Friday, May 28, 2010

MAHARAMIA WA KISOMALI WAKIMBILIA KISIWANI PEMBA

Watu tisa wanaodaiwa maharamia waliotaka kuishambulia meli ya Namtuna katika eneo la kati kati ya kisiwa cha Unguja na Pemba wamefukuzwa na halikopta ya askari wa umoa wa Ulaya na inadaiwa maharamia hao wamekimbilia Pemba.

Askari hao waliokuwa doria katika helikopta hiyo ya umoja wa Ulaya wamesema tukio hilo limekuja siku tatu tangu kutokea kwa tukio jingine katika kisiwa cha Sheli sheli.

Kiongozi wa opereseheni wa umoja huo unaofanya doria katika pwani ya Afrika ya Mashariki amesema wamepigiwa simu kuhusiana na kuwepo kwa tukio hilo kati kati ya visiwa vya Pemba na Unguja na hivyo kutuma helikopta hiyo na hatimae kuikoa meli hiyo na maharamia hao kukimbilia Pemba.

Amesema maharamia hao wameshindwa kuwafuatilia baada ya kuingia katika eneo la Pemba kutokana na sheria haziwapi mamlaka ya kuingi katika pwani ya Tanzania.

Akizungumzia tukio hilo mwana sheria mkuu wa serikali jaji Fred Tungelema amesema wakati umefika kwa serikali ya Tanzania kuweka mpango wa kuliwezesha jeshi kulinda maeneo yote ikiwemo bahari kuu.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa kusini Pemba Hassan Nassir amesema tukio hilo bado halijathibitishwa na kusema maharamia hao kukimbilia kisiwani humo ni uvumi.

Hivi karibuni mkurugenzi wa shirika la bandari Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe amesema tatizo la maharamia katika pwani ya Afrika ya Mashariki limesababisha wenye meli kupandisha gharama za usafirishaji wa mizigo.

Akizungumza katika mkutano uliojadili ushiriki wa Zanzibar katika soko la pamoja la Afrika Mashariki amesema hali hiyo inaweza kudhorotosha shughuli za bandarini na kuongezeka kwa bei za bidhaa.

No comments:

Post a Comment