Thursday, June 17, 2010

KOMBE LA DUNIA "LIMEKULA KWA WALALA HOI"

Taarifa toka BBC kufuatia uchunguzi ikiwa raia wa kawaida wanafaidika na mashindano ya kombe la dunia inaonesha kuwa waliofaidi hadi sasa ni shirikisho la mpira duniani (FIFA),pamoja na mabwanyenye.

1.Raia mmoja, Angela Ncube, mchuuzi wa barabarani amesema kuwa ukiritimba mkali wa biashara umedidimiza ndoto za wengi akiwemo wamiliki wa nyumba na wafanyabiashara. Ncube amesema kuwa alilazimishwa kuhama kutoka karibu na uwanja wa mpira huko Johannesburg alipojaribu kuuza pipi na bidhaa ndogo ndogo kwa mamilioni wanaoingia uwanjani.

2.Taarifa ya FIFA inasema haijawakwaza wachuuzi wenye biashara ndogo ila imewapa fursa wenye biashara za wastani waweze kunufaika ili kujenga nafasi za ajira, taarifa ambayo ni vigumu kukubalika ikiwa utachunguza hali halisi ya maisha ya wananchi wa kawaida.

3.Polisi na walinzi wamezingira viwanja vinavyotumiwa kwa mashindano haya, wakichunguza mihadarati inayoweza kusababisha ghasia. Wananyang'anywa chakula au kinywaji kisichotoka kwa makampuni yaliyosajiliwa na FIFA au mamlaka nyingine.

4.Umasikini wa kupindukia pamoja na ukosefu wa ajira unaokadiriwa kufikia asilimia 25 umesababisha mamia ya watu kumiminika mitaani wakijaribu kuuza bidhaa ili kukidhi maisha. Wengi wao wamekuwa wakiuza bendera, jezi na kofia zinazohusiana na Kombe la Dunia kwa raia wenzao lakini wamezuiliwa kuwasogelea wageni.

5.Ndani ya viwanja, bidhaa kama pombe ya wadhamini maalum Budweiser inaruhusiwa lakini pombe maarufu nchini humo inayotengenezwa na kiwanda cha pili kwa ukubwa duniani SAB Miller hairuhusiwi. Kampuni hiyo imefanikiwa kuuza bidhaa zake katika maeneo ya wazi ambako mkono wa FIFA haufiki.

6.Watalii wachache. Upungufu wa fedha. Afrika ya Kusini ilitarajia mamilioni ya watalii lakini ukweli wa mambo ni kwamba imepokea watu 370,000 au pungufu. Wengi wamehofia maisha yao, gharama kubwa na uhalifu. Wamiliki wa hoteli, migahawa na biashara zinazotegemea utalii imewabidi wapunguze matumaini ya kipato kikubwa walichotarajia.

7.Waimbaji wa nchi hiyo ambao ni maarufu kote duniani, walitarajia vibarua lakini wasanii kama Black Eyed Peas na Shakira ndiyo waliobahatika kwenye sherehe rasmi.

Kundi la wamiliki wa nyumba na mawakala wa biashara ya nyumba waliodhani watapandisha bei za kupanga nyumba wakati wa Kombe la Dunia wamejikuta katika majonzi makubwa na nyota ya jaha imekuwa janga.

No comments:

Post a Comment