Wednesday, April 14, 2010

MWINYI AWAPASHA WANAOPINGA MSETO ZANZIBAR


RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, amesema wanachama wa CCM wanaopinga Serikali ya Mseto Zanzibar, wamechelewa kwa kuwa ilipitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) mwaka juzi.

Mwinyi alisema hayo jana baada ya kujiandikisha katika kituo cha Miembeni katika jimbo la Kikwajuni.

“Mimi au hata mwana CCM mwingine atakuwa amechelewa kutoa maoni ya kupinga Serikali hiyo. Tuliijadili na kupitisha Butiama, kwamba inafaa kwa Zanzibar. Tuiunge mkono,” alisema Mwinyi alipoombwa maoni yake kuhusu hilo.

Hoja ya Mwinyi imekuja baada ya uvumi baadhi ya viongozi visiwani hapa wanapiga kampeni ya siri ya kupinga maafikiano ya kuundwa kwa Serikali ya Mseto.

Mwinyi alisema anafurahia jinsi uandikishaji wa wapiga kura unavyoendeshwa na Wazanzibari wengi kuona umuhimu wa kujitokeza kabla ya kazi hiyo kumalizika mwisho wa mwezi ujao.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salum Ali, alisema kazi ya kuandikisha wapiga kura inafanyika katika hali tulivu, yakizingatiwa maafikiano baina ya Rais Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad.

“Hadi sasa Wazanzibari zaidi ya 300,000 wameandikishwa na kupewa kadi za kupigia kura, tunatarajia kuwa na wapiga kura zaidi ya 500,000 kwa uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu,” alisema Ali.

Aidha, baadhi ya viongozi wa CUF wameendelea kulalamikia kuwapo baadhi ya wanachama wao ambao wameshindwa kuandikishwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya kuchelewa kupewa kitambulisho cha ukazi ambacho ni muhimu kwao kuandikishwa.

“Tumelalamika vya kutosha, lakini tuna imani kuwa Rais Karume atafanya lolote ili kusaidia. Baada ya maafikiano, tunahitaji kuwa na uchaguzi huru,” alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Salim Bimani

.

No comments:

Post a Comment