Monday, April 12, 2010

ZANZIBAR YANYANG'ANYWA UENYEJI RIADHA TAIFA CUP

Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA), kimepokwa uenyeji wa Mashindano ya Taifa ya mwaka huu yaliyokuwa yafanyike mwezi ujao kwenye Uwanja wa Amani visiwani humo.

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya Chama cha Riadha Tanzania (RT), jana, zinasema kuwa sasa mashindano ya mwaka huu yatafanyika tena jijini Dar es Salaam kama ilivyokuwa mwaka jana.

Mwaka jana, mashindano hayo ambayo hushirikisha takriban mikoa yote ya bara na visiwani, yalifanyika Uwanja wa Taifa jijini, ikiwa ni mara ya kwanza uwanja huo kutumika kwa michezo ya riadha tangu ufunguliwe.

Awali, RT ilitangaza kuwa Zanzibar itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya taifa, ili kuutangaza uwanja huo wa Amani ambao unafanyiwa ukarabati mkubwa hivi sasa.

Hata hivyo, mtoa habari huyo hakuweza kubainisha sababu za ZAAA kunyang’anywa uenyeji huo na kupewa Dar es Salaam, lakini alithibitisha kuwa, tayari Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAAA), kimeishapewa barua ya kujiandaa na mashindano hayo.

Juhudi za kuwatafuta viongozi wa RT ili kubainisha sababu za mabadiliko hayo, jana zilishindikana.


.

No comments:

Post a Comment