Wednesday, July 14, 2010

UNAIDS YATOA RIPOTI YAKE

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi yamepungua hasa miongoni mwa vijana.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, UNAIDS limesema kuwa vijana barani Afrika wanaongoza katika mapinduzi ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi kutokana kubadilika kitabia ikiwemo na kufanya ngono salama na kupunguza idadi ya wapenzi.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa hii leo na Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, UNAIDS, maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi yamepungua miongoni mwa vijana katika nchi 16 kati ya 25 ambazo ziliathiriwa vibaya na ugonjwa huo. Utafiti wa shirika hilo umebaini kuwa nyingi ya nchi hizo ziko katika nafasi nzuri ya kufanikiwa kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi kwa asilimia 25 miongoni mwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Ripoti hiyo imefafanua kuwa vijana wameweza kuonyesha kuwa wanaweza kuwa mawakala wa mabadiliko katika mapinduzi ya kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, UNAIDS, limezitaka nchi mbalimbali duniani kote kujifunza kutokana na mafanikio hayo na kuandaa mipango madhubuti kuhusu elimu ya afya na kujamiiana, uwepo wa vifaa vya kupima virusi vya Ukimwi na kupatikana kwa urahisi vifaa vya kuzuia maambukizo ya virusi hivyo kama vile condom za kiume. Inakisiwa kuwa vijana milioni tano duniani kote wenye kati ya umri wa miaka 14 hadi 24 wanaishi na virusi vya Ukimwi na karibu asilimia 80 ya vijana hao wanaishi katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara. Ripoti hii iliyotolewa kabla ya mkutano wa dunia utakaojadili ugonjwa wa Ukimwi wiki ijayo huko Vienna, imegundua kuwa kiwango cha virusi vya Ukimwi kimepungua miongoni mwa vijana katika nchi 16 kati ya 25 zilizoathiriwa vibaya na virusi hivyo, ikiwemo Kenya, ambako kumekuwa na mabadiliko ya asilimia 60 kati ya mwaka 2000 na 2005.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa Botswana, Ivory Coast, Ethiopia, Kenya, Malawi, Namibia na Zimbabwe zote zimefanikiwa kufikia lengo lililokubaliwa mwaka 2001 la kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2010.

Aidha, Burundi, Lesotho, Rwanda, Swaziland, Bahamas na Haiti pia ziko katika mwelekeo wa kulifikia lengo hilo. Utafiti wa shirika hilo umegundua kuwa chanzo kikubwa cha kupungua kwa maambukizi ya virusi hivyo ni vijana kubadilika kitabia.


Vijana katika nchi 13 kati ya 25 wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kabla ya kujiingiza katika vitendo vya ngono na katika zaidi ya nusu ya nchi 25 vijana wamekuwa wakichagua kuwa na wapenzi wachache. Matumizi ya condom za kiume pia yamechangia kupungua kwa maambukizi hayo, huku nchi 10 zikiripotiwa kutumia zaidi condom hizo miongoni mwa wanawake, na nchi 13 condom hizo zikitumiwa zaidi na wanaume. Cameroon, Tanzania na Uganda zimeripotiwa kuongeza matumizi ya condom kwa wanawake na wanaume. Mwezi Novemba mwaka uliopita Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, UNAIDS, lilikadiria kuwa kiasi watu milioni 33.4 duniani kote walikuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi.
.

No comments:

Post a Comment