Thamani ya sarafu ya Euro imepanda katika masoko ya fedha, baada ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro kutangaza kuwa kanda hiyo ipo tayari kuipatia Ugiriki msaada wa dharura wa Euro bilioni 30.
Lakini Ugiriki inayokumbwa na mzigo mkubwa wa madeni imesema kuwa kwa hivi sasa haitochukua msaada huo. Waziri wa Fedha wa Ugiriki Giorgos Papaconstantinou ameeleza waziwazi kuwa nchi yake haijaomba msaada kutoka nchi hizo za kanda ya Euro.
Yeye anatumaini kuwa serikali yake itaendelea kupata fedha katika masoko ya hisa. Amesema, uamuzi wa washirika wake katika kanda ya Euro umedhihirisha kuwa wana imani na Ugiriki.
Nchi zinazotumia sarafu ya Euro zipo tayari kuipatia Ugiriki mkopo wa dharura wa Euro bilioni 30 kwa riba ya asilimia tano. Hata shirika la fedha la kimataifa IMF lipo tayari kuisaidia Ugiriki iliyo na matatizo ya fedha.
Ugiriki inahitaji kupata kama Euro bilioni 11.5 hadi mwezi ujao. Hiyo ni sehemu ya Euro bilioni 54 zinazohitajiwa na serikali ya Ugiriki katika mwaka huu ili iweze kulipa madeni yake na kukidhi mahitaji ya dharura ya bajeti.
Hesabu za mwisho zimeonyesha kuwa Ugiriki ina deni la kama Euro bilioni 300.
.
No comments:
Post a Comment