Monday, June 21, 2010

WALIOJITOKEZA KUCHUKUA FOMU ZA KUWANIA NAFASI YA URAISI KUPITIA CCM ZANZIBAR

Huku ikiwa kipindi cha uchaguzi mkuu kinakaribia viongozi kadhaa wamejitosa katika kuchukua fomu za kugombea nafasi ya Urais Zanzibar ambapo rais aliekuwepo madarakani kwa sasa Mh, Amani Karume anatarajiwa kumaliza muda wake wa uongozi.

Licha ya kua uchukuaji wa fomu hizo leo hii ulikua ni tofauti na watu walivyozoea, wagombea wengi hawakuingia kwa sherehe katika ofisi za CCM Kisiwandui lakini baadhi ya wapambe waliwasubiri wagombea wao na kuwasinidiza kwa magari wakati walipomaliza kukabidhiwa fomu hizo.

Wagomea waliochukua fomu leo hii alikua ni pamoja na Mohammed Aboud,Dr Ali Mohammed Shein,Balozi Ali Karume,Dr Mohammed Gharib Bilal,Shamsi Vuai Nahodha,Ali Juma Shamhuna,Hamad Bakari Mshindo.

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuchukua fomu Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud amesema Zanzibar hivi sasa iko kwenye mazingira mazuri zaidi kuliko nyakati nyengine zozote katika historia yake ya kuendeleza malengo ya maridhiano hivyo kuna kila sababu ya hali hiyo kuendelezwa.

Aboud aliahidi kuandaa mazingira mazuri ya kiuchumi yatakayovutia wawekezaji wa sekta binafsi na kuwekeza kwenye kutoa huduma ya afya ili Zanzibar iwe kituo cha kutoa huduma hiyo ndani ya afrika mashariki.


Kwa upande wake makamu wa Rais Dk ali Mohammed Shein ameahidi kuwa tahakikisha kuwa wanzanzibari wanaishi kwa amani na kuendeleza utamaduni wao wa kuvumiliana na kusaidiana na kuondosha tofauti zilizopo ambazo hazileti picha nzuri katika maisha ya mwanadamu.

Nimeamua kuichukua chanagmoto hii ya kugombea nafasi hii ya uongozi kwa nia safi, thabiti na kwa moyo mkunjufu nikiwa na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wazanzibari kama nilivyofanya huko nyuma nikiwa mtumishi wa SMZ na ambavyo nimekuwa nikiwatumikia hivi sasa nikiwa katika serikali ya Tanzania, huku nikiamini moyoni mwangu kuwa nimefanya uamuzi sahihi, kwa manufaa ya chama changu na ananchi wa zanzibar na Tanzania” amesema Dk Shein.

Dk Shein amesema ingawa mambo mengi yanasemwa lakini yeye hana roho ya ‘korosho’ kama inavyodaiwa wala si kiongozi wa kukata utepe na kuzinduwa miradi ya maendeleo tu bali ni mchapa kazi na viongozi wengi wanalifahamu hilo akiwemo rais Mkapa.

“Wapo wanaosema kwamba mimi kazi yangu kubwa ni kufunguwa miradi ya maendeleo kwa kukata utepe …si kweli hayo ni maneno tu ambayo lengo lake kubwa ni kunikatisha tamaa uwezo wangu mkubwa rais Kikwete hata rais Mstaafu Mkapa anajunifahamu katiak uwezo wangu”alisema.

Akizungumzia suala la kujiandikisha alisema kwamba hakujiandikisha kupiga kura Zanzibar kwa zaidi ya chaguzi mbili sasa lakini huko si kuvunja katiba wala sheria za uchaguzi na kumuondoshei sifa ya kuwa rais wa Zanzibar na kukataa suala la kuwa hauziki kwa wananchi.

“Wapo watu wanasema hivyo kuwa mimi sijajiandikisha kupiga kura Zanzibar…nimekutupa kwetu….si kweli mimi naongoza kwa kuwasaidia wananchi wa kwetu Mkanyageni…na wale ambao hawajuwi katiba wakasome..wasikurupuke tu” alisema huku akiwa na mkewe pembeni.

Akizungumza katika hilo balozi wa italia Ali Karume alisema pamoja na kuwa anaunga mkono maridhiano lakini suala la kura ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ya ndio au hapana hawezi kutaja msimamo wake kwa kuwa kura ya maoni itategemea na wakati husika lakini pia alisistiza kuendeleza kilimo ambacho ndicho kitu muhimu kwa kuinua pato ya taifa.

“Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo kama baadhi ya sekta zitapewa kipaumbele ikiwemo kilimo kama mnavyojua kilimo ni kitu muhimu sana cha kuweza kukuza uchumi na kuwapatia wananchi chakula lakini pia pato la taifa linainuka kwa kilimo pia” alisema balozi Karume.

Waziri kiongozi Mstaafu Dk Mohammed Gharib Bilal ambaye ni mtaalamu wa fizikia amehidi kusimamia suala zima la elimu na afya na amesema ingawa kisasi ni haki lakini amewatoa khofu wazanzibari endapo watampa ridhaa ya kuongoza, hatolipa umuhimu suala hilo, na kuahidi iwapo atapata nafasi ya uongozi ataendesha nchi kwa misingi ya utawala wa sheria huku akisisitiza suala la nidhamu katika utawala wake.

“Najua kisasi ni haki lakini mimi alipoingia rais Amani hajanifanyia kisasi chochote kwa hivyo wananchi wasiwe na khofu juu ya hilo sitalipiza kisasi” alisistiza Dk. Bilal

Aidha alisisitiza suala la kuimarisha Muungano uliopo na ksuema kwamba Tanzania ni mfano wan chi nyingi katika muungali wake hivyo ni vyema kuendelezwa na kero hizo zinazoitwa kero zinapaswa kurekebishwa.

“Muungano wetu ni imara pamoja na kuwepo kwa matatizo mbali mbali jambo la msingi ni kuyapatia ufumbuzi wake matatizo hayo kwa njia za kistaarabu kama inavyofanywa sasa” alisema Dk Bilal.

Dk Bilal alisema kwamba msimamo kuhusu kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa itategemea matokeo ya kura ya maoni itakayopigwa July 31 mwaka huu lakini kimsingi anakubaliana na hali ya amani iliyopo.

Kati ya wagombea wote Dk Bilal alikuja na umati mkubwa ukiwa na vionjo mbali mbali katika mkutano wake na waandishi wa habari na kabla ya hapo wazee wa mikoa mitano ya Unguja na Pemba walimkabidhi jumla ya shilingi milioni moja kama mchango wao uchukuaji fomu za kugombea urais wa Zanzibar.

fedha hizo zilikabidhiwa na Mzee Abdulrazak Simai Kwacha kwa niaba ya wazee wa mikoa mitano ya Unguja na Pemba.

Kamishna wa Elimu na Utamaduni, Hamad Bakari Mshindo alisema kwamba Zanzibar inahitaji mabadiliko makubwa katika sekta mbali mbali kwa ajili ya kuleta maendeleo ikiwemo elimu.

“Tunahitaji mabadiliko makubwa katika sekta za kiuchumi na elimu ili tupate maendeleo katika nchi yetu” alisema na kuahidi kwamba yupo taayri kushirikiana na wengine katika kuleta maendeleo.

Waziri kiongozi, Shamsi Vuai nahodha amesema msimamo wake katika kura ya maoni yeye binafsi anataka iwepo amani, lakini katika hilo ni vyema wazanzibari wakafanya maamuzi ya busara yenye kuendeleza umoja na mshikamano na akasema iwapo atapata ridhaa ya kuingia ikulu atateuwa watu kutoka pande zote za Zanzibar ili kuondosha malalamiko ya upande mmoja kutoshirikishwa katika serikali.

Waziri kiongozi huyo amesema cheo alichonacho kwa sasa ni sawa na bendera kufuata upepo au kondakta katika gari yenye dereva wake lakini anataka apewe ridhaa ya kuongoza ili aweze kuendesha gari mwenyewe.

Naibu waziri kiongozi Ali Juma Shamhuna alijisifia uadilifu wake katika chama chake na kusema kwamba yeye ni kiongozi muadilifu na safi na ameshafanya kazi na marais wote bila ya kukwaana kisiasa na yupo tayari kukubaliana na mbadiliko yatakayoheshimu misingi ya ilani ya CCM pamoja na utawala bora.

Shamuhuna alisema kwamba akichaguliwa kuwa rais wa Zanzibar atahakikisha analeta mabadiliko makubwa ya kisiasa na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

“Mimi naunga mkono maoni ya chama cha mapinduzi katika suala la serikali ya umoja wa kitaifa….mimi kura yangu ya ndio tu katika kura ya maoni July 31” alissisitiza Shamhuna.

No comments:

Post a Comment