Friday, April 9, 2010

WAZIRI WESTERWELLE ATOA MWITO WA KUPAMBANA NA UHARAMIA AFRIKA


Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amezitaka nchi za Afrika mashariki zisimame kidete zaidi katika kupambana na uharamia kwenye himaya za bahari zao.

Waziri Westerwelle alitoa mwito huo mjini Dar Es Salaam kwenye mazungumzo yake na rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.

Amesema kwa kushirikiana na Ujerumani, nchi hizo zitaweza kukomesha uharamia unaotishia biashara ya kimataifa.Waziri huyo wa Ujerumani pia ameshauri kwamba nchi zaidi za Afrika zichukue hatua za kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa uharamia na hasa wa kutoka Somalia.

Naye waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe amesema mashambulio yanayofanywa na maharamia kwenye pwani za Afrika Mashariki yamesababisha madhara makubwa ya kiuchumi.

Waziri Membe pia ameitaka jumuiya ya kimataifa ifanye juhudi kubwa zaidi ili kurejesha mfumo imara wa utawala nchini Somalia.

Katika juhudi za kuiunga mkono Tanzania katika harakati za kupambana na maradhi ya malaria na ukimwi, waziri wa misaada ya maendeleo Dirk Niebel aneongozana na waziri Westerwelle katika ziara ya nchini Tanzania ameahidi msaada wa Euro milioni 8.5 zaidi kwa ajili ya miradi ya elimu ya afya inayotekelezwa nchini humo.


.

No comments:

Post a Comment