Saturday, May 22, 2010

JE TUMEJIFUNZA KUTOKANA NA CHAGUZI ZILIZOPITA?

Ndugu zetu,

Assalaam Alaaykum,

UMOJA, UHURU NA UADILIFU

Baada ya Uchaguzi wa 2005

Katiba ya Zanzibar ya 1984

Wakati Maalim Seif Sharif ni Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Katiba ya Zanzibar ilirejelewa na kuthibitishwa katika mwaka 1984. Ni ndivyo kabisa, kwa vile wakati huo nchi ilikuwa chini ya mfumo wa chama pekee (one-party system) katiba ya nchi kuwa ni yenye kulingana na mfumo wa kisiyasa ulikuwepo nchini wakati huo. Katiba hii ndio ilioendesha uchaguzi wa 1990, haikuwa sivyo kuwa hivyo, kwa sababu nchi ilikuwa katika mfumo wa chama pekee, na katiba halikadhaalika ilikuwa katika mfumo huo.

Kuletwa Nchini Mfumo wa Zaidi ya Chama Kimoja

Mnamo 1992 uliletwa nchini mfumo wa zaidi ya chama kimoja (multi-party system) na kufuta mfumo wa chama pekee (one-party system). Ilikuwa ni ndivyo kabisa mara tu baada ya kuletwa mfumo huo wa zaidi ya chama kimoja, wakati huo huo katiba ya nchi itengenezwe iwe yenye kulingana na mfumo wa kisiyasa uliopo nchini, yaani mfumo wa zaidi ya chama kimoja. Hili halikufanywa, nchi iliendelea kuishi katika katiba ya mfumo wa chama pekee hali ya kuwa nchi wakati huo ishaingia kwenye mfumo wa chama zaidi ya kimoja. Huu ni mpingano mkubwa wa kisiyasa na kiutaratibu wa uendeshaji wa mambo ya nchi.

Uchaguzi wa 1995

Uchaguzi wa 1995 ndio uchaguzi wa awali kufanywa tangu pale nchi kuingizwa kwenye mfumo wa zaidi ya chama kimoja. Lenye kushangaza ni kwamba kwa muda wa miaka mitatu hata kufika huu uchaguzi wa 1995 katiba ya nchi iliendelea kubakia ile ile ya mfumo wa chama pekee. CUF, wakiwa ni wakhusika na waathirika kwa kubaki katiba kongwe kwenye mfumo mpya ilikuwa ni wajibu wao kuhakikisha kuwa wanaingia kwenye uchaguzi kwa katiba ya zaidi ya chama kimoja, badala ile ya chma pekee. CUF waliingia kwenye uchaguzi kwa katiba ile ile ya chama pekee.

Uchaguzi wa 2000

Maara tu baada ya uchaguzi wa 1995 ilikuwa ni wajibu wa CUF kudurusu na kuzingatia matokeo ya uchaguzi huo na kujifunza kutokana na kasoro zake. Kuu ya kasoro hizo ni ile katiba kongwe, katiba iliokwisha pitwa na wakati. Madhumuni muhimu ya kuzingatia kasoro hizo ilikuwa ni kupanga nyenzo na mbinu za kuepuka zisitokee kasoro hizo kwenye uchaguzi ufuatiao, yaani ule wa 2000. CUF haikufanya hivyo, natija yake kasoro zilezile - kuu ya kasoro hizo ni vile kutumika katiba ileile, katiba kongwe iliokwisha pitwa na wakati - ziliokuwepo katika uchaguzi wa 1995 zilitokea tena, na kuongeza maafa baada ya uchaguzi.

Uchaguzi wa 2005

Maara nyingi baada ya uchaguzi wa 2000 na matokeo yake, CUF walikuwa wakiahidi Umma kwamba hawataingia kwenye uchaguzi 2005 mpaka katiba itengenezwe ilingane na mfumo uliomo nchini, yaani mfumo wa zaidi ya chama kimoja. Miezi michache tu kukaribia wakati wa uchaguzi, uongozi wa CUF uligeuza muelekeo wake na kuanza kusema kuwa CUF itaingia kwenye uchaguzi hata kama katiba haitageuzwa. Kitendo hichi kiliwatia khofu na wasiwasi wengi waliokuwa wakitarajia matengenezo nchini Zanzibar. Zaidi wengi walitambua natija ya uchaguzi itakavyokuwa iwapo CUF wataingia kwenye uchaguzi katika katiba kongwe, katiba iliokwisha pitwa na wakati. Wengi walinasihi kuwa CUF ni vyema wasiingie kwenye uchaguzi iwapo katiba haitatengenezwa. Wako waliofika kuwaeleza CUF kuwa natija za uchaguzi itakuwa ndio kama vilevile za uchaguzi zilizopita, yaani ule wa 1995 na wa 2000. Uongozi wa CUF uling’ng’ania kuingia kwenye uchaguzi kwa hali yoyote ile.

Muumini Hatafunwi na Nyoka Pango Moja Mara Mbili

Mafunzo ya Dini yetu tukufu yanatufunza kwamba Muumini haifai kutafunwa na nyoka pango moja mara mbili. Makusudio ni kwamba ni wajibu wa Muumini kuchukuwa kila hadhari baada ya kuumwa na nyoka. Waswahili wanasema: “Ukiumwa na nyoka, ukiona ung’ongo huogopa”. Hii ndio sifa ya Muumin, bali ni ndivyo kwa kila mwenye busara. Kwa nini tukaumwa na nyoka pango moja mara tatu, 1995, 2000 na 2005. Kitendo hiki si dharau tu, bali ni zaidi ya hivyo; si sio kuwa ni mpango wa makusudi kwa madhumuni makusudi. Hatujui uchaguzi wa 2010 utakuwa vipi, lakini tukilinganisha matokeo ya tangu 1995, tuna sababu ya kukhofia kwamba na uchaguzi wa 2010 utakuwa vilevile katika katiba ileile kongowe ya 1984. Je, ikiwa hivyo ni nani wa kulaumiwa, ni uongozi wa CUF au Umma wa Zanzibar? Penye uhai tutaona.

Tufanyeje?

Naileta makala hii humu barazani mwetu adhimu, si kwa kuwa haya niliojaaliwa kuyaeleza yupo asieyajuwa na kuyafahumu, bali madhumuni khasa ya kuleta maelezo haya ni kuomba mashauri ya ndugu zetu wa ukumbi huu nini la kufanywa ili kuendeleza juhudi za kufikia matengenezo ya nchi yetu.

Wa Billah Tawfiiq

Frouk

May 22, 2010

.

No comments:

Post a Comment