Monday, May 17, 2010

MKUTANO WA WAISLAM NA SERIKALI WAANZA LEO UJERUMANI

Baraza jipya la waislam nchini Ujerumani leo linaanza mkutano wake wa kwanza mjini Berlin .Sambamba na hilo katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkali.

Majadiliano hayo kati ya wawakilishi wa serikali ya Ujerumani na wawakilishi wa waumini wa dini ya kiislam nchini Ujerumani leo yanaingia katika duru ya pili, baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Wolfgang Schäuble katika duru ya kwanza miaka minne iliyopita kuwasilisha ajenda muhimu mbele ya kamati hiyo.Sasa masuala hayo yako chini ya mrithi wake Thomas de Maizière kwa ufafanuzi zaidi.

Masuala hayo ni pamoja na elimu kwa maimamu katika vyuo vikuu vya hapa Ujerumani, mafunzo ya dini ya kiislam katika shule, mambo yaliyokatazwa katika uislam pamoja na chuki dhidi ya uislamu katika jamii ya Ujerumani

Kwa upande mwengine katika mkutano huo, kuna wawakilishi kutoka serikali kuu, serikali za mikoa pamoja na serikali za mitaa.Aidha kuna wajumbe wa vyama vinavyowakilisha takriban asilimia 20 ya waislam wa Ujerumani pamoja na watu binafsi waliyoalikwa kutoa mitizamo yao kwa niaba ya waislam wengine.

Hata hivyo Mwanzoni mwa mwaka huu waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani aliikatalia jumuiya mojawapao muhimu ya waislamu-baraza la waislamu,Milli Görüs kushikiriki kwa ukamilifu kwenye mkutano. Waziri huyo alieleza kwamba jumuiya hiyo bado ipo chini ya uchunguzi .

Lakini waziri wa mambo ya ndani wa sasa Thomas de Maiziere pia amesisisttza kwamba uamuzi huo ulikuwa sahihi.

Akizungumza hivi karibu waziri huyo alisema:

´´ Milli Görüs kwa muda mrefu imekuwa si miongoni mwa washiriki katika mkutano wa kiislam.Alimradi ni uchunguzi wa kisheria na siyo dhidi ya mtu binafsi, lakini pia juu ya tuhuma za vyama hivyo kutumiwa kwa ajili ya kufanya uhalifu, au ukwepaji kodi na tuhuma nyingine nzito,basi nakubaliana na uamuzi huo´´

Baraza la waislam lilitangaza kujitoa kabisa kushiriki katika majadiliano hayo na serikali.Chama kingine cha pili kwa ukubwa cha waislam nchini Ujerumani kilichomo katika baraza la waislamu nacho mnamo siku chache zilizopita kilitangaza kujiondoa kutoka katika majadiliano hayo.

Sababu kubwa ni kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani alikataa kwanza kufanyika kwa kikao cha ndani na waislam kuhusiana na suala la uwakilishi katika majadiliano hayo.

Lakini Waziri huyo wa Ndani de Maizière ameendelea kushikilia msimamo wake huo.

´´ Huko kungelikuwa sawa na kukataa misingi ya mkutano na hilo mimi nimelipinga vilevile.

Nasikitika kwa hayo lakini,mkutano unaweza kufanyika bila ya baraza hilo la waislamu´´.

Iwapo waziri wa mambo ya ndani ataendelea kutokubali kufikiwa kwa mwafaka basi mdahalo unaweza kufanyika nje ya mchakato wa mkutano. Huo ndi msimamo wa baraza Kuu la waislamu.


Aiman A. Mazyek ambaye ni Katibu Mkuu wa baraza hilo amemshutumu Waziri huyo wa ndani kwa kuuuweka mdahalo chini ya sera za wageni, hali suala hilo linawahusu waislamu milioni nne wanaoishi nchini Ujerumani.

´´Bilashaka bado hatujaufunga mlango , lakini tumesema tu ni kuwa kuna mipaka na kwamba hatuwezi kuendeleaa hivyo ati kwa sababu tu ya kushiriki.Tunataka kujadili uislamu katika misingi ya kanuni zetu lakini siyo kwa sera za wageni na za kuwahusisha wageni katika jamii ya kijerumani, uislamu hauhusiani na hayo, kwa hivyo tunaona kushiriki ni kama kupoteza nguvu ´´

Mkutano huo wa Berlin unafanyika siku moja baada ya kumalizika kwa kikao cha maimamu wa kiislam barani Ulaya huko mjini Vienna Australia, ambako wawakilishi kutoka Ujerumani Uingereza na Uholanzi, walielezea umuhimu wa kushirikiana na mamlaka husika pamoja na polisi katika kuzuia ongezeko la vijana wenye kufuata itikadi kali za kiislam.

No comments:

Post a Comment