokuwa akiongea na shirika la habari la AFP.

"Kila mmoja wao alichapwa bakora 25 na watatumikia siku 15 jela kwa vitendo vyao viovu walivyovifanya", aliongeza Sheikh Mohamed.

Wakazi wa eneo hilo walithibitisha kucharazwa bakora kwa vijana hao.Kundi la Al shabab linatumia sharia za kiislamu katika maeneo wanayoyatawala. Wezi hukatwa mikono au miguu kulingana na kosa lenyewe na wazinzi hucharazwa bakora.

No comments:

Post a Comment