Friday, June 18, 2010

KUINGIA NYUMBANI

Katika mila nyingi za Waislamu utaona kumewekwa mbele "aibu" kuliko "halali" na "haramu" na hili ni moja katika mambo yanayotuletea matatizo.

Inataka tuwafundishe watoto wetu wa kike na wa kiume umuhimu wa kutofanya ya haramu na kutilia mkazo hapo badala ya kuvutia upande wa kutotenda ya aibu khasa iwapo hilo linaloonekana kuwa ni la aibu linapingana na maamrisho ya dini yetu.

Kwa mfano, ukimfundisha mtoto mpaka akaelewa kuwa kuzini ni madhambi na akainukia na kukhofu kutenda hilo, ni afadhali (kwa mara zisizohisabika) kuliko kumwambia kuwa ni "aibu." Kuna wasichana wengi ambao hudhibiti bikra zao mpaka wakishaolewa na baada ya hapo huwa mengine tena na sababu yake kubwa ni kukhofia ya aibu kuliko kutenda ya haramu.

Wanawake wengi Duniani, khasa katika nchi wanamoishi Waislamu wengi, wanadhulumiwa na kuteswa kwa namna za kiajabu kabisa. Moja ni hiyo ya kushona tupu zao; na kuna akhasi ya hayo. Katika nchi fulani wasichana hunyakuliwa usiku na kupekekwa kwa "manyakanga" ili kufyekwa tupu zao ili wasiwe na hamu yoyote ya kuingiliwa maishani mwao. Sasa kama huo si uqatili na uovu wa hali ya mwisho kabisa, basi ni kitu gani hicho?

Na yote haya yanatokana na huko kuona aibu iliyopelekea watoto wa kike kuzikwa wangali wahai, na siku ya Qiyama waliotenda hayo watakuja kuhojiwa kama tulivyoelezwa katika Qur-an Tukufu. Tuwafundishe zaidi watoto wetu wa kiume na wa kike kukhusu ya halali na haramu kuliko ya aibu kimila.

Kusherehekea hadharani kuwa mwanao wa kike amebikiriwa na mumewe ni kutangaza yasiyofaa kuelezwa licha kutangazwa ulimwenguni ili kila mmoja ayajue.

Kila la kheri,
Ibrahim

No comments:

Post a Comment