Wednesday, June 30, 2010

BILAL ATUMIA MBINU ZA JK

Kinyang'anyiro cha kuwania uteuzi wa urais wa Zanzibar ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeingia katika hatua nyingine, baada ya kambi inayomuunga mkono Waziri Kiongozi wa zamani, Dk. Mohammed Gharib Bilal, kuanza kutumia mbinu za kusaka ushindi ambazo zilitumiwa na kundi la wanamtandao waliokuwa wakimuunga mkono Rais Jakaya Kikwete wakati wa harakati za kusaka urais wa Muungano mwaka 2005

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano umebaini kuwa moja ya mbinu hizo za kambi ya Bilal ni pamoja na ile ya kutishia kujitoa katika chama hicho iwapo jina lake litaondolewa katika kinyang’anyiro hicho kwa njia ya mizengwe, hasa katika vikao vya chama vitakavyofanyika Dodoma.

Habari kutoka kwa watu walio karibu na kambi hiyo ya Dk. Bilal, zinaeleza kwamba iwapo hilo litatokea, Dk. Bilal ataombwa kujiunga na Chama cha Jahazi Asilia na kugombea urais.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba mbinu hii ya kutishia kujitoa CCM ndiyo iliyotumiwa pia na vinara wa kundi la mtandao ambao miezi kadhaa kabla ya mchakato wa kusaka mgombea wa urais wa chama hicho walipenyeza taarifa ndani ya vyumba vya habari na katika taasisi nyeti za dola kuwa mgombea wao (Kikwete) alikuwa tayari kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo () iwapo angeenguliwa katika mchuano huo kwa njia ya mizengwe.

Habari ambazo zilipatikana wakati huo zinaeleza kuwa tishio hilo la kuwapo kwa taarifa za Kikwete kuwa tayari kujitoa CCM ndizo ambazo kwa kiwango kikubwa ziliwatisha viongozi wa juu wa chama hicho hata wakalazimika kuacha mchakato wa kumsaka mgombea urais ufanyike kwa uwazi, na baadaye Mwenyekiti wa chama hicho wakati huo, Benjamin Mkapa, akatoa hotuba za kulibeba kundi la mtandao.

Hoja nyingine ambayo inajengwa na kambi ya Dk. Bilal ambayo inafananishwa na ile iliyotumika kumbeba Kikwete mwaka 2005 ni ukweli kwamba yeye ndiye aliyestahili hasa kuwa mgombea urais mwaka 2000 baada ya kuibuka mshindi wa kura kwenye mchakato wa awali ulioanzia ndani ya kikao cha Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar.

Katika mazingira ambayo hadi sasa Tanzania Daima Jumatano haijaweza kuyanyumbulisha, kumekuwa na taarifa zinazoonyesha kwamba miongoni mwa watu wanaomuunga mkono Dk. Bilal katika mchuano wa sasa ni makamanda wa juu waliokuwa wakiongoza mtandao wa Kikwete mwaka 2005.

Kikubwa ambacho kinaonekana kuwashangaza wengi ni kwamba hatua hiyo inakuja wakati kukiwa na ushahidi wa wazi kwamba mwaka 2000 makamanda hao wa mtandao ndio waliokuwa wapinzani wakubwa wa Dk. Bilal, na ndio maswahiba waliomsaidia chaguo lao, Amani Abeid Karume, kushinda.

Tofauti pekee ambayo inaonekana kuwa inaweza ikawa doa linalomtofautisha Bilal na Kikwete katika azima yao ya kusaka urais ni hatua ya Bilal kuamua kuchukua fomu mwaka 2005, wakati akijua kuwa Karume alikuwa ana fursa nyingine ya kikatiba kumalizia ngwe yake ya pili.

Wakati uamuzi huo wa Bilal kupambana na Rais Karume miaka mitano iliyopita kwa upande mmoja ulikuwa ukionekana kuwa ni wa mwanasiasa jasiri anayesimamia kile anachokiamini pasipo kumhofia yeyote, kwa upande wa pili umekuwa ukitajwa na wapinzani wake kuwa ni kielelezo cha mwanasiasa mwenye uchu wa hatari wa kusaka uongozi kwa gharama zozote.

Hata hivyo, habari za ndani za CCM zinasema hata Kikwete (wakati huo akisubiri kugombea) alitoa pendekezo ndani ya kamati kuu mwaka 2000 akitaka chama kiruhusu rais aliye madarakani (Mkapa) ashindanishwe na mwanachama mwingine, kwa maana ya kuimarisha demokrasia; jambo ambalo lilipingwa na uongozi wa chama.

Wapinzani wa Dk. Bilal wa kundi moja la wahafidhina wa CCM wamekuwa wakikifananisha kitendo hicho cha Dk. Bilal kuwa sawasawa na kile alichokionyesha Maalim Seif Sharif Hamad wakati alipokuwa mwanachama wa chama hicho, miaka ya 1980 alipojitokeza na kumpinga waziwazi aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo, marehemu, Abdul Wakil Nombe.

Kwa mujibu wa wahafidhina hao, kitendo hicho cha Bilal kuonyesha dhamira ya kuutaka urais kwa staili ile ile ya Maalim Seif kinamweka katika mazingira ya kumfanya akose sifa ya uvumilivu na ustahimilivu ambayo alikuwa nayo Kikwete wakati alipokubali kusubiri hadi Mkapa amalize ngwe yake ya miaka 10 mwaka 2005.

Hoja hizo za wahafidhina zinapingana vikali na zile za wapenzi wa Dk. Bilal ambao wanakiona kitendo chake cha kukubali kuondoa kwake jina mwaka 2005 kwa shinikizo na ushauri wa viongozi wengine wa juu wa CCM kuwa ni cha kistaarabu na kuungwa mkono.

“Hii ni mara ya tatu Dk. Bilal anawania nafasi hiyo, mara ya kwanza alienguliwa kwa mizengwe, mara ya pili aliondoa jina lake tena kwa maandishi, safari hii hakuna sababu ya kumzuia na ikitokea hivyo, ataondoka CCM na kujiunga na upinzani na anao watu wengi nyuma yake,” kilisema chanzo kimoja cha habari kilicho karibu na mwanasiasa huyo.

Katika hatua nyingine, mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amemtaka Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Shamsi Vuai Nahodha, kumtanguliza Mungu mbele katika harakati zake za kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar.

Mama Nyerere ameyasema hayo nyumbani kwake Msasani, jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo kati yake na waziri huyo kiongozi, ambapo alitumia nafasi hiyo kumuasa mambo mbalimbali ambayo yatamsaidia kufanikikisha harakati zake hizo.

Alisema jambo kuu ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika kila jambo, hali itakayomfanya aweze kushinda vikwazo vitakavyomkabili katika kufanikisha lengo lake la kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais wa Zanzibar.

“Mimi na Mwalimu tulikuwa tukitamtanguliza sana Mungu katika kila jambo na ndiyo maana tumefanikiwa kuifanya Tanzania iwe na amani, nawe mwanangu mtangulize Mungu, hakika utafanikiwa,” alisisitiza mjane huyo wa Baba wa Taifa.

Naye Waziri Nahodha amesema ataweka mbele masilahi ya Mzanzibari na Mtanzania kwa ujumla, iwapo atapata nafasi ya kuwatumikia Wazanzibari katika nafasi ya urais.
.

No comments:

Post a Comment