Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kuondoa woga baada ya nchi wanachama kusaini mkataba wa kuanzishwa kwa soko la pamoja la Jumuiya la Afrika Mashariki (EAC) linalotarajiwa kuanza utekelezaji wake Julai, mwaka huu.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mohammed Aboud Mohammed, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa Baraza la Biashara Zanzibar (ZBC), uliofunguliwa na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, mjini hapa jana.
Alisema soko la pamoja la Jumuiya hiyo lina faida kubwa kwa nchi wanachama katika kukuza uwekezaji, kuongeza masoko na ajira kwa wananchi toka nchi wanachama wake.
Waziri Aboud alisema wafanyabiashara na wananchi wa Zanzibar, wanapaswa kujitayarisha ili waweze kulitumia vizuri soko la pamoja hasa katika masuala ya uwekezaji na masoko ya ndani ya nchi wanachama.
Hata hivyo, alisema soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki litatawaliwa na ushindani mkubwa na kuwataka wananchi kujenga mazingira mazuri yatakayowasaidia kunufaika na ajira ndani ya soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema serikali ya Muungano na ya Zanzibar, tayari zimeweka mazingira ya kulinda ajira za ndani ya Zanzibar kwa vile wageni watanufaika na ajira ambazo wataalamu wake hawapatikani ndani ya nchi.
Waziri Aboud alisema Zanzibar ni nchi ya visiwa lazima kuwepo na utaratibu wa kulinda ajira za ndani ndiyo maana serikali imeamua kuweka ajira maalum kwa wageni.
“Serikali ya Muungano imezingatia maslahi muhimu ya nchi kabla ya kuingia katika soko la pamoja na hakuna sababu kwa wananchi kuwa na woga kuhusu soko la pamoja,” alisisitiza.
Alisema Zanzibar inatarajia kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo kupitia jumuiya hiyo ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege Karume kisiwani Pemba, bandari huru, umeme wa pepo na mradi wa kilimo Zanzibar.
Alisema mradi wa bandari huru, unatarajiwa kujengwa katika eneo la Mpigaduri na utagharimu dola za Marekani milioni 400 na mradi wa umeme wa upepo dola milioni 70 wakati ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Karume Pemba utagharimu dola milioni 78 na mradi wa kilimo dola milioni 100.
Alifafanua kuwa miradi hiyo itasaidia utekelezaji wa Mpango wa serikali wa Kukuza Uchumi na Kupunguza umaskini kwa wananchi wa Zanzibar (Mkuza).
.
No comments:
Post a Comment