Monday, October 26, 2009

MAMBO KANGAJA HUENDA YAKAJA

Kihistoria Zanzibar ni nchi ya kale sana . Wataalamu wa historia wanatwambia kwamba hii ni mojawapo ya Dola kongwe na ya asli (ancient state) katika Ulimwengu. Na kwa kuwa ni kisiwa kilichozungukwa na bahari, basi kilibahatika kutembelewa na watu kutoka nchi mbali mbali.

Nyaraka za wasafiri wa kale walioitembelea Zanzibar zinatueleza kuwa Wasafiri kutoka Misri na Ugiriki walifika Zanzibar mnamo mwanzoni mwa Karne ya Tano baada ya kuzaliwa Nabii Issa. Wasafiri wengine kama Ibn Batuta na Ibn Mas-ud pia waliitembelea Zanzibar na kuandika khabari zake kama walivyoiona katika dahari hizo.

Wengine wengi walifika katika Visiwa hivi wakitumia Pepo za Musim (Monsoon Winds) kutoka sehemu za Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Waarabu na nchi za Kusini ya Arabuni, Bara Hindi, Mashariki ya Mbali khasa Uchina na Visiwa vya Java na Sumatra (ambavyo sasa ni Indonesia ) na wote hao walivutiwa na Zanzibar .

Katika yaliyowavutia ni kuiona Zanzibar kuwa ni nchi yenye ardhi nzuri yenye miti mingi na maji safi ya kunywa ya kutosha pamoja na bandari nzuri na salama ya kuegesha vyombo vyao na kupata mahitajio yao mengine.

Baadaye wengi katika wasafiri hawa waliovutiwa sana na mandhari nzuri na bashasha ya watu wake walifanya maskani yao hapa Zanzibar . Na hapo ndipo yalipoanza maingiliano makubwa kati ya wageni na wenyeji.

Hayo tuliyoyaeleza hapo juu ni historia. Wanaoishi sasa katika Karne hii hawayajui. Yamesalia katika kumbukumbu za taarikh ya kale. Lakini sisi wazee tumediriki kuyaona baadhi ya mambo haya ambayo wengi katika vijana wa leo hawayajui.

Kwa hivyo, si vibaya kuwazungumzia vijana ijapokuwa kwa uchache tu. Kwa hakika, sifa za Zanzibar ni zile zile walizotuhadithia wasafiri wa kale. Na katika kusifu wamesema waliyosema kwamba: Visiwa vya Zanzibar hewa yake ni safi , ardhi yake ina rutba nyingi yenye miti mingi ya namna kwa namna na yenye maji safi ya kunywa. Wenyeji wake ni watu wazuri, wachangamfu, wenye hishma na wanaopenda wageni.

Hizo ni sifa iliyopewa Zanzibar na watu wake. Tuliyoyaona sisi ni namna ya watu wa Zanzibar wa mjini na mashamba walivyokuwa wakipendana, wakihishimiana na wakisaidiana hata ikawa la mmoja wao ni la wote, likiwa la msiba au la furaha.

Kutokana na hayo, neema ikazagaa katika kila pembe ya Visiwa hivi. Hapakuwa na chuki, bughudha wala utengano wa aina yoyote baina yao kama ilivyo sasa, mambo ambayo sasa yamezipeperusha neema zote tulizozishuhudia wakati huo.

Katika zama zetu, watoto nao pia walikuwa wa watu wote, wakitunzwa vilivyo na wazee wote wa mtaa bila ya kuwabagua. Watoto wote wa umri mdogo walihudhuria katika vyuo vya Qur-ani mitaani pamoja na baadaye kwenda skuli pamoja.

Haya yalisaidia sana katika kuwafanya watoto hao wajuane kama walivyo wazee wao na kuwahishimu wazee.

Watoto wadogo walihifadhiwa vizuri ili wakulie katika malezi mazuri. Watoto wote iliwabidi warejee majumbani likichwa jua. Baada ya hapo, watoto wakubwa ama wakenda miskitini kujifunza dini au wakibaki majumbani mwao kudurusu masomo yao . Ilikuwa hapana ruhusa watoto kuzurura ovyo majiani mpaka saa za usiku kama ilivyo hivi leo na matokeo yake tunawapoteza vijana wetu wanaotumbukia katika kila aina ya balaa lisilokuwa na tija wala kheri kwao.

Wakati huo, watu wote wakiweza kulala majumbani mwao kwa usalama pasina khofu ya kuingiliwa na majambazi wa kupora mali yao , kuua au hata kuwanajisi watoto vigori kama ilivyo hivi leo. Huo ulikuwa wakati ambao wafanya biashara na wenye maduka walikuwa na usalama wa mali zao na hawakuwa wakilazimika kujifungia ndani kwa milango ya chuma kama wanyama waliomo katika “zoo”.

Uko wakati ule? Wakati akinamama walivyoweza kujifaragua na mapambo yao ya dhahabu kwenda katika mashughuli ya arusi bila ya wasiwasi wa kushambuliwa na wahuni wa kuwavunjia hishima zao na kuwapora mapambo yao .

Wakati wenye mashamba, wakulima na wafugaji, walipokuwa na uhakika wa usalama wa mazao yao na wanyama wao.
Wakati majenzi ya nyumba yalipokuwa yakifuata rasim na ramani zilizowekwa na sheria. Magari makubwa na madogo yakifuata sheria za barabarani ili kuepusha ajali za kila siku na wapitao njia kusalimikana maisha yao .

Wakati maji ya mifereji yakihifadhiwa ili kuepusha maradhi mabaya yasiwapate watu.
Wakati lugha yetu ya Kiswahili iliyojaa ufasaha wa tungo na tenzi za wataalamu na mabingwa wa fani ya lugha yetu ilipohifadhiwa na kuhifadhika bila ya kuingiliwa na maneno na misemo isiyo na asli yoyote ya lugha ya Kiswahili.

Basi haya tuliyoyaeleza hapa na mengi mengineyo ndiyo yanayotufanya wazee tuliyoijua Zanzibar ya zama zile kulalamika na kusononeka. Tumebaki kujiuliza ziko wapi kheri, tijara na neema tulizoziona? Iko wapi salama na amani na adabu zetu za asli pamoja na ustaarabu wa Waswahili? Yote yameondoka. Zanzibar imebaki inaning’inia.

Kutokana na hayo basi, ni wajibu wa kila mwananchi mwenye ghera na uchungu wa Visiwa hivi “wanasiasa, wasomi, walimu, masheikh na wazee mitaani “kushirikiana pamoja na kusimama kidete kuyahuisha yale yote yaliyonasibishwa na mema na mazuri ya nchi hii. Ni wajibu wetu kuwarithisha watoto wetu nchi yao ikiwa na utukufu wake ule ule wa asli uliyoifanya Zanzibar isifike na kutajika katika kila pembe ya Ulimwengu huu.

Na haya si ndoto za Alinacha! Yanawezekana kabisa ikiwa tutakuwa na nia ya dhati ya kuyasimamisha.

Najua kuwa tunaposimulia haya, vijana husema kutujibu masikitiko yetu kuwa “Ya Kale Hayapo”. Lakini na sisi wazee tuliyoiona Zanzibar wakati wa hadhi na utukufu wake tunawaambia: “Mambo Kangaja Huenda Yakaja”.

No comments:

Post a Comment