Wednesday, March 3, 2010

UMEME ZANZIBAR KUREJEA JUMANNE IJAYO

Huduma ya umeme visiwani Zanzibar inatarajiwa kurudi Jumanne ijayo baada ya kukamilika kazi za utengenezaji wa kituo cha kupokea umeme kilichopo Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Hassan Ali Mbarouk, aliwaambia waandishi wa habari waliotembelea katika kituo chenye kufanyiwa matengenezo cha Fumba kwamba ikiwa kazi ya kurejesha huduma hiyo itafanyika kama ilivyopangwa basi huduma hiyo itarejea siku hiyo.

Alisema kazi hiyo iliyobakia ni kuunganisha waya za umeme kutoka nchi kavu na baharini na kazi hiyo ya kuunganishwa kwa waya kutoka katika vituo vya Fumba hadi Ras Kiromoni Tanzania Bara itachukua muda wa siku tatu.

Akitaja hatua zitakazochukuliwa za kurejesha huduma hiyo, Kaimu Meneja huyo alisema hadi Jumapili ijayo kazi ya matengenezo itakuwa imemalizika na matarajio Machi 8 kutafanyika vipimo vya majaribio na Machi 9 ndiyo huduma hiyo inatarajiwa kuwashwa.

Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kuchelewa kwa huduma hiyo kumesababishwa na mafuta yaliyokuwemo ndani ya waya zinazoleta umeme kutokuwa safi na kulazimika kusafishwa kwa muda wa siku tatu.

Wakazi wa visiwa hivyo wamekosa huduma ya umeme tangu Desemba mwaka jana, baada ya kutokea hitilafu katika kituo cha kupokea umeme huo kutoka Ras Kiromoni hadi Funmba mjini Unguja.

No comments:

Post a Comment