Friday, July 23, 2010

KOSOVO HAIJAKIUKA SHERIA YA KIMATAIFA

Mahakama ya Haki ya Umoja wa Mataifa imesema hatua iliyochukuliwa na Kosovo kujitenga na Serbia haijakiuka sheria ya kimataifa. Jaji Mkuu wa mahakama hiyo ya kimataifa iliyoko The Hague, Uholanzi, Hisashi Owada, alitoa uamuzi huo usio na mafungamano ambao huenda ukawa na athari zake miongoni mwa makundi yanayopigania kujitenga kote ulimwenguni. Kosovo imekuwa inatambuliwa na mataifa 69 kama nchi huru, ikiwemo Marekani na mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton ameupokea kwa furaha uamuzi huo akisema kuwa umoja huo uko tayari kuzisaidia Serbia na Kosovo kufanya mazungumzo ya kuimarisha nguvu zao za kujiunga na umoja huo. Rais wa Serbia Boris Tadic alisema kuwa nchi yake haitabadilisha sera zake kuelekea Kosovo na serikali sasa inazingatia kuchukua hatua zaidi. Serbia na Urusi ziliyaongoza mataifa mengine kadhaa kutoitambua Kosovo kama taifa huru.

No comments:

Post a Comment