Saturday, March 27, 2010

WALIMU ZANZIBAR WAPIGWA MARUFUKU KUVAA MABAIBUI

Na Salim Said

Wizara ya Elimu ya Zanzibar, imewataka walimu wa shule za serikali wanaovaa baibui kujieleza kwa maandishi sababu za kuvaa nguo hizo wawapo kazini.


Waziri wa Elimu wa Zanzibar, Haroun Ally Suleiman aliliambia gazeti hili jana kuwa wizara ina mwongozo wa mavazi kwa walimu na wanafunzi wanapokuwa shuleni hivyo hawaruhusiwi kuvaa baibui.


Alisema mwongozo huo wa mwaka 1988, ndio unaowaelekeza walimu na wanafunzi aina ya mavazi wanayopaswa kuvaa wawapo shuleni.


"Zanzibar tuna mwongozo wa mavazi kwa walimu na hata wanafunzi, ulitungwa tangu mwaka 1988," alisema Haroun. Alisema kwa mujibu wa mwongozo huo, walimu wanazuiwa kuvaa baadhi ya baibui hasa zile ambazo zinazovaliwa nyakati za jioni visiwani.


“Hatutaki mavazi ambayo yatamsumbua mwalimu wakati wa kufundisha, hatutaki mavazi yanayofunika uso au baibui ya jioni, haya haturuhusu kabisa,â€‌ alisema Waziri Haroun.


Kauli ya waziri huyo imekuja baada ya gazeti hili kumtaka atoe ufafanuzi wa malalamiko ya baadhi ya walimu wa Kisiwa cha Pemba kwamba Mratibu wa Elimu ya Msingi Faki Suleyum Faki amewataka wajieleze kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kuvaa baibui kazini.


Walimu hao walisema mratibu huyo amekuwa akiwataka wasivae nguo hizo kwa muda wote wawapo kazini jambo ambalo walisema kuwa hawajui msingi wake.


“Sisi hatuoni sababu ya mwalimu kukatazwa kuvaa baibui, hili ndilo vazi letu la stara, sasa serikali inapotuambia tusivae je inataka tutembee uchi,â€‌ alihoji mwalimu mmoja wa shule ya sekondari ya Minungwini ambaye hakutaka kutajwa gazetini.


Walimu hao walidai kuwa mratibu huyo amewataka wajieleze kwa kuvaa baibui baada ya kuwakuta wameyavaa wakati wa kazi alipokuwa akitembelea baadhi ya shule za serikali visiwani humo juzi.


"Kwa kweli sisi wengine kazi hii itatushinda kwa sababu, inatupelekea kumwogopa kiumbe mwenzetu badala ya Mwenyezi Mungu, leo akija mkaguzi kutoka wizarani walimu wanajificha, akiondoka ndio wanarudi," alisema mwalimu mwingine.


Mwalimu huyo alisema utaratibu huo, umewaathiri sana walimu wa kike katika shule nyingi Kisiwani Pemba kwani unawalazimisha waache vazi lao la asili na linaloendana na imani ya dini yao.


"Hivi sasa walimu wengi hatuvai baibui, kwa sababu ukikutwa tu na mkaguzi kutoka wizarani hiyo itakuwa kesi kwako, kwa hiyo wengine huamua tu kuacha kuvaa," alisema mwalimu mwingine.


Jitihada za gazeti kumpata Mratibu huyo wa Elimu zilishindikana baada ya kukosa mawasiliano yake ya simu ya mkononi. Hata hivyo, moja ya utamaduni wa muda mrefu wa visiwa vya Zanzibar ni vazi la baibui ambalo hutofautiana mitindo, ambalo huchukuliwa kama sehemu ya dini ya Kiislaam kwa wanawake kusitiri miili yao.


Katika siku za hivi karibuni vazi hilo la baibui limeshika kasi baada ya kuibuka kwa mitindo mbalimbali ya nguo hiyo maarufu visiwani Zanzibar na hivyo hata baadhi ya wageni kulipenda vazi hilo.

.

No comments:

Post a Comment