Wednesday, October 28, 2009

MAISHA YA SKULI ZAMANI

Walimu wakiwapenda wanafunzi
Na Abdulla Al-Harthy

Kuna kitu kimoja au viwili mimi siwezi kusahau juu ya maisha yaliokuwepo Visiwani wakati ule wa neema, utulivu na sharaf zilizokuwepo.

Kimoja ni wakati wa masomo na walimu wetu tuliokuwa nao wa kila aina na kila mchaganyiko, pamoja na jitihada zao za kutusomesha.

Ninachokikumbuka mimi ni juu ya walimu wetu mbali mbali, akiwemo Maalim Ibrahim Kassim ambaye alikuwa mwalimu wa hesabu huko Mnazi Mmoja. Alikuwa akitaka kukupiga huwa anatafuna ulimi na ukikinga anakwambia upo tyari kupigana? Wakati huo huwa huku anakunja koti lake na kukutandika magumi.

Maalim Aboud Jumbe alikuwa katika walimu waliosifika kwa Kiingereza huko Mnazi Mmoja Secondary School. Alikuwa na baiskeli yake aina ya Humber. Akitoka kazini na kurudi nyumbani, wakati mwengine alikuwa akinipakia. Hayo yalikuwa mapenzi ya kweli kati ya walimu na wanafunzi wa zama zetu.

Kina Maalim Hija Saleh na Malim Uledi Jabu walikuwa ni katika walimu mahodari kabisa kwa hesabu katika skuli za msingi (Primary School).
Maalim Uledi Jabu alikuwa sifa zake ni kupenda kuwasaidia wanafunzi wake. Yeye alikuwa akisomesha Historia na Kiswahili.

Alikuwa anavaa koti na kanzu na kunako koti lake, kwa kawaida , kulikuwa hakukosi kichwa cha samaki au cha kuku.

Tulipohamia Shimoni School (hivi sasa kuna Uwanja wa Mao Dze Dung) kulikuwa na kina Maalim Hilal, Ahmed Zahran, Seyyid Ahmed Mansab, Hassan Mshangama na Mohammed Aley.
Tulikuwa tumegawiwa siku za uhamisho magurupu mawili. Kundi moja likenda Kupaz (Coopers – sasa Uwanja wa Maisara) na sisi tukaenda Mashimoni. Mimi nilikwenda na wenzangu kunako mabanda ya makuti – juu kwenye paa na ukutani pia.

Pamoja na kuwa na mabanda mengine ya makuti juu na ukuta wa mawe chini, Sh. Abdulla Saleh Farsy alikuwa akitusomesha Kiarabu na Dini.

Saa nne tulikuwa tukimfukuzia Said Njugu kununua njugu, na kina mama walikuwa wakiuza mbaazi, na mbatata za urojo. Wakati huo kiwanja cha mpira kilichopo Shimoni ndio kilikuwa kinafukiwa, kwani kwanza kulikuwa na jaa la taka la mji.

Gari iliokuwa ikija skuli ni moja tu ambayo, ilikuwa tunaiita gari la mabati kutoka Nyumba ya Moto (nyumba ambayo wakiishi watoto waliolelewa na Mfalme). Kulikuwa hakuna hata apandae baiskeli, na hiyogari ilikuwa ikipandisha wanafunzi hata tulikuwa tukiionea huruma.

Mimi sijawahi kuipanda, lakini ilichukua mtoto yeyote yule wa Kisiwani aliokuwa akisoma skulini hapo.

Kulikuwa wakati huo hakuna Mzanzibari anayesoma skuli za nje wala za mapesa. Skuli za nje zilikuwa ni za Comorian na ya misheni iliopo nje ya Kupaz.

Sijui huo ubepari unaozungumzwa leo ulionekana vipi wakati kulikuwa hakuna anayeweza kumiliki hata kumpeleka mtoto wake skuli kwa gari, wakati ambapo kulikuwa hakuna wamiliki wa magari na ikiwa walikuwepo walikuwa hawajai mkononi.

Inasikitisha kuona kuwa Uzanzibari ule sasa haupo na umemezwa na hali ya sasa kutokana na mambo yalivyobadilika.
Mimi nashukuru kuwa ni miongoni mwa tuliojifaidia kuona yaliopita ambayo ni ya kutafakhari nayo, pia tunaomba Mungu ayarudishe kama yalivyokuwa.

Tulikuwa tunapewa mabuku, wino, nibu, dawa za homa tuliokuwa tukila kila wiki. Daktari wa meno, Dk. Soud alikuwa akitupitia kila skuli mwaka mara mbili na pia wakati huo kulikuwa hakuna sare za skuli.

Sare zimeanza Skuli ya Darajani ambako mimi sijasoma. Aghlabu wanafunzi tulikuwa
tukivaa kanzu au suruali ndefu au fupi (kipande).

Lakini kulikuwa na feshini ya kuvaa kaki na shati jeupe au fulana ya navy blue kutoka dukani kwa Maalim Abdulrauf lililokuwepo hapo Kinu cha Taa, Malindi.
Ukivaa hivyo ndio unaonekana umesha-staff kimji wakati ule.

Kulikuwa hakuna makuu. Pamoja na viatu vya mpira vyeupe miguuni basi mambo hapo yamejishia. Ndugu zetu wa kike wote walikuwa Skuli ya Rahaleo na ya Forodhani.

Wanafunzi wote wa kike walikuwa kunako skuli hizo mbili za mjini na walikuwa wanatoka watokako kwa miguu hadi skuli. Awe atavyokuwa lazima autwange kwa miguu (Ubepari huo!).
Mchana utaona wasichana mikoba yao ya ukili begani . Wakubwa na mabuibui yao na wadogo na magauni yao au na ushungi wao (mmeziona skuli ziliopo leo mjini?).

Kabla ya Skuli ya Rahaleo kujengwa mwisho wa miaka ya 40 wanafunzi wa kike walikuwa wakisoma Forodhani, nyuma ya Msikiti wa Ijumaa wa Forodhani, uliopo nyuma ya Palace (Kasri ya Mfalme).

Walimu, pamoja na wasomi wote wa kike wametokea hapo au kuanzia hapo.

Mungu aibariki Zanzibar na awaoneshe watoto wetu yale tuliyoyaona sisi wazee wao.

No comments:

Post a Comment