Thursday, April 1, 2010

ZANZIBAR INA ZIADA YA WALIMU 2,000

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amani Zanzibar Mh,Haroun Ali Suleiman, amesema Zanzibar ina ziada ya walimu 2,000 wa elimu ya msingi.

Waziri Haroun alisema hayo juzi mjini hapa alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya sekta hiyo tangu Rais Amani Abeid Karume alipoingia madarakani.

Alisema wamefanikiwa kuwa na walimu wa ziada kutokana na kuongeza juhudi za kusomesha walimu katika ngazi mbalimbali.

Aliongeza kuwa hivi sasa hawana walimu wa daraja la IIIA na kuongeza kuwa kuna walimu 1,200 wanaopata mafunzo kwa ngazi ya diploma katika visiwa hivyo.

“Tunategemea miaka miwili ijayo tunaweza tukafuta ngazi ya diploma na kuwa na walimu wanaochukua digrii,” alisema.

Aidha, alisema juhudi hizo pia zimesaidiwa na wahisani mbalimbali na kutoa mfano kuwa Marekani imewasaidia vitabu vya masomo ya sayansi na kwamba sasa kila mwanafunzi atapata kitabu kimoja cha kwenda kusoma nyumbani.

“Marekani imetumia dola milioni tano kwa ajili ya kutoa vitabu hivyo kwa wanafunzi na sasa kupitia Benki ya Dunia tunachapisha vitabu vya masomo mengine,” alisema.

Alisema pamoja na mafanikio hayo, wizara hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi pamoja na uhaba wa samani shuleni.


.

No comments:

Post a Comment