Sunday, May 23, 2010

SMZ YAPATA "KIGUGUMIZI" KURIDHIA SHERIA YA RUSHWA 2007

Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), kimesema Zanzibar imekumbwa na ‘kigugumizi’ na kushindwa kuridhia sheria ya kupambana na rushwa tangu ilipopitishwa na Bunge mwaka 2007

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa kituo hicho Profesa Chris Maina Peter, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya haki za binadamu ya Zanzibar ya mwaka 2009 uliofanyika jana mjini Zanzibar.

Alisema tangu sheria hiyo kupitishwa imeshindwa kufanyakazi Zanzibar kwa vile inahitaji kuridhiwa na Baraza la Wawakilishi kwa vile masuala ya rushwa hayamo katika orodha ya mambo ya Muungano.

Hata hivyo alisema sheria hiyo ina umuhimu mkubwa katika kujenga misingi ya haki za Binadamu na utawala bora hasa katika vyombo vya kusimamia sheria.

Aidha alisema maridhiano yaliyofikiwa kati ya Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF yana nafasi kubwa ya kuondoa malalamiko ya watu kunyimwa fursa ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Alisema utafiti walioufanya wapo watu Unguja na Pemba hawajaandikishwa kutokana na urasimu wa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi.

Hata hivyo alisema baada ya kufuatilia tatizo hilo kwa watendaji wa Idara ya usajili wa vitambulisho vya Mzanzibar Mkazi walisema vitambulisho vingi wanavyo baada ya wahusika kushindwa kujitokeza kwenda kuvichukua.

No comments:

Post a Comment