Hotuba iliyotolewa kwa waandishi wa Habari na Bwana Muhammad Yussuf kuelezea azma yake ya kutaka kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi katika ukumbi wa EACTROTANAL siku ya Alkhamisi tarehe 24 Juni 2010
SOMENI KWA FURAHA!!
AMUR
Ndugu Wana-habari,Wazanzibari wenzangu,Mabibi na Mabwana, Kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kunipa nguvu, afya njema na uhai wa kuwepo hapa leo. Pia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Chama Cha Mapinduzi kwa kunipa fomu hii adhimu inayonipatia nafasi ya kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kama tujuavyo, kipindi cha pili na cha mwisho cha uongozi wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Amani Abeid Amani Karume, kitamalizika mnamo mwezi Oktoba 2010. Kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, Mheshimiwa Karume hatoweza tena kugombea kipindi kingine cha miaka mitano. Katika hali hii, ni jambo la kawaida kabisa kujitokeza wana-CCM wengine wengi tu kugombea nafasi itakayowachwa wazi na Mheshimiwa Rais Karume. Na vile vile, ni jambo la kupongezwa kabisa kuona kuwa mara hii jumla ya wana-CCM 11 wamejitokeza kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama chetu; mimi nikiwa mmoja miongoni mwao.
Huu ni uthibitisho tosha na wa dhahiri kuwa Chama cha Mapinduzi kinaheshimu misingi ya demokrasia ya kweli ndani yake yenye lengo la kuwapa fursa wanachama wake kugombea nafasi yoyote katika chama na serikali zake. Ni kutokana na hali hii basi, na kwa madhumuni ya kutumia haki yangu ya kidemokrasia kwa mujibu wa katiba ya chama chetu na ile ya Zanzibar, ndiyo sababu ya kwanza iliyonisukuma kuchukua fomu kugombea nafasi hii katika uongozi wa taifa letu.
Kwa hivyo, kati ya wanachama wetu hao 11, Hamlashauri Kuu ya Taifa itamteua mgombea mmoja tu miongoni mwao kukiwakilisha chama chetu katika uchaguzi ujao. Napenda kukiri kwa dhati kabisa kuwa wagombea wote hao ni wazuri na wenye kila sifa zifaazo, uwezo na uzoefu wa kutosha, kwa mujibu wa katiba ya chama chetu na katiba ya Zanzibar, kushika wadhifa wa urais wa Zanzibar. Hii inamaanisha kuwa sifa za wagombea sote sisi sio jambo la mjadala mkubwa; kwani sote ni wanachama hai wa chama chetu na wengine wameshikilia nyadhifa mbali mbali katika chama na serikali kwa muda mrefu na kujulikana sana. Mimi sijapata kushika wadhifa wowote ule wa uongozi katika chama; lakini nimeshika nyadhifa mbali mbali katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Maelezo zaidi yamo katika CV yangu.
Lakini, kutoshika wadhifa wowote ule wa uongozi katika chama hauninyimi sifa za kugombea wadhifa wa Urais wa Zanzibar. Kwa mujibu wa katiba ya CCM, inatosha tu, pamoja na sifa nyingine, kuwa mwanachama hai wa CCM, kugombea wadhifa wowote ule katika uongozi wa chama na/au serikali.
Kwa hivyo, jambo la msingi hapa sio kukimbilia Ikulu kwa sababu au mapenzi tu ya kutaka wadhifa wa Urais; bali ni kupata mgombea, sio tu atakayekiwezesha chama chetu kushinda katika uchaguzi ujao, bali la muhimu zaidi ni kupata mgombea mwenye uwezo, upeo na ubunifu wa sera na mikakati mizuri ambayo utekelezaji wake utaweza kuiletea nchi yetu maendeleo makubwa ya kiuchumi.
Hata hivyo, napenda kuahidi kuwa mgombea mwingine yoyote yule miongoni mwetu atakayebahatika kuteuliwa na chama chetu kugombea wadhifa wa Urais wa Zanzibar asiyekuwa mimi, basi nitampongeza kwa dhati kabisa na kushirikiana naye kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa anakiwezesha chama chetu kushinda katika uchaguzi ujao. Nasema hivi kwa sababu mchakato wa kumpata mgombea anayefaa kukiwakikisha chama chetu ni jambo la kidemokrasia kwa misingi ya ushindani na wala sio uadui wa kisiasa. Kadri chama kinapopata wagombea wengi wenye ujuzi na uzoefu tofauti ndivyo ambavyo chama kinavyopata upeo mpana wa kuteua mgombea anayefaa. Wakati wa kutafuta mgombea kwa njia ya mizengwe na usiri mkubwa umepitwa na wakati na hauna tena nafasi katika karne hii ya 21.
Katika kulizingatia hili kwa makini, Halmashauri Kuu ya Taifa, bila ya shaka yoyote ile, italazimika kumteua mgombea mwenye uwezo na ubunifu mkubwa katika jitihada za kuleta maendeleo makubwa nchini. Kutokana na elimu, uwezo na uzoefu mkubwa nilioupata katika utumishi wangu wa zaidi ya miaka 40 katika Serikali, katika medani ya kitaifa na kimataifa, nina kila sababu ya kuamini kuwa Zanzibar inahitaji kiongozi mwenye elimu, uwezo na uzoefu wa aina yangu ili kuiwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa sana kimaendeleo, kiuchumi, kijamii na hata kisiasa. Na hii hasa ndio sababu yangu ya pili iliyonisukuma kuamua kugombea wadhifa wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi.
Kwa lugha nyingine, wakati wa kulipa fadhila nilizopewa na wananchi wa Zanzibar, tokea kunisomesha mpaka kufikia mafanikio makubwa niliyoyapata katika maisha yangu umefika. Nasema hivi kwa sababu ikiwa mtoto niliezaliwa katika familia ya kimasikini, kama walivyokuwa wazee wangu wote, nimeweza kufanikiwa kuboresha maisha yangu kwa kiasi nilichonacho, basi nina kila sababu ya kuamini kuwa mtoto yoyote wa kimasikini anaweza kuboresha maisha yake ilimradi tu ikiwa atapatiwa fursa na nafasi za kujiendeleza na kuzitumia ipasavyo kama nilivyofanya mimi. Katika Zanzibar yenye kujali maslahi ya watu wake, mtu hapaswi kutoka katika familia ya kitajiri ili kufanikiwa. Kinachohitajika ni nia ya kujituma kwa vitendo, kutumia fursa zilizopo na kufanya kazi kwa bidii.
Kwa hivyo, katika kuthibitisha uwezo na uzoefu wangu huo, napenda kutumia nafasi hii, kuelezea kwa uwazi na ufasaha mkubwa nini nanakusudia kufanya katika kuiletea Zanzibar maendeleo ya kweli na endelevu ikiwa nitateuliwa na chama changu kugombea na hatimaye kuchaguliwa na wananchi kushika wadhifa wa Urais wa Zanzibar. Naamini kwa dhati kabisa kuwa kiongozi wa kweli ni yule mwenye uwezo wa kuitoa nchi yake katika dimbwi la umasikini uliokithiri na kuiingiza katika bwawa la utajiri na neema. Kwa mnasaba huu basi, nimeamua kujitosa moja kwa moja katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar ili niwatumikiye Wazanzibari kwa madhumuni ya kufanikisha mambo muhimu makubwa kama hivi ifuatavyo:
1) Haja ya kuondokana na uhasama, chuki na mfarakano baina ya Waunguja na Wapemba
Ndugu Wananchi,
Ndugu Wana-habari,
Katika kipindi karibu chote cha utawala wa Rais Karume, kwa bahati mbaya, chuki, uhasama na mfarakano miongoni mwa wananchi wetu katika visiwa vyetu vya Unguja na Pemba, bado ulizidi kuhatarisha usalama, amani na mshikamano wa kitaifa katika nchi yetu. Kama alivyowahi kusisitiza Mwenyekiti wa chama chetu, Mheshimiwa Jakaya Kikwete, “mpasuko wa kisiasa” baina ya wananchi wa visiwa vyetu viwili bado ulikuwa ni suala sugu ambalo lilipaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu haraka iwezekanavyo. Kwa bahati nzuri, Wazanzibari wengi tumefarijika kuona kuwa suala hili, hivi karibuni tu, limepatiwa ufumbuzi mzuri baada ya Rais Karume na Maalim Seif kufikia maridhiano yenye lengo la kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya Uchaguzi Mkuu mnamo mwezi wa Oktoba. Bila ya shaka yoyote ile, hii ni nafasi moja nzuri sana na ya kipekee ambayo, kama itatumiwa ipasavyo, basi uhasama, chuki na mfarakano baina ya wananchi wetu utakuwa ni jambo la historia.
Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza viongozi hao wawili kwa ujasiri wao huo na kuahidi kuwa ikiwa nitachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, basi nitaendeleza kwa vitendo yote yale yaliyokubaliwa ikiwa ni pamoja na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya kura ya maoni. Pia, naahidi kuwa tokea sasa ninaunga mkono wazo la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na nakusudia kujenga hoja na kutumia ushawishi wangu kuwashawishi wapiga kura kupiga kura ya ndio. Pamoja na ukweli kuwa kura ya maoni inawapa fursa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kulitolea uamuzi suala hili, lakini papo hapo kiongozi muadilifu ana jukumu la kusaidia katika kuonyesha njia kwa kuwaelimisha wananchi juu ya hasara na faida zitakazopatikana kwa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kwa lugha nyingine, faida za kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kubwa zaidi kwa maslahi ya nchi yetu na Wazanzibari kwa jumla kuliko hasara zitakazopatikana nayo.
Kwa hivyo, ikiwa Halmashauri Kuu ya Taifa itaniteua mimi kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, basi katika kampeni za uchaguzi zitakazofuatia uteuzi wangu, nitaahidi na kusisitiza juu ya umuhimu na ulazima wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, sio tu baina ya CCM na CUF, bali vile vile pamoja na kuvishirikisha vyama vingine vyote vitakavyoshiriki katika uchaguzi ujao ilimradi tu navyo viwe vimepata viti katika Baraza la Wawakilishi. Hii inatokana na ukweli kuwa bila ya usalama, amani na mshikamano wa kitaifa, hakuna maendeleo yoyote yale yatakayoweza kupatikana nchini. Hili ni jambo la kwanza kabisa nitakalolitekeleza kama Rais wa Zanzibar ikiwa CCM itashinda katika uchaguzi ujao na wananchi walio wengi watapiga kura za ndio kwa madhumuni ya kuundwa kwa SUK.
Hata hivyo, napenda kutanabahisha jambo moja muhimu katika kuzingatia mustakbal wa Zanzibar baada ya kuundwa kwa SUK. Suala kubwa ambalo wananchi tunapaswa kujiuliza ni hili: Jee, baada ya kuundwa SUK nini kitafuatia baada yake? Inafaa kujiuliza hivi kwa sababu haitoshi tu kuwaingiza katika serikali viongozi wa vyama vya upinzani kwa sababu au mapenzi tu ya kushiriki katika shughuli za uendeshaji serikali; hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa kuushirikisha upinzani katika serikali kunamaanisha kuupoteza upinzani wenyewe katika kutekeleza jukumu lake muhimu la kuimurika na kuikosoa serikali. Hii ni hatari kubwa sana kwa uhai wa demokrasia ya kweli yenye lengo la kuendeleza misingi madhubuti ya uwajibikaji na utawala bora.
Kwa hivyo, kuna haja ya kuhakikisha kuwa SUK itakayoundwa baada ya Uchaguzi Mkuu ujao itakuwa ni serikali ya muda mfupi tu kwa madhumuni ya kujenga misingi ya kuaminiana na kuweka mazingira mazuri ili chaguzi zifuatazo zifanyike katika mazingira ya uwazi kabisa, uhuru na haki; kwani, kwa bahati mbaya, hali hii hasa ndio chimbuko la mizozo ya kisiasa isiyokwisha nchini kwetu. Kama Rais wa Zanzibar, ninakusudia kuipitia katiba ya Zanzibar na Sheria zote za Uchaguzi nchini na kuzifanyia marekebisho yapasayo kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa chaguzi zote zinazofuata zinafanyika katika mazingira ya uwazi, uhuru na haki kabisa.
2. Haja ya kudumisha Muungano bila ya kudhoofisha mamlaka ya Zanzibar kwa mujibu wa katiba zetu zote mbili.
Ndugu Wananchi,
Ndugu Wana-habari
Kama tujuavyo, Muungano wa Tanzania bado unaendelea kukaribisha malumbano na manung’uniko yasiyokwisha baina ya pande zetu mbili hadi hii leo miaka 46 tokea kuanzishwa kwake. Kwa hivyo, ninaahidi kuzishughulikia kero za Muungano na kuzimaliza katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza kwa kupendekeza marekebisho ya katiba zetu zote mbili kama vile ipasavyo.
Napenda kutanabahisha hapa kuwa kuimarisha Muungano haina maana hata kidogo ya kuingiza kila kitu katika orodha ya mambo ya Muungano. Nasema hivi kwa sababu ni ukweli usiofichika kuwa Muungano utaimarika zaidi ikiwa hatua za makusudi zitachukuliwa kuyaondoa yale mambo yote yaliyomo katika orodha ya Muungano ambayo upande mmoja wa Muungano unaamini kuwa kuendelea kubakia kwake hakuleti faida wala maslahi mazuri kwake na hivyo kuna muelekeo wa kuuathiri vibaya upande wake. Hili halina mjadala ikiwa dhana ya kuanzishwa kwa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar imejengeka kikweli kweli katika misingi ya usawa, uhuru na upendo tokea hapo awali.
Isitoshe, inafaa kukumbusha hapa kuwa utaifa wa Tanzania unapata uhalali wake zaidi kutokana na mambo matatu ya msingi: uraia, mambo ya nje, na ulinzi na usalama. Nasisitiza hapa kuwa haya ni mambo ya kikatiba na ya msingi kabisa katika utaifa wa Tanzania. Bila ya ushirikiano wa kudumu baina ya Tanganyika na Zanzibar katika masuala haya matatu hapana shaka yoyote ile kuwa Muungano utavunjika. Na kwa vyovyote vile iwavyo, hakuna ushahidi wowote ule wa kuonesha kuwa manung’uniko makubwa ya Watanzania kwa jumla, na hasa zaidi ya Wazanzibari, yanatokana na mambo matatu haya.
Lakini, ni dhahiri kuwa mambo mengine yote yaliyomo katika orodha ya Muungano ni masuala ya kisera tu ambayo kuondolewa kwake hakutoathiri hata kidogo utaifa wa Tanzania au kusababisha kuvunjika kwa Muungano.
Kwa hivyo, ikiwa Halmashauri Kuu ya Taifa itanichagua kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi ujao, nitawaahidi wananchi kwa jumla na hususan wapiga kura, kuwa iwapo nitachaguliwa basi nitaanzisha mjadala wa kina na endelevu baina ya SMZ na SMT kwa kutumia nguvu ya hoja kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa mambo yale 11 tu yaliyomo katika Makubaliano ya Muungano ya 1964 yanaendelea kubakia katika orodha ya mambo ya Muungano. Mambo mengine yote yaliyoingizwa hapo baadaye hayana budi kuangaliwa upya kwa madhumuni, sio tu ya kuondosha kero, bali hasa zaidi kuimarisha Muungano. Hata kuhusu yale mambo 11 ya Muungano ya awali, si vibaya hata kidogo nayo kuangaliwa upya kwa madhumuni ya kuleta maelewano na maridhiano mema baina ya pande mbili husika.
Kwa mfano, ni kweli kabisa kuwa suala la Mambo ya Nje na Ulinzi ni suala la Muungano tokea hapo awali; lakini, suala la Ushirikiano ya Kimataifa (International Cooperation) si suala la Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano ya 1964. Hili liliingizwa hapo baadaye; pengine kwa sababu tu lina uhusiano wa karibu na Mambo ya Nje ya nchi. Lakini, ni ukweli usiofichika kuwa Ushirikiano wa Kimataifa unahusika zaidi na Maendeleo ya Kimataifa (International Development). Na ndio maana nchi nyingi zilizoendelea, kama vile Marekani, Uingereza, Sweden, Canada, na kadhalika, zimeanzisha Taasisi au Wizara maalum zinazohusiana na Ushirikiano wa Kimataifa. Iweje, kwa hivyo, Zanzibar isiwe na Wizara yake maalum inayohusika na suala hili muhimu la Ushirikiano wa Kimataifa kwa madhumuni ya kujiletea maendeleo?
Kwa kweli, moja katika manung’uniko makubwa ya SMZ, ni suala ambalo linajikita zaidi na misaada ya kiuchumi na kimaendeleo; na ndio maana mara nyingi hutokea mivutano isiyo ya lazima baina ya pande zetu mbili za Muungano. Ili kuepukana na hali hii, Zanzibar inahitaji kuwa na uhuru wa kutosha kushirikiana na nchi, Taasisi au Jumuiya mbali mbali kwa madhumuni ya kufaidika moja kwa moja na misaada ya kiuchumi na kimaendeleo bila ya kuingiliwa na SMT kwa yale mambo yasiyokuwa ya Muungano.
Kwa mfano, hakuna sababu yoyote ile ya msingi ya kuizuia Zanzibar kujiunga na OIS – taasisi ambayo malengo yake makubwa yamejikita katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi zaidi kuliko ile dhana inayoashiria kuwa Jumuiya hii ni taasisi yenye lengo na madhumuni ya kueneza dini ya Kiislamu miongoni mwa wanachama wake. Uwanachama wa nchi kama vile Uganda, Mozambique, Gabon na nyingi nyinginezo zenye wananchi wengi wanaofuata madhehebu ya dini ya Kikristo katika Jumuiya hii, ni ushahidi tosha kuwa lengo kubwa la Jumuiya hiyo ni kuendeleza Mashirikiano ya Kiuchumi na Kimaendeleo na wanachama wake zaidi kuliko kitu kingine. Kwa hivyo, hakuna sababu ya kuendelea kuizuia Zanzibar kujiunga na Jumuiya hii ikiwa Tanzania inashindwa kwa sababu yoyote ile kujiunga nayo. Kama kiongozi wa Zanzibar nitaanzisha mjadala wa kina na SMT kwa kutumia nguvu ya hoja ili kuhakikisha kuwa Tanzania au Zanzibar inajiunga na OIS katika kipindi changu cha miaka mitano ya kwanza.
Kwa mnasaba huu basi, hakuna sababu yoyote ile ya kuizuia Zanzibar kujiunga na taasisi za kimataifa kama vile, UNESCO, FAO, WHO, WFP, IAEA, WMO, IFAD – taasisi ambazo malengo yake makubwa yamo nje ya masuala ya Muungano ikiwa Zanzibar inakusudia kufanya hivyo siku za mbele. Na wala hakuna sababu ya msingi ya kukhofia kuwa Muungano utavunjika ati tu kwa sababu Zanzibar imejiunga na taasisi kama hizo. Kinyume chake, kuna kila sababu ya kuamini kuwa ushawishi wa Tanzania katika medani ya kimataifa utazidi kuongezeka na kupanuka zaidi kwa sababu Tanzania itakuwa na kura mbili katika Jumuiya hizo; kama vile ambavyo USSR hapo zamani ilivyokuwa ikifaidika kwa kuziruhusu Ukraine na Belorussia kujiunga na Umoja wa Mataifa. Na kwa kweli sote tunaelewa fika kuwa Urusi haikusambaratika kwa sababu ya uwanachama wa nchi hizo katika Jumuiya ya Umoja wa Mataifa (UNO).
Kama hili halitoshi, kilio kingine kikubwa cha Wazanzibari kinaambatana na kushindwa kwa ZFA kujiunga na FIFA. Mimi naamini kwa dhati kabisa kuwa inawezekana kabisa kwa Zanzibar kujiunga na Shirika hili la Soka Duniani ikiwa tu ZFA yenyewe itajisafisha kiutendaji na kujitegemea yenyewe kimapato. Kinyume chake, chama cha mpira kilichobobea migogoro isiyokwisha na kilichokosa nidhamu ya hali ya juu katika utendaji na uongozi wake, hakina nafasi wala uwezo wa kuushawishi uongozi wa FIFA kukubali ombi lake la kujiunga na Shirika hilo.
Isitoshe, pamoja na mambo mengine muhimu, Serikali ya Zanzibar kwa kushirikiana na SMT itapaswa kubuni mkakati wa kidiplomasia ya hali ya juu kwa madhumuni ya kuishawishi FIFA kulikubali ombi la ZFA. Jazba, lawama na ukosefu wa maelewano baina ya ZFA na TFA – yote haya yana muelekeo wa kudumaza jitihada za ZFA katika kujiunga na FIFA zaidi kuliko kuisaidia kufanikisha lengo hilo. Kama Rais wa Zanzibar, nitabuni mkakati kabambe wa kidiplomasia ya hali ya juu, ikiwa ni pamoja na kuzishawishi nchi zenye ushawishi mkubwa sana katika uongozi wa FIFA, kama vile Uingereza, Ufaransa, Uswisi kwa kushirikiana na SMT, ili kuhakikisha kuwa ZFA inajiunga na FIFA katika kipindi changu cha miaka mitano ya kwanza cha uongozi wangu.
3. Haja ya kuboresha uchumi wa Zanzibar
Wazanzibari wezangu,
Hali ya uchumi wa Zanzibar bado hairidhishi pamoja na maendeleo ya wastani yaliyokwisha kupatikana. Kwa hivyo, kuna haja kubwa ya kuboresha uchumi wa Zanzibar kwa njia ya kuleta mabadiliko kwenye sekta muhimu kabisa za kukuza uchumi wetu kama vile utalii, kilimo, uvuvi, biashara na viwanda. Nitahakikisha kuwa ukuwaji wa sekta hizi unaendana sambamba na mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu; huduma za afya na ujenzi wa miundo mbinu na njia mbadala za kupata nishati.
Inasikitisha kuona kuwa sera zote za kuboresha uchumi (Utalii, Viwanda, na Biashara) katika miaka kumi iliyopita hazijapata utekelezaji wa nguvu kwa kiwango ambacho tungelitegemea. Hakukuwa na ufanisi wa kutosha katika utekelezaji wake, mapato na ajira iliyotarajiwa.
Kwa mfano, SMZ ilitangaza kuanzisha maeneo huru ya uchumi ili wawekezaji waingize rasilmali zao katika ujenzi wa viwanda kwa madhumuni ya kuongeza ajira na kipato kwa wananchi wetu. Maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika maeneo huru kule Fumba, ukiacha lile eneo la viwanda vidogo vidogo hapo Amani, hayakufanywa lolote. Utalii pia umekuwa ukivujisha mapato na kutoa sehemu ndogo tu ya ajira kwa Wazanzibari. Matokeo yake, Zanzibar bado inaendelea kukumbwa na ukosefu mkubwa wa ajira kwa Wazanzibari hasa vijana wetu.
Katika jitihada za kukabiliana na hili, ninakusudia kutoa kipaumbele kwa Wazanzibari katika soko la ajira katika sekta za utalii, biashara, viwanda na kilimo. Asiyekuwa Mzanzibari ataajiriwa ikiwa tu muajiri ameshindwa kupata Mzanzibari mwenye sifa zifaazo. Mipango maalumu itabuniwa na kutekelezwa ili kuhakikisha kuwa Wazanzibari wanapatiwa utaalamu wa kutosha katika fani mbali mbali ili waweze kutimiza masharti ya soko la ajira nchini kwa misingi ya ushindani.
Ili kuongeza mapato makubwa zaidi katika uchumi wetu, nitahakikisha kuwa Serikali inabuni vianzio vipya vya mapato katika sekta zote za uchumi wa Zanzibar. Moja katika mbinu nitazozitumia ni kuifanyia marekebisho sera ya misamaha ya kodi kwa madhumuni ya kuepukana na matumizi yake mabaya. Nitaiangalia upya Sheria ya ununuzi na uuzaji wa vifaa na mali za serikali (Procurement Act) kwa madhumuni ya kupunguza gharama za ununuzi wa vifaa na kuongeza mapato ya serikali yatayopatikana katika uuzaji wa mali zake; nitaondoa kabisa utaratibu wa kuuziana mali za serikali kwa upendeleo na bei poa. La muhimu zaidi, nitaipitia bajeti ya serikali kifungu hadi kifungu kwa madhumuni ya kufuta matumizi yote yasiyokuwa ya lazima na hivyo kuiwezesha serikali kupata mapato ya ziada yatokanayo na ufanisi na nidhamu ya kifedha katika utekelezaji wa miradi na matumizi ya fedha.
Isitoshe, nitazipiga mnada gari zote za serikali za kifakhari za aina ya PRADO ili kuhakikisha kuwa mawaziri na viongozi wengine wa idara za serikali na mashirika yake wanatumia gari za gharama ndogo, kama vile RAV4 na kadhalika. Katika serikali nitakayoiongoza, itakuwa ni marufuku kuendelea na utaratibu unaowaruhusu mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa maidara na mashirika mbali mbali ya serikali kuendesha gari za serikali kama mali zao binafsi. Magari yote ya serikali yatakuwa chini ya usimamizi wa PWD; na yataendeshwa na madereva wa serikali na kuhudumiwa na mafundi wa serikali. Utekelezaji wa sera hii utaipunguzia serikali matumizi makubwa yasiyo ya lazima, kama vile malipo ya lita 25 za petroli au dizeli kwa siku yanayotolewa kuwahudumiya viongozi hao. Mapato yatayopatikana na mnada wa magari hayo pamoja na mapato ya ufanisi huo (efficiency gains) yatatumika katika kuboresha huduma za afya na elimu.
4. Haja ya kuleta mabadiliko katika mfumo wa huduma za jamii - zikiwemo elimu; huduma za afya na pia kutafuta mbinu za kupata vianzio mbadala vya nishati
Ndugu Wana-Habari,
Elimu ndio ufunguo wa maisha na maendeleo endelevu. Pia tukumbuke kuwa elimu ya msingi na sekondari ni haki ya kila mtoto nchini. Hili ni lengo la Serikali ya Mapinduzi tokea kufanyika kwa Mapinduzi ya 1964. Ni jambo la kufurahisha sana kuona kuwa kiwango cha uandikishaji watoto katika skuli za msingi kinazidi kukua mwaka hadi mwaka. Lakini, ongezeko hili haliendani na idadi ya skuli za msingi na hivyo kusababisha watoto wengi kulazimika kusoma katika darasa moja. Kwa mfano, hivi sasa kuna baadhi ya skuli zinachukua hadi watoto 100 katika darasa moja. Nyingine zinalazimika kusomesha kwa zamu. Utaratibu huu unaathiri sana maendeleo ya kitaaluma kwa watoto hawa. Serikali nitakayoingoza mimi itahakikisha kuwa idadi ya wanafunzi katika darasa inapunguzwa hadi kufikia watoto 35 kwa darasa na kuondoa kabisa utaratibu wa kusoma kwa zamu ili kuwapa watoto nafasi ya kutumia utoto wao ipasavyo. Nasema hivi kwa sababu mtoto aliyecheza mchana kutwa na kulazimikakuanza masomo katika nyakati za jioni hawezi kujifunza ipasavyo.
Isitoshe, kwa bahati mbaya, kiwango cha elimu nchini kimeshuka sana katika kipindi cha miaka ya karibuni. Katika kurekebisha hali hii, ninakusudia kuboresha kiwango cha elimu nchini kwa kuongeza bajeti yake marudufu i.e. kutoka asilimia 18 hadi asilimia 25 ya bajeti ya serikali. Tutajenga maskuli ya kisasa ya kutosha badala ya kuendelea kujenga majengo ya skuli ya aina ya mabanda ya kuku; kuziingizia skuli zetu zote kompyuta na maktaba za kisasa; na kuyapa kipaumbele masomo/mafunzo ya sayansi na teknolojia; kuajiri walimu wa kutosha na kuwapa taaluma ipasayo na mishahara mizuri inayolingana na hadhi ya taaluma yao ili kukidhi ongezeko kubwa la wanafunzi na kuinua kiwango cha elimu katika skuli za msingi na sekondari.
Katika Sekta ya Afya, pamoja na mambo mengine mbali mbali, ninakusudia kuboresha afya ya jamii. Nitatowa kipaumbele katika jitihada za kutokomeza kabisa maradhi ya Malaria na udhibiti wa maradhi ya kuambukiza hasa ya Ukimwi. Nitahakikisha kuwa kunakuwepo uwiano mzuri wa utoaji wa huduma ya afya mijini na mashamba (yaani huduma bora za afya zisiwe mijini tu, lakini mashamba pia zipatikane). Nitazifanyia ukarabati na kuzipatia zana za kileo hospitali zetu zote zinazomilikiwa na serikali na kuhakikisha kuwa hospitali na kliniki za watu binafsi ziko katika hali nzuri na ya kuridhisha. Hatua za makusudi zitachukuliwa kuajiri madaktari na wakunga wenye sifa zifaazo na kuwapatia mafunzo zaidi kila ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwaongezea mishahara kulingana na hadhi ya taaluma zao na haja ya kukabiliana na hali ngumu ya maisha. Mipango maalumu itabuniwa ili kuhakikisha kuwa kila Mzanzibari anapatiwa bima ya afya ili, yeye pamoja na familia yake, aweze kupatahuduma bora za afya yake hapa hapa nchini na kumudu gharama za matibabu ambazo kila kukicha zinazidi kuongozeka.
5. Haja ya Kupatikana kwa Nishati Mbadala na Kuboresha Huduma za Maji Safi
Ukosefu wa kupatikana kwa nishati ya uhakika ni suala linaloendelea kuwa sugu mwaka hadi mwaka na hivyo kuendelea kuathiri vibaya sekta zote za uchumi wa taifa. Ukosefu wa umeme umeleta athari kubwa za kiuchumi ikiwemo viwanda kufungwa, kupanda kwa gharama za uendeshaji katika mahoteli ya kitalii; na mamia ya wajasiriamali kupoteza ajira na kipato.
Isitoshe, huduma za maji nazo bado haziridhishi hata kidogo na hivyo kusababisha uhaba mkubwa wa maji katika maeneo mengi wanayoishi wananchi; hasa zaidi katika majumba ya ghorofa na katika viwanda na shughuli nyingine za uchumi. Matatizo haya sugu katika sekta hizi mbili muhimu za uchumi wa taifa, kwa pamoja, yanazorotosha uchumi wa Zanzibar kwa kiasi kikubwa na kuathiri vibaya sana ukuaji wake.
Kwa kutilia maanani matatizo haya sugu, ikiwa nitachaguliwa, ninaahidi kuleta mabadiliko makubwa katika mfumo mzima wa huduma za sekta mbili hizi na hasa zaidi katika kufikiria uwezekano wa kutafuta vianzio mbadala vipya na vya uhakika vya nishati.
6. Haja ya kuleta mabadiliko katika mfumo wa ardhi na ujenzi
Mabibi na Mabwana,
Kuanzia miaka ya 1990, SMZ ilifanya mapitio ya sheria za ardhi ili kuhakikisha kuwa inawatambuwa wamiliki ardhi; ilitoa hati miliki na kuzirekodi ardhi za wananchi wote nchini. Kwa bahati mbaya, miaka ishirini imepita, inasikitisha kuona kuwa bado sheria hizi hazikutekelezwa vya kutosha; na ndio maana kumekuwa na uendeshwaji wa shughuli za ardhi zisizoridhisha. Hali hii, mbali ya uuzwaji wa viwanja kinyume na sheria, dhulma kubwa inaendelea kufanywa dhidi ya baadhi ya wenye ardhi zenye thamani kubwa, hasa katika maeneo ya vijiji vilivyo kando na bahari ambako utalii umeshamiri. Baya zaidi, hali hii imesababisha ujenzi wa ovyo katika miji yetu ya Unguja na Pemba.
Kwa madhumuni ya kukabiliana na hili, hatua zifaazo zitachukuliwa kusafisha miji yetu na kudhibiti ujenzi wa ovyo ikiwa ni pamoja na kuanzishwa na kutekelezwa kwa sera mpya ya mipango miji; nitapiga marufuku utoaji holela wa viwanja na kuhakikisha kuwa shughuli hizo zinatekelezwa na mamlaka moja tu nchini kote chini ya Wizara inayohusika badala ya utaratibu unaotumika hivi sasa ambapo Sheha, Diwani, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa n.k. wanaonekanwa kuwa na mamlaka ya kutoa viwanja.
Isitoshe, kuna baadhi ya wananchi ambao, pengine kwa makusudi kabisa, wameshindwa kujenga katika viwanja walivyopatiwa na serikali kwa muda uliowekwa kwa mujibu wa sheria. Baadhi ya wananchi hao, wamekuwa wakijaribu kuviuza viwanja hivyo kwa mamilioni ya fedha. Hii si sawa hata kidogo; na ni hatari kwa maslahi mema ya nchi wetu. Kwa hivyo, serikali yangu itahakikisha kuwa wananchi hao wananyang’anywa viwanja hivyo na kupewa wananchi wasiokuwa navyo.
Ndugu Wana-habari,
Majumba mengi ya maendeleo yanayomilikiwa na serikali hivi sasa yapo katika hali mbaya; mengine kati ya yale yaliyotaifishwa yanaanguka na kuporomoka ovyo hasa wakati wa mvua za masika; na mengine yanauzwa na/au kukodishwa kwa upendeleo na bei poa. Ninakusudia kubuni sera maalumu yenye lengo la kuyafanyia ukarabati majengo yote yanayomilikiwa na serikali, na kuyauza kwa mnada yote yale yaliyo katika hali mbaya sana kwa wananchi watakaokuwa tayari kuyatengeneza kwa kuzingatia bei halisi katika soko la kuuziana majumba; badala ya kuuziana kwa njia za upendeleo na/au bei poa kama ifanyikavyo hivi sasa. Papo hapo, nitaangalia uwezekano wa kuanzisha Revolving Fund ya ujenzi wa nyumba kwa madhumuni ya kuwapatia wananchi mikopo itakayowawezesha kujenga nyumba za bei nafuu.
7. Vita dhidi ya ufisadi na rushwa
Ndugu Wananchi,
Ufisadi na rushwa ni adui mkubwa wa haki. Kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile, kuna haja kubwa ya kuendeleza vita dhidi ya ufisadi na rushwa kwa kasi na ari kubwa zaidi bila ya muhali. Kama Rais wa Zanzibar, nitahakikisha kuwa misingi ya maadili ya uongozi na uwajibikaji inafuatwa na kutekelezwa kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuondokana na tabia mbovu ya kulindana. Nitaanzisha Kitengo Maalum cha Kudhibiti Rushwa na Ufisadi katika nchi. Utekelezaji wa mambo haya utasaidia kwa kiasi kikubwa sana kuirejeshea Serikali na chama heshima yake; na papo hapo kuvutia hisia, imani na nyoyo za wapiga kura na wananchi kwa jumla. Na huu hasa ndio msingi muhimu katika utekelezaji mzima wa siasa safi na utawala bora wenye muelekeo wa kukipendezesha chama chetu, serikali na viongozi wake kwa mtazamo wa wananchi kwa jumla.
8. Kipaumbele katika kuhifadhi mazingira
Ndugu zanguni,
Inafaa kuzinduana hapa kuwa Zanzibar, isipofanya tahadhari, kuna hatari kubwa ya kupoteza rasilimali zake, ikiwemo ardhi yenye rutuba, misitu na miti ya asili, wanyama, na maeneo ya uvuvi. Kusema kweli, vitu vyote hivyo, tayari, viko mbioni kutoweka kwa haraka. Kama kiongozi wa nchi, nitachukuwa hatua thabiti katika jitihada zetu za pamoja ili kuhakikisha kuwa Serikali inashirikiana na wadau mbali mbali katika kuendeleza, kukuza na kuhamasisha ushirikishwaji wa jumuiya zisizo za kiserikali na watu binafsi katika kulinda na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
9. Watu wenye ulemavu
Pamoja na jitihada zinazoendelezwa na SMZ zenye lengo na madhumuni ya kuwasaidia watu wenye ulemavu kukabiliana na ulemavu wao; bado watu wenye ulemavu wanaendelea kukabiliwa na matatizo makubwa katika jamii ya Wazanzibari hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa hali ya mazingira ya maisha yao ya kila sibu bado hayaonekani kuwa ni ya kirafiki.
Kwa mfano, majengo yanayoendelea kujengwa nchini, bado hayazingatii mahitaji ya watu wenye ulemavu, kama vile kutiwa lifti, au njia maalumu zenye kuwawezesha kupanda na kushuka kwa urahisi. Mabarabara yanayojengwa nayo hayana njia maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu; taasisi nyingi za serikali na zisizo za kiserikali bado hazina watu wenye ujuzi wa kutumia alama maalum kwa watu wasioona, na wasiosikia. Kama rais wa Zanzibar, hatua za makusudi zitachukuliwa kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapatiwa mahitaji yao ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku. Lengo kubwa litakuwa ni kuwafanya watu wenye ulemavu wajihisi wako sawa na watu wengine wote bila ya kuonekana kubaguliwa kwa namna yoyote ile.
10. Utaratibu wa kuchagua viongozi katika Serikali ya Zanzibar
Ndugu wananchi na waandishi wa habari,
Utaratibu unaotumika hivi sasa wa kuwapata viongozi wa Zanzibar, hasa Rais wake, una mapungufu makubwa kwa kiasi ambacho kinawafanya Wazanzibari wengi kutoridhika nao. Napenda kusisitiza hapa kuwa, ikiwa chama chetu kinataka kuvutia hisia, imani na nyoyo za wapigwa kura kwa madhumuni ya kuungwa mkono kwa sauti kubwa, basi wananchi wa Zanzibar lazima waonekanwe kuridhika na utaratibu wa kuchagua viongozi wao. Kuna haja kubwa, kwa hivyo, ya kuondoa dhana ya muda mrefu iliyojengeka miongoni mwa Wazanzibari inayoashiria kuwa Tanzania Bara, na wala sio Zanzibar, ndio inayowachagulia Wazanzibari kiongozi wao; na hata kumg’oa aliye madarakani ikiwa hatakiwi.
Inafaa ifahamike hapa kuwa Urais wa Zanzibar si suala la Muungano; kwa hivyo, Wazanzibari wanapaswa kujiwekea utaratibu wao wenyewe utakaowaruhusu kuchagua viongozi katika ngazi zote za serikali bila ya kuingiliwa, kwa namna yoyote ile, na chama au taasisi za Tanzania Bara. Kwa mnasaba huo, kuna haja kubwa ya kuimarisha shughuli na majukumu ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu maamuzi makubwa yanayoihusu Zanzibar moja kwa moja kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa maamuzi au mapendekezo yanayotolewa na kamati hiyo kuhusu masuala yanayoigusa Zanzibar moja kwa moja yanaheshimiwa kwa vitendo. Na haya ndio hasa yaliyokuwa madhumuni ya msingi ya kuanzishwa kwa Kamati hiyo tokea hapo awali. Utekelezaji wake, kwa hivyo, utasaidia sana katika kujenga imani, hisia na nyoyo nzuri za wananchi kwa chama tawala na serikali yake. Ninakusudia kulishughulikia hili kwa kushirikiana na wenzetu wa Bara kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa maamuzi yote yanayoihusuZanzibar moja kwa moja yanafanywa na Wazanzibari wenyewe kupitia vyombo vinavyohusika. 11.
Hitimisho
Ndugu Wananchi,
Nimelazimika kuchukua muda mrefu kidogo kusoma hotuba hii kwa sababu ya umuhimu na unyeti wa uamuzi ambao Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM italazimika kuufanya katika zoezi hili zima la kumtafuta mgombea atakayefaa na hasa zaidi yule atakaye kihakikishia chama chetu ushindi katika uchaguzi ujao. Mimi si malaika, na si kweli hata kidogo kuwa nina majibu ya kila tatizo linaloikumba Zanzibar. Lakini, nina hakika kuwa nimejaribu angalau kuainisha kwa uwazi kabisa nini hasa matatizo ya Zanzibar kwa kadri niyaonavyo na jinsi ambavyo kiongozi ajaye atakavyo lazimika kuyashughulukia pindi akichaguliwa. Ozoefu wangu wa zaidi ya miaka 40 nilioupata katika utumishi wa Serikali ya Tanzania, SMZ na Umoja wa Mataifa umenisaidia sana katika kuyaona mambo kama nilivyoainisha hapa. Na huu hasa ndio uoni wangu kwa mnasaba wa mustakbali wa Zanzibar ya kesho ambao, ikiwa nitateuliwa kugombea urais wa Zanzibar, ninakusudia kuuingiza katika Ilani ya Uchaguzi wa 2010.
Hata hivyo, hapana shaka yoyote ile kuwa masuala mengi bado yanahitaji majibu. Kwa mfano, wapi nakusudia kupata fedha za kutosha kuiwezesha serikali kukabiliana na utekelezaji wa yote hayo niliyoyaeleza hapo awali? Ni vianzio vipya vipi vya mapato ninavyokusudia kuvianzisha kwa madhumuni ya kuongeza mapato ya serikali? Kitu gani kinachonifanya kuamini kuwa kero za Muungano zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu mnamo miaka mitano ijayo ya kipindi cha kwanza cha urais wangu? Hivi kweli ufisadi na rushwa vitashughulikiwa ipasavyo katika uongozi wangu na hivyo kuhakikisha kuwa ushindi unapatikana dhidi ya vita hivyo? na mengine mengi.
Kusema kweli, mpaka hivi sasa sina majibu kamili ya masuala hayo; lakini ninajua fika na kuamini kwa dhati kabisa kuwa yote hayo yanawezekana. Nasisitiza: yote hayo yanawezekana kwa sababu kinachohitajika hapa ni fikra na mawazo mapya. Zanzibar inao wasomi na wataalamu wa kila fani waliopo ndani na nje ya nchi ambao wanaweza kutayarisha mipango kabambe itakayoweza kutukwamua kutoka katika hali mbaya ya kisiasa na kiuchumi tuliyonayo hivi sasa. Kinachokosekana ni nia njema na ujasiri wa kuwatumia wasomi na wataalamu wetu hao ipasavyo na kikamilifu bila ya kujihisi kuwa kwa kufanya hivyo tutadhoofisha umaarufu wetu au mamlaka yetu. Kwa lugha nyingine, kwanza tunapaswa sisi wenyewe kubadilika; na pili, tunapaswa vile vile kuleta mabadiliko makubwa na ya kweli katika mfumo mzima wa utawala.
Isitoshe, Zanzibar inaweza kujifunza sana kutokana na mafanikio makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo yaliyopatikanwa katika nchi zinazoendelea kama vile South Korea, Singapore, China, Taiwan, Brazil, India, Indonesia, Mauritius na kadhalika. Kwa mfano, Hong Kong inaweza kabisa kuwa ndio kielelezo kizuri juu ya jinsi ambavyo mahusiano ya kiuchumi na kisiasa baina ya Zanzibar na Tanzania Bara yanavyoweza kuendelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa misingi ya kuelewana, kusaidiana na kushirikiana. Ili iweze kupiga hatua kubwa kimaendeleo, Zanzibar lazima ibuni na kutekeleza mikakati itakayoiwezesha kushindana na nchi hizo katika uuzaji wa bidhaa zake katika soko la dunia. Kwa manasaba huo, Zanzibar haina budi kufufua viwanda vyake vilivyokufa na kuanzisha viwanda vipya ili iweze kuzalisha bidhaa mbali mbali na kuziuza ndani ya Tanzania na nchi za nje. Kwa kufanya hivyo, Zanzibar itaongeza mapato yake ya nje na hivyo kuiwezesha kuongeza ajira kwa wananchi wake nakutunisha mapato yao.
Kwa upande wa Muungano, sina budi kusema kuwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jakaya Kikwete, hapana shaka yoyote ile kuwa hakuna kero isiyoweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu; ilimradi tu ikiwa tutajadiliana kwa kutumia nguvu ya hoja badala ya hoja ya nguvu; tena bila ya kusudio la kutaka kuuathiri vibaya au kuuhatarisha Muungano wetu. Hii ndio nia na msimamo, kama sikosei, wa Mwenyekiti wetu pale aliposema kwa yakini kuwa hakuna lisilojadilika.
Kwa bahati mbaya wengi wetu tumeshindwa kuitumia nia hii njema ya Mwenyekiti wetu na Rais wa Jamhuri ya Muungano ipasavyo na kikamilifu kwa kujenga hoja muwafaka katika jitihada zetu za pamoja za kufikia ufumbuzi wa kudumu. Badala ya kutatua kero za Muungano, tumeufanya Muungano kuwa ndio kero. Tumejikuta tuna ukosefu mkubwa wa nia njema na ujasiri wa kujenga hoja madhubuti ndani ya wakati unaofaa. Katika uongozi wangu, sitokua mpungufu wa nia njema na ujasiri wa kulishughulikia suala hili kwa kuitumia nia njema ya Mwenyeketi wetu ipasavyo na kikamilifu kwa madhumuni ya kuudumisha na kuimarisha Muungano wetu kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.
Kwa mfano, katika jitihada za kuleta mashirikiano ya karibu baina ya pande zetu mbili, Zanzibar inaweza kubuni mikakati ya makusudi yenye lengo la kuwekeza katika mashirika, mabenki au makampuni makubwa yaliyopo Tanzania Bara, kama vile CRDB, VODACOM, Kampuni za Migodi ya Dhahabu na Almasi, na kadhalika, kwa kununua hisa na hivyo kuiwezesha kuvuna mapato yatokanayo. Katika kufanya hivyo, Zanzibar inaweza kuitumia Ofisi yake iliyopo Dar es Salaam kikamilifu kwa madhumuni ya kufuatilia kwa ukaribu zaidi shughuli za mabenki, mashirika na makampuni yanayotia faida kibiashara na kupendekeza serikalini ipasavyo badala ya kujikita zaidi katika kuendeleza shughuli za kuomba misaada kutoka nchi wafadhili tu pekee. Kwa lugha nyingine, Zanzibar na Tanzania Bara zinahitaji kuendeleza mahusiano na mashirikiano mapya yenye kujikita zaidi katika kukuza na kuboresha chumi zao badala ya kuangaliya kila kitu kwa mtazamo wa kisiasa tu.
Namalizia kwa kusisitiza hivi: Naam, yote haya yanawezekana kabisa; kwa sababu ni vyema wote wale wenye mawazo na fikra za kizamani wakatanabahi kuwa Zanzibar ya 2010 haina budi kuongozwa na watu wenye fikra na mawazo mapya; na walio tayari kuleta mabadiliko makubwa na ya kweli katika mfumo mzima wa utawala. Kwa bahati mbaya, mawazo ya kizamani sio tu yamepitwa na wakati, lakini kubwa zaidi ni kuwa kuna hatari kwamba wimbi la mabadiliko ya kweli lina athari ya kuwaacha nyuma wote wale watakaopingana nalo.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
.
No comments:
Post a Comment