Monday, May 24, 2010

HUKUMU YA LIYUMBA LEO

Macho na masikio ya Watanzania wengi leo yanaelekezwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa ajili ya kusikiliza hukumu ya kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba (62).

Kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Edson Mkasimongwa, ambaye pia ni Msajili wa Baraza la Ushindani, ndiye anayetarajiwa kusoma hukumu hiyo inayosubiriwa kwa shauku kubwa.

Kusomwa kwa hukumu hiyo leo ni utekelezwaji wa amri iliyotolewa na kiongozi wa jopo hilo, Mkasimongwa, Aprili 22, mwaka huu, muda mfupi baada ya Liyumba anayetetewa na mawakili Jaji mstaafu Hillary Mkate, Onesmo Kyauke, Majura Magafu na Hudson Ndusyepo kumaliza utetezi wao.

Liyumba na Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, walipandishwa kizimabani kwa mara ya kwanza Januari 27 mwaka jana na kufunguliwa kesi namba 27/2009, wakikabiliwa na mashitaka mawili ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma, mbapo Liyumba alidaiwa kuidhinisha mabadiliko ya ujenzi wa majengo ya minara pacha bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa BoT, hivyo kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Hata hivyo, Mei 27 mwaka jana Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, aliifuta hati ya mashitaka iliyokuwa ikiwakabili washitakiwa hao na kuwaachilia huru, lakini muda mfupi baadye walikamatwa tena na kupelekwa Kituo cha Polisi Salender Bridge na siku iliyofuata Liyumba peke yake ndiye alifikishwa mahakamani hapo na kufunguliwa kesi mpya namba 105/2009.

Aprili 9, mwaka huu, Liyumba alifutiwa shtaka la pili ambalo ni la kuisababishia serikali hasara hiyo. Mkasimongwa alisema jopo hilo limepitia kwa kina ushahidi uliotolewa na mashahidi wanane wa upande wa Jamhuri na vielelezo 12 na kupitia majumuisho ya kesi hiyo yaliyowasilishwa na mawakili wa pande zote mbili, jopo hilo liliona Liyumba ana kesi ya kujibu katika shitaka la kwanza la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

.

No comments:

Post a Comment