Sunday, May 2, 2010

UGIRIKI YAPATA MKOPO WA EURO BILIONI 120

Ugiriki imefikia makubaliano na Umoja wa Ulaya pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, kupewa Euro bilioni 120 ili kuikoa nchi hiyo isifilisike.

Nchi hiyo nayo imeahidi kupunguza matumaizi ya serekali yake kwa kiwango cha Euro bilioni 30 mnamo miaka mitatu ijayo.

Katika mkutano wa baraza la mawaziri la nchi hiyo uliotangazwa kwa njia ya televisheni, waziri mkuu wa nchi hiyo, Georges Papandreou, alisema wananchi itawabidi wajitolee zaidi ili kuepukana na janga.

Serekali yake inapanga kutangaza hatua kali za kupunguza matumizi hadi mwaka 2012, mishahara itapunguzwa na malipo ya pensheni yatakwenda chini. Licha ya hayo, kodi ya mauzo itapandishwa na matumizi ya wizara ya ulinzi yatapunguzwa.

Hatua hizo zimekabiliwa na maandamano ya raia wa Ugiriki. Katika mwaka wa mwanzo nchi za sarafu ya Euro zitatoa hadi Euro bilioni 30, kama mkopo kwa Ugiriki, nalo Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, litatoa Euro bilioni 15.

Katika mikutano ya hadhara ya jana ya kuadhimisha sherehe za sikukuu ya wafanya kazi, Mei Mosi, maelfu ya watu waliandamana mabarabarani huko Ugiriki kupinga hatua hizo za kukaza mkwiji, na kupelekea kutokea mapambano na polisi wa kuzuwia fujo.

Hatua hizo za kukaza mkwiji ni shuruti ya kufikiwa makubaliano hayo na zimesisitizwa na Ujeruman pamoja na nchi nyingine zinazotumia sarafu ya Euro.

Hii leo, mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro wanakutana mjini Brussels katika mazungumzo ambayo mwenyekiti wake atakuwa waziri mkuu wa Luxembourg, Jean-Claude Junker, kiongozi wa kundi la nchi zenye kutumia Euro.

Mazungumzo hayo yatatuwama juu ya hali ya mambo ilivyo huko Ugiriki na uthabiti wa sarafu ya Euro.

.

No comments:

Post a Comment