Saturday, May 15, 2010

MAFURIKO NCHINI KENYA

Kenya imetoa tahadhari ya mafuriko huku ikitangaza kuwa mabwawa matatu katika mto mrefu kabisa nchini humo, huenda yakafurika katika siku chache zijazo, huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha.

Mabadiliko ya hali ya hewa,imelaumiwa kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi ambayo yameharibu majengo na kusababisha vifo nchini Kenya.

Mkuu wa kitengo cha kukabiliana na maafa nchini Kenya kanali Vicent Anami amesema kua, kumesalia nafasi kidogo tu, kabla ya bwawa la Masinga kuanza kufurika na baadae mabwawa ya Kiambere na Gitaru pia.

Hali hiyo itasababisha mafuriko makubwa katika maeneo ya Kaskazini Mashariki na Mashariki mwa Kenya. Shirika la Msalaba Mwekundu limesema watu 81 wamepoteza maisha yao katika mafuriko na maporomoko ya ardhi, tangu mwanzo wa mwaka huu.

Msemaji wa shirika hilo, Nelly Muluka, amesema idadi ya watu walioathirika na mafuriko hayo inatarajiwa kuongezeka.

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo la Afrika Mashariki imesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi siyo tu nchini Kenya lakini pia Tanzania na Uganda.

No comments:

Post a Comment