Tuesday, May 11, 2010

OCAMPO AKUTANA NA WATU WALIOATHIRIKA NA GHASIA ZA UCHAGUZI NCHINI KENYA


Luis Moreno Ocampo amesema jana kuwa amefanya ziara katika eneo linalokumbwa mara kwa mara na uhalifu nchini Kenya la mtaa wa mabanda la Mathare ili kufahamu maoni ya baadhi ya watu walioathirika na ghasia za baada ya uchaguzi, ambazo zimesababisha watu zaidi ya 1,000 kuuwawa. Mtaa wa mabanda wa Mathare unafahamika kwa kiwango chake cha juu cha uhalifu na kusambaa kwa utengenezaji na matumizi ya pombe za kienyeji.

Mwendesha mashtaka amesema anaamini uhalifu dhidi ya ubinadamu umefanyika wakati wa ghasia hizo. Majaji wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita waliidhinisha mwezi uliopita kuwa Moreno Ocampo anaweza kuanza kufanya uchunguzi kuhusu suala hilo.

Serikali ya Kenya jana iliahidi kutoa ushirikiano kwa mahakama hiyo kuhusiana na uchunguzi huo. Tamko hilo limetolewa katika mkutano mjini Geneva baina ya baraza la umoja wa mataifa la haki za binadamu na ujumbe wa serikali ya Kenya ukiongozwa na waziri wa sheria wa Kenya.

Katika muhtasari wa mkutano huo , Kenya imesema itatoa ushirikiano kamili kwa mahakama hiyo ya kimataifa na kutoa uhakikisho wa kuwalinda mashahidi dhidi ya vitisho vya kutaka kuwadhuru.

Ahadi ya kuwalinda mashahidi ambao huenda wakatoa ushahidi imekuja baada ya ombi la kufanya hivyo lililotolewa na Austria, Korea ya kusini, Ireland, Australia , Norway na Ureno. Kenya pia imekubali kuchukua hatua zaidi kuzuwia hali ya kuepuka kuchukuliwa hatua kwa wale waliohusika katika ghasia hizo za baada ya uchaguzi.

Luis Moreno-Ocampo , mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita , ICC, ambayo ni mahakama pekee ya kudumu ambayo ni huru duniani , amekwenda nchini Kenya wiki iliyopita kukutana na watu walioathirka na ghasia zilizosababisha kumwagika damu nchini Kenya.

Akizungumza mjini Nairobi , amesema kuwa ni muhimu kufanya uchunguzi wa uhalifu huu ili kuhakikisha kuwa uchaguzi wa mwaka 2012 nchini Kenya unakuwa wa amani. Ameongeza kusema kuwa uchunguzi huo unapaswa kuwa onyo kwa mataifa mengine ya Afrika ambayo yanakaribia kufanya chaguzi.

Ocampo amesema kuwa katika mwaka mmoja na nusu ujao , kutakuwa na karibu chaguzi 15 katika bara la Afrika na wao wanapaswa kuhakikisha kuwa chaguzi hizi zinakuwa za amani. Kenya itatoa ishara kwa nchi zote kwamba ukifanya uhalifu dhidi ya ubinadamu utapelekwa The Hague katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita.

Ethiopia, Rwanda, Burundi, Tanzania na Uganda ni baadhi ya nchi za Afrika ambazo zinatarajia kufanya uchaguzi mnamo muda wa miaka miwili ijayo.

.

No comments:

Post a Comment