Tuesday, April 13, 2010

ALBINO AKATWA MKONO MORO


Watu wanne wanaodaiwa kuwa ni wa jamii ya Kimasai, wamemkata mkono wa kushoto Said Abdallah (41) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino) kwa kutumia sime na kisha kutoweka nao.

Tukio hilo lilitokea juzi majira sa saa 10:15 jioni katika kijiji cha Kibaoni, Kata ya Melela Wilaya ya Mvomero, Morogoto na kwamba albino huyo alikatwa mkono huo baada ya kuvamiwa na watu hao akiwa shambani kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro alipolazwa kwa matibabu, alisema akiwa shambani kwake ghafla walitokea watu hao wakiwa na sime na fimbo na kumtaka awauzie tumbaku na kabla hajawauzia mmoja wa watu hao alimpiga fimbo sehemu ya kichogoni na baadaye kumkata kwa panga katika paji la uso.

Abdallah alisema kuwa watu hao waliendelea kumshambulia kwa fimbo na hivyo kupoteza fahamu na alipozinduka alijikuta mkono wake wa kushoto ukiwa umekatwa katika sehemu ya kiwiko na hakuweza kuona kipande cha mkono huo.

Alisema baadaye alipiga kelele za kuomba msaada ambapo alitokea mwanamke mmoja ambaye hakumfahamu na kumsaidia kumrudisha nyumbani kwake huku damu nyingi zikimtoka.

Alisema watu hao walishawahi kumtishia maisha kutokana na kuingiza mifugo yao katika shamba lake, lakini alisema kuwa hakutoa taarifa polisi kutokana na wafugaji hao kuvamia sehemu kubwa ya kijiji hicho na kufanya uharibifu wa mazao huku wakitishia maisha ya wakulima wengine kijiji hapo.

Alisema kuwa kitendo cha kumkata mkono na watu hao kuondoka na kipande cha mkono huo kinaashiria kuwa ni kutokana na imani za kishirikina na si visasi.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kibaoni, Asikile Yuda, alisema kupitia kamati yake ya ulinzi na usalama pamoja na wasamalia wema walikwenda katika kituo cha polisi cha kati mjini hapa na kutoa taarifa kisha kupewa PF3 na baadaye kumpeleka katika hospitali ya rufaa ya mkoani hapa.

Alisema kuwa tukio hilo ni la kwanza kutokea katika kijiji hicho licha ya kuwepo kwa migogoro mingi ya wakulima na wafugaji na hivyo kuiomba serikali kuhakikisha kuwa ulinzi unaimarishwa kijijini hapo ili matukio ya aina hiyo yaweze kudhibitiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Issa Machibya alifika wodi namba moja alikolazwa albino huyo na kumpa pole na kulitaka jeshi la Polisi mkoani hapa kuhakikisha kuwa watu waliohusika katika tukio hilo wanakamatwa haraka na kufikishwa mahakamani.


.

No comments:

Post a Comment