Tuesday, March 16, 2010

WACHACHE WADIANDIKISHA DAFTARI LA KUDUMU ZANZIBAR


Idadi ya wapiga kura Zanzibar imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na idadi ya walioshiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Hali hiyo imebainika katika majimbo mengi ambayo tayari yamekamilisha awamu ya mwisho ya uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Uchunguzi wa Nipashe umegundua kuwa majimbo mengi yameandikisha wapiga kura wachache, ingawa sababu hazijabainishwa.

Majimbo ambayo tayari yamekamilisha uandikishaji wapiga kura ni Mgogoni, Konde, Nugwi, Tumbatu na Mkwajuni

Uchunguzi unaonyesha kuwa katika Jimbo la Mgogoni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, watu walioandikishwa ni 6,284 tofauti na watu 7,835 walioandikishwa mwaka 2005 sawa na upungufu wa watu 1,551.

Aidha, katika Jimbo la Konde kisiwani Pemba watu walioandikishwa ni 7,451 tofauti na watu 8,177 walioandikishwa mwaka 2005, idadi ambayo ni sawa na upungufu wa watu 7,26.

Katika Jimbo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, watu walioandikishwa ni 8,452 tofauti na mwaka 2005 ambapo watu 9,626 walijiandikisha sawa na upungufu wa watu 1,172, wakati katika Jimbo la Tumbatu walioandikishwa ni 9,451 ikilinganishwa na watu 10,115 walioandikishwa 2005. Aidha, katika Jimbo la Mkwajuni watu 5,503 ndio walioandikishwa ikilinganishwa na watu 8,088 walioandikishwa 2005 sawa na upungufu wa watu 2,785.

Hata hivyo uchunguzi huo unaonesha idadi kubwa ya majimbo yaliyoathiriwa na upungufu wa watu walioandikishwa ni Pemba ambako ni ngome kuu ya Chama Cha Wananchi (CUF).

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salum Kassim Ali, alithibitisha kuwepo kwa upungufu mkubwa wa idadi ya watu wanaoandikishwa ikilinganishwa na 2005 tangu kuanza kwa zoezi la awamu ya pili Machi Mosi.

Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Uzanzibari Ukaazi, Mohammed Juma Ame, alisema idadi ya watu walioandikishwa imepungua kutokana na kudhibitiwa kwa vitendo vya udanganyifu.

Alisema tangu kuanza kutumiwa utaratibu wa teknolojia ya kisasa, majaribio ya watu kuandikishwa zaidi ya mara moja umekuwa ukikwama na kuna idadi kubwa ya watoto waliokamatwa wakitaka kuandikishwa wakiwa chini ya umri wa miaka 18.

Alisema kinachoonekana ni kwamba baadhi ya vyama vya siasa vilikuwa vikiandikisha watu zaidi ya mara moja, jambo ambalo limeweza kudhibitiwa na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Alisema anaamini wapiga kura wa Zanzibar hawatafika 500,000 kwani mbinu zote za udanganyifu zimedhibitiwa.

Aidha, alisema jambo linaloshangaza ni kuona kuna idadi kubwa ya watu waliochukua vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, lakini idadi ya watu waliojitokeza kujiandikisha ni ndogo.

Alitowa mfano katika Jimbo la Mgogoni Kisiwani Pemba, ambapo waliopewa vitambulisho vya ukaazi ni 8,813, lakini waliojitokeza kujiandikisha ni 7,513, wakati katika Jimbo la Konde vitambulisho vilivyotolewa ni 9,595 wakati waliojitokeza kujiandikisha ni 7,451.

Katika majimbo ya Unguja kama Nungwi vitambulisho vilivyotolewa ni 9,571, lakini watu waliojitokeza kuandikishwa ni 8,452.

Katika Jimbo la Tumbatu waliopewa vitambulisho ni 10,129, lakini walioandikishwa ni 9,451.

Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani, alisema hujuma za kisiasa zinazofanywa na watendaji wa serikali, ikiwemo Ofisi ya Usajili wa Wazanzibari Wakaazi na Tume ya Usajili ndio chanzo cha hali iliyojitokeza.

Alisema hadi sasa watu wengi wamekwama kuandikishwa kutokana na kunyimwa vitambulisho vya Uzanzibari Ukaazi.

Alisema katika Jimbo la Nungwi kuna watu 8,66 wameshindwa kuandikishwa kutokana na kukosa vitambulisho, licha ya kujitokeza kuomba vitambulisho, lakini wamezunguushwa hadi zoezi la uandikishaji limemalizika.

Alisema katika Jimbo la Konge, watu 7,54 wamekosa haki ya kuandikishwa wakati awamu ya mwisho ya uandikishaji imemalizika.

***Nipashe


.

No comments:

Post a Comment