Wednesday, March 24, 2010

TANGU LINI UWELEWANO UKAPIGIWA KURA YA MAONI?



• Wengi wakikataa, ina maana uhasama uanze upya?
• Wenye uchu wa madaraka wamejaa Zanzibar na dunia nzima

Na Walusanga Ndaki

JE -- kwa msomaji wa makala hii – uliwahi kuona wapi watu wanaoamua kuheshimiana na kuelewana wakalazimishwa kupiga kura ya maoni?
Vilevile – jambo muhimu zaidi – iwapo kura ya maoni itaonyesha kwamba watu wengi hawataki maelewano kwa kupitia serikali ya mseto nchini Zanzibar, je huo ndiyo uwe mwisho wa maelewano baina ya watu wa visiwa hivyo?
Je, baada ya kura maoni kukataa maelewano, wanasiasa wa Zanzibar ambao hivi sasa wanakazania sharti ifanyike kura ya maoni, watafanya nini?...

Wataanza kuwaambia wananchi kwamba kwa vile kura ya maoni kuanzisha serikali ya mseto imekataa jambo hilo, kwa hiyo waendelee na uhasama wao kama ilivyokuwa huko nyuma?
Kama si hivyo, nia yao hasa ni nini ya kuwauliza watu kwa kura kuhusu jambo lenye kuleta heri kwa wote?
Je, kuna watu wanaogopa kukosa vyeo katika Zanzibar mpya ambapo “ulaji” wa kupitia siasa utabidi kugawanywa katika mikono mingi zaidi?
Kama si hivyo, nia ya kura ya maoni ni ya nini?

Je, wakati wa kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika, au wakati wa kuuganisha vyama vya Afro-Shiraz na TANU, wananchi wa Zanzibar – na wa Bara – waliulizwa kuhusu mambo hayo ambayo yalikuwa muhimu zaidi ya hili la kuleta uelewano na kuunda serikali ya mseto?
Hawa wanasiasa wanaong’ang’ania kura ya maoni leo hii – wengi wao wakiwa watu wazima wakati hayo yanafanyika -- hawakuwepo wakati huo na wakaitoa hoja kama hiyo ya kura ya maoni? Mbona walikaa kimya wakati huo? Au hivi sasa siasa zimekuwa za “mteremko mno?”

Maswali au kauli kama hizi zimetawala kuhusu Muswada wa Kura ya Maoni Zanzibar ambayo wanasiasa wanafiki wamekuwa waking’ang’ania ifanyike katika visiwa hivyo kabla ya kuundwa kwa serikali ya mseto!
Wananchi wengi nchini Tanzania, wenye nia njema kwa Wazanzibar na wengine kokote waliko duniani, wamesema wazi kupiga kura ya maoni kwa watu ambao maelewano yatawaletea neema na faida nyingi, ni jambo la kupoteza muda na fedha.

Hii ni kwa kutia maanani kwamba kura kama hiyo – kwa mategemeo ya wanasiasa wajuvi -- inaweza ikapigwa kwa misingi ya ushindani wa kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) na kuzaa matokeo ambayo siku zote yamechochea kuleta uhasama visiwani humo.
Kwa faida tu ya wasomaji, Muswada huo unatarajiwa kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo.
Kwa ufahamisho wa wasomaji wa tovuti hii, hii ni mara ya pili kwa mwandishi wa makala hii, kupinga kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu kuanzishwa kwa serikali ya mseto nchini Zanzibar kwani ni jambo la unafiki wa kisiasa na ni la kupoteza muda.

Kwa kweli – kwa watu wanaowaheshimu wananchi wenzao na kuwachukulia kwamba nao pia wana busara – kura hiyo ya maoni ambayo wanasiasa kadhaa wameng’ang’ania ifanyike -- ni jambo la kipuuzi!
Halina faida yoyote kwa mwenye nia njema na hali ya Zanzibar. Kinyume chake, wale wanaotaka kukwepesha serikali ya mseto -- hasa wanasiasa wa Tanzania Bara na “washikaji” zao wa Zanzibar – watakuja kujuta na kuona aibu kwa kung’ang’ania kitu ambacho hata watoto wa shule za msingi wanakiona ni kichekesho!

Jambo hili halihitaji maelezo marefu hasa kwa Wazanzibar kujua kilicho bora na kilicho kibaya kwao.
Makala hii inasisitiza tena kwamba matatizo ya Zanzibar yataisha tu pale Wazanzibar watakapong’amua kuwa kitu kimoja na kuanza kuamua kile kilicho muhimu kwao kwanza badala ya kuwafurahisha watu walio nje ya visiwa hivyo, watu ambao uchungu wa uhasama visiwani humo hawaujui!

Wazanzibar wanaoendekeza ushabiki wa kisiasa kwa kuwasikiliza wanasiasa wanaoishi nje ya visiwa hivyo, hususani wale wa bara, ni dhahiri watakuja kujilaumu siku moja, kwani moto wa kweli wa uhasama ukiibuka visiwani humo ni wao na familia na marafiki zao ambao watapiga magoti kuomba amani ambayo leo wanaikwepa.

Wenye uchu wa madaraka wamejaa Zanzibar, Tanzania Bara na dunia nzima – wote wakiwa ni wanasiasa wanaotegemea kuishi kwa kuwalaghai binadamu wenzao!
Wazanzibar wajifunze kuamua kilicho muhimu kwao kwanza –- wasikubali kuwafurahisha wanasiasa wa Tanzania Bara au kwengineko duniani!
Wasipofanya hivyo leo, wajue watakuja kujuta kwani watakuwa wamechelewa kufanya jambo lolote lenye heri kwao kwa kupoteza muda wao wakiwasikiliza wapiti njia!

.

No comments:

Post a Comment