Wednesday, May 19, 2010

MAKONTENA 50 YAINGIZWA ZANZIBAR BILA YA KODI

Makontena 50 ya saruji yenye thamani ya Dola za Kimarekani 84,000 sawa na Sh. milioni 114.8 yameingizwa Zanzibar yakitokea nchini Pakistan bila kulipiwa kodi kupitia Bandari ya Malindi Mjini Zanzibar.

Uchunguzi uliofanywa umegundua kuwa makontena hayo yaliingizwa visiwani humu kufuatia msamaha wa kodi uliotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha na Uchumi), Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini.

Kibali cha msamaha wa kodi kimetolewa Mei 12, mwaka huu chenye kumbukumbu namba WF/EXEMPT/TA/2010/VOL.II/NO.2 akitakiwa Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Kanda ya Zanzibar kutotoza kodi ya ushuru wa forodha mzigo huo.

Shehena hiyo ya Saruji ililetwa Zanzibar na meli ya mizigo ya MV Concord ikitokea Karachi nchini Pakistan na kuwasili Zanzibar wiki iliyopita. Nyaraka za usafirishaji mzigo huo yenye kumbukumbu namba Karzan-091 ya Aprili 24, mwaka huu, inaonyesha makontena hayo yaliletwa na kampuni ya uwakala wa mizigo ya Abdul Enterprises C/F Company ya Darajani mjini Zanzibar.

Kampuni hiyo imepewa kazi ya kuingiza saruji hiyo na Halmashauri ya Wilaya ya Kati Unguja kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ.

Kwa mujibu wa msamaha wa kibali cha msamaha wa kodi cha waziri saruji hiyo haitakiwi kutozwa ushuru wa forodha pamoja na Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT)

Hata hivyo, saruji hiyo imeanza kuingia katika soko la ndani la Zanzibar na kuuzwa katika maduka ya rejareja. Mzigo huo wa saruji uliingizwa nchini kwa kutumia nyaraka za usafirishaji zenye namba 20100425CON703ZNZ ya Aprili 25, mwaka huu.

Naibu Kamishina wa TRA Kanda ya Zanzibar, Hassan Mcha, alithibitisha jana makontena hayo kutolewa bila ya kulipiwa kodi kutokana na msamaha wa kodi uotolewa na Waziri wa Fedha Zanzibar.

Akizungumza na Nipashe Dk. Makame alithibitisha kutoa msamaha huo lakini alisema hana taarifa kama saruji hiyo imeanza kuingizwa katika soko la ndani la Zanzibar.
.

No comments:

Post a Comment