Thursday, April 1, 2010

ASILI YA KISWAHILI

Audhu biLlahi mna shaytani rajym. Rabby ish rahlysadry wayasirly amry wahlul uqdatan min lisany yafqahu qawly.

Assalamu alaykum,


Hivi karibuni nilialikwa Nairobi katika mkutano uliolipiwa na African Union na Arab league kwa lengo moja la kusomesha Kiswahili katika skuli zote za bara la Afrika; na sababu kubwa zilizopelelea kuteuliwa Kiswahili ni kuwa lugha hii ina mengi yanayotokana na lugha za Kibantu na Kiarabu. Kweli kuna maneno yaliyochukuliwa kutokana na lugha nyinginezo kama Kihindi, Kireno, Kifursi, lakini maneno yenye asili ya Kiarabu ni mengi sana tena sana sana; wala hatuwezi kuyatoa maneno hayo tukabakiwa na Kiswahili tukijuacho leo na jana.


Ni kweli pia kuwa sehemu kubwa sana ya nahau ya Kiswahili inatokana na lugha za Kibantu hadi kufika wanaisimu kuitangaza kuwa lugha hii ni moja katika lugha za Kibantu. Haya yalikaririwa na baadhi ya wataalamu wa isimu waliokuweko katika mkutano huo wa Nairobi. Waliokuwa wakidai kuwa lugha hii ni ya Kibantu moja-kwa-moja walitoa mifano ya maneno wanayoyaita "common core of vocabulary" yaani maneno ambayo binAdam lazima awe nayo kwani yanamkhusu kwa karibu sana na iwapo maneno hayo ni ya lugha fulani basi ni moja katika sababu zinazoonesha kuwa lugha hiyo inatokana na lugha hiyo/hizo za asili ya maneno hayo. Tukatolewa mifano ya viungo vya mwili wa binAdam kama "kichwa, mgongo, kiuno" na kadhalika. Hoja ya pili ilielemea upande wa nahau na pakazungumzwa tabaka za makumbo ya isimu na kwa hakika kweli mengi sana ya hayo yalitokana na lugha za Kibantu. Mimi kwa upande wangu nikasema kuwa huu msimamo wa wanaisimu sikubaliani nao kwa sababu ni mtizamo wa kidoto unaoangalia vipengee fulani tu katika lugha ikisha kufikia uamuzi kama huo.


Nikaelezea kuwa ni kweli kabisa kuwa katika hiyo muiitayo "common core of vocabulary" au tuseme "maneno asasi" kuna yenye asili ya Kiarabu pia. Nikawauliza: jee kuna kitu muhimu kuliko uzao wa Mwanamke? Ilikuwaje basi neno hilo likawa na asili ya Kiarabu! Lakini suala muhimu kwangu ni kwanini mkazingatia isimu tu zinazomkhusu binAdam na mkayaweka upande maneno mengine yanayomkhusu kama vile "akili, fikra, busara, dhaniya, roho, uhai, mauti" na kadhalika ambayo pia ni muhimu kwa mwana wa Adamu?


Hata katika hiyo nahau, jee mmezingatia vile Kiswahili kinavyozungumzwa na Waswahili wenyewe au mnaangalia katika vitabu vilivyoandikwa na wale waliosomea nahau na kuandika walipokuwa shuleni? Hebu tuangalie mifano michache. Kwa dasturi, Waswahili wanaamkiana hivi:


Assalamu alaykum.

Waalaykum salaam.
Keyf halek?
Tayyib.
Khabari.
Nzuri.

Utaona katika maamkio hayo ya kila siku hamna hata neno moja lenye asili ya Kibantu. Nilipokuwa nikifanya tafiti katika sehemu za Amu, Pate na Siu nikiwasikia wenyeji wakisema maneno kama haya ambayo yanaonesha kadiri ya maneno ya asili ya Kiarabu yaliyomo katika lugha hii:


"BismilLahi baadatu na himdi na shkuri na salamu na salatu za Mhamadi 'lbashiri. Mhamadi alifutu hakudumu na dahari. Ayyuhaa 'lmaghruri ina khadaa Duniya."


Lakini wataalamu fulani walioko Chuo Kikuu cha Dar es-Salaam walipokumbana na maneno kama hayo katika kuandika kwao makamusi wakatupiga chenga na kuanzisha mtindo mpya wa kiajabu. Wakayachuja maneno hayo na kuyatia katika kumbo waliitalo "kishairi"! Na iwe iwavyo, sasa hicho "kishairi" ni cha lugha gani? Si kinasemwa na kuandikwa na haohao Waswahili!


Kwa ufupi, kwangu mimi naona ni makosa kusema "Kiswahili ni lugha ya Kibantu" na tukasita hapo. Mafrudhi tuseme "Kiswahili ni lugha ya Kibantu, lakini si kama lugha yoyote nyingine ya Kibantu kwa sababu ya kadiri kubwa sana ilivyoathiriwa na lugha ya Kiarabu."


Wala hatuwezi kulinganisha idadi ya maneno yenye asili ya Kihindi, Kireno, Kifursi na kadhalika na idadi ya maneno yenye asili ya Kiarabu katika lugha hii.


***Ibrahim Noor.

No comments:

Post a Comment