Wednesday, July 7, 2010

SEMENYA APATA IDHINI KUREJEA MBIEONI


Mwanariadha wa Afrika Kusini Castor Semenya amepata idhini kutoka shirikisho la riadha duniani IAAF kurejea kushiriki mashindano ya riadha kama mwanamke.

Semenya mwenye umri wa miaka 19, hajashiriki mashindano yoyote katika muda wa karibu mwaka mmoja kutokana na utata kuhusu jinsia yake, na amekuwa akisubiri matokeo ya kubaini ikiwa ni mwanamme au ni mwanamke.

Utata huo ulizuka Agosti mwaka uliopita kwenye mashindano ya mbio za ulimwengu mjini Berlin wakati Semenya aliposhinda mbio za mita 800 kwa wanawake huku akimwacha mpinzani wa karibu kwa zaidi ya mita 20.

Kufuatia utata huo ambao pia ulikuwa umejitokeza kwenye mashindano ya riadha kwa vijana barani Afrika, IAAF iliagiza uchunguzi kufanyika kubaini jinsia ya Semenya ili kuamua ikiwa ataruhusiwa kuendelea kushindana kama mwanamke.

Taarifa kutoka IAAF imethibitisha uamuzi huo wa kumpa idhini Semenya kuendelea kushiriki katika mashindano ya riadha kama mwanamke, baada ya kamati ya wataalamu wa afya kukamilisha uchunguzi wake.

Taarifa hiyo imesema, ''Mchakato ulioanzishwa mwaka 2009 kuhusu Castor Semenya umekamilika. IAAF inakubali kauli ya kamati ya wataalamu wa afya kwamba anaweza kuanza kushiriki mashindano ya riadha mara moja.''

Hata hivyo taarifa hiyo imesema maelezo ya afya kuhusu jinsia ya Semenya yatabakia kuwa siri, na IAAF haitasema chochote kuhusu swala hilo.

Kufuatia idhini hiyo Semenya anaweza kuamua kushiriki mashindano ya kimataifa ya vijana nchini Canada baadaye mwezi huu, lakini huenda akapendelea kuanza kujiandaa kwa michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika mjini New Delhi, India mwezi Oktoba.

Mjini Berlin Semenya alishinda mbio za mita 800 kwa muda wa dakika moja sekunde 55.45, na kumwacha kwa karibu mita 20 aliyekuwa bingwa wa dunia wakati huo Janeth Jepkosgei kutoka Kenya.

Rekodi ya dunia ya mbio za mita 800 ni dakika moja sekunde 53.28 iliyowekwa na Jarmila Kratochvilova wa Jamhuri ya Czech mwaka 1983 na haijapata kuvunjwa tangu wakati huo.

Kuidhinishwa kwa Semenya kuendelea kushiriki mbio za mita mia nane kama mwanamke huenda kukatoa fursa ya rekodi hiyo kuvunjwa.

1 comment:

  1. Mwanariadha wa Afrika Kusini Castor Semenya
    ni Africa kusini au umekosea

    ReplyDelete