Sunday, May 23, 2010

MAHUBIRI YALINICHOCHEA NIRIPUE UBALOZI

Mwanafunzi Nassib Mpamka (15), anayetuhumiwa kufanya jaribio la kulipua Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, amekiri na kudai kuwa alihamasishwa na mahubiri ya shehe wa msikiti wa Mtambani na kwamba wazo la kulipua ubalozi huo alikuwa nalo tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Mpamka, ambaye anashikiliwa na Polisi, katika madai yake alisema alitaka kulipua ubalozi huo baada ya kusikia mahubiri hayo aliyodai kuwa yalihusu majeshi ya Marekani kuua Waislamu duniani.

Hata hivyo, Katibu wa msikiti huo, Shehe Abdallah Mohamed, alipozungumza na gazeti hili juzi mara baada ya sala ya Ijumaa, alisema shule ya Mtambani ambayo awali Mpamka alidaiwa kusoma, haihusiki na kutoa mafunzo ya ugaidi na wala hakuna mwanafunzi wao aliyekamatwa akihusishwa na kashfa hiyo.

Shehe Mohamed alisema huenda kuna njama zinazoandaliwa na wahusika ambao hakuwataja majina, ambazo alidai lengo ni kuidhoofisha taasisi yao.

“Inawezekana uzushi wa jambo hili ukawa si wa bure, maana hata Marekani ilipotaka kuipiga Iraq ilianza kutoa visingizio vingi vikiwamo vya kuwapo silaha kali, kitu ambacho mpaka leo bado hakijathibitika,” alisema kiongozi huyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi, Peter Kivuyo akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu tukio hilo, alisema mtuhumiwa huyo alibainisha kuwa shehe huyo ambaye mpaka sasa hajatajwa jina, alikuwa akihubiri mara kwa mara kuhusu vitendo vya majeshi ya Marekani kuwaua Waislamu katika nchi mbalimbali duniani.

“Mwanafunzi huyo alisema kuwa mahubiri na mafundisho ya shehe huyo yalimgusa na mawazo yalijengeka akilini mwake, akapata wazo hilo tangu mwishoni mwa 2009… sasa sijui nisemeje, maana mafundisho mengine kwa kweli ni mabaya,” alisema Kivuyo.

Kivuyo alisema hivi sasa wanahojiwa watuhumiwa wawili, yaani Mpamka na mwenzake Amani Thomas (15), ambaye pia ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Biafra.

Thomas anadaiwa ndiye alikwenda na Mpamka kufanya jaribio hilo, lakini yeye alibaki katika eneo ambalo linatumika kuuzia maua lililo karibu na ubalozi huo, wakati Mpamka akifanya jaribio hilo.

Awali Kamishna Kivuyo alisema Mei 16 saa 2:30 usiku, Mpamka alifika katika viunga vya ubalozi huo katika eneo ambalo linaegeshwa magari ya kubebea maji na kurusha chupa iliyokuwa imejazwa mafuta ya taa na kuwekwa utambi kwa lengo la kulipua magari hayo. Kutokana na juhudi za walinzi wa ubalozi huo waliokuwa kazini, walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na kumfikisha Polisi kwa mahojiano zaidi.

Kamishna Kivuyo aliongeza kuwa uchunguzi utakapokamilika, hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa.

Awali gazeti hili liliripoti kukamatwa kwa Mpamka baada ya kudaiwa kuingia katika ubalozi huo kwa kupitia geti namba tatu na kujaribu kufungua koki ya tanki ya mafuta katika ubalozi huo.

Mara baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, siku iliyofuata maofisa wa usalama wa Taifa na polisi walifika katika shule ya sekondari ya Biafra na kuchukua wanafunzi wanane kwa ajili ya mahojiano kuhusu jaribio la kutaka kulipua ubalozi huo.

Uchunguzi zaidi uliofanywa na gazeti hili na habari za uhakika kutoka ndani ya Polisi, ulibaini kuwa Mpamka ni mtoto yatima na alikuwa akiishi Kinondoni Moscow aribu na hoteli ya Livingstone, kwa shangazi yake aliyejulikana kwa jina la Chiku Simba.

Simba alipohojiwa na gazeti hili kama ana uhusiano na mtoto huyo, alijibu kuwa hamfahamu na akadai kuwa suala hilo halitambui na kwamba habari hizo amekuwa anazisikia tu kwenye vyombo vya habari.

Hata hivyo, majirani wa kijana huyo walisisitiza kwamba kijana huyo alikuwa akiishi hapo na kwamba Simba ni shangazi yake. Baada ya kupata msisitizo huo, gazeti hili lilirudi kwa Simba kupata uhakika ambapo shangazi huyo alikiri kuishi na Mpamka na kukataa kuelezea zaidi.

Majirani wa Mpamka pamoja na marafiki zake wa mtaani, walieleza kushtushwa na habari za kijana huyo kwa maelezo kuwa mtoto huyo ni mkimya, hana mazoea na watoto wenzake na wala hana tabia ya kukaa vijiweni.

Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amekanusha kusema kwamba anatilia shaka ulinzi wa ubalozi huo, kutokana na tukio hilo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kova alisema yeye ndiye mwenye jukumu na wajibu wa kuhakikisha ulinzi wa balozi zote zilizoko katika kanda yake unakuwa wa uhakika na hivyo isingewezekana tena ajidharau.

“Haiji kwa mimi ambaye ndiye mlinzi wa balozi hizo ukiwamo wa Marekani, leo nigeuke na kusema ulinzi huo ni dhaifu na hivyo kuwa na shaka nao, pengine ilitafsiriwa vibaya niliposema ulinzi katika balozi umeimarishwa,” alisema Kamanda Kova.

.

No comments:

Post a Comment