Wimbi la utekaji wa meli linaloendeshwa na maharamia wa Kisomali limechukua sura mpya baada ya kuingia katika mwambao wa visiwa vya Pemba na Unguja.
Kufuatia hali hiyo, Ubalozi wa Ufaransa hapa nchini umekiri kuwapo kwa maharamia tisa, baada ya meli yao ya kivita kuwanasa watekaji hao katika mwambao wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Dar es Salaam jana, Balozi wa Ufaransa nchini, Jacques Champagne de Labriolle, alisema maharamia hao walikimbilia katika mwambao wa Tanzania baada ya kunaswa na vyombo maalumu vya meli ya kivita kutoka nchini Ufaransa iliyojulikana kwa jina la Eunavfor Atalanta, iliyowasili nchini jana alfajiri.
Balozi Champagne de Labriolle alisema meli hiyo ilikuwa na wanajeshi zaidi ya 50 wa Umoja wa Ulaya (EU), ambao walikuwa wakitokea nchini Somalia kulinda na kuzuia vitendo vitakavyofanywa na maharamia katika meli zinazopeleka misaada ya chakula nchini humo.
Akizungumzia tukio hilo, nahodha wa meli hiyo, Kamanda Fontarensky Guillautie, alisema waliwanasa maharamia hao wakiwa na boti mbili, ambao waliamua kukimbilia katika boti za wavuvi kwa lengo la kujificha.
“Baada ya kuwaona maharamia hawa waliamua kukimbia hadi kwenye boti za wavuvi kwa lengo la kujichanganya ili wasikamatwe… sisi kwa mujibu wa sheria zetu hatuna ridhaa ya kukamata watu wa namna hii katika mwambao wa Tanzania,” alisema Kamanda Guillautie.
Alisema waliwanasa maharamia hao baada ya kupewa taarifa za kuwepo njama za kutekwa kwa meli iliyokuwa na mzigo, ambayo haikufahamika mara moja ilikuwa inaelekea wapi, lakini kutokana na tukio hilo ililazimika kuingia Tanzania ili kujinasua kwenye makucha ya watekaji.
Balozi Champagne de Labriolle alisema hili ni tukio la kwanza kwa maharamia wa Kisomali kuingia Tanzania, ni vyema serikali ikawatafuta na kuwachukulia hatua za kisheria, kwa vile wanatishia usalama na kuzorotesha uchumi unaochangiwa na usafiri wa baharini.
“Ni vizuri vyombo vya dola vya hapa nchini vikafanya kazi ya kuwatafuta na kuwachukulia hatua za kisheria kwa kuwafungulia kesi mahakamani watu hawa ambao wamekuwa tishio kwa nchi zinazofanya biashara kwa kutumia Bahari ya Hindi,” alisema Balozi Champagne de Labriolle.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini limesema limejizatiti vya kutosha kwa ajili ya kukabiliana na tukio lolote la utekaji nyara utakaofanywa na maharamia hao.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, aliiambia Tanzania Daima jana kuwa jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola limeweka mikakati mikali ya kudhibiti hali hiyo.
“Unajua suala hili limeanza mbali mno, sasa limeanza kusogea kwenye ukanda wetu, napenda kukuhakikishia kuwa sisi polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine tumejipanga vizuri kukabiliana na hali hii,
“Unajua suala hili ni la kimataifa, hatuwezi kulikwepa, tumejipanga, kuanzia ukanda wa pwani hadi hapa Dar es Salaam ili kuona meli zote zinasafiri salama,” alisema DCI Manumba.
No comments:
Post a Comment