Tuesday, March 23, 2010

MUSWADA KURA ZA MAONI ZANZIBAR WAPINGWA

Wakati muswada wa Sheria wa kuanzishwa kwa Serikali ya Mseto visiwani hapa, ukitarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaotarajiwa kuanza kesho, maoni dhidi ya muswada huo yameongezeka.

Idadi kubwa ya wakazi wa hapa wakiwamo wanachama wa CCM, wasomi na wanasheria kama vile Awadh Ali Saidi, wameendelea kusisitiza kuwa kuupigia kura za maoni muswada huo, ni kupoteza fedha na muda kwa kuwa tayari Baraza la Wawakilishi lilishatoa uamuzi kwa niaba ya Wanzibari, kuwa na
Serikali hiyo iundwe baada ya uchaguzi mkuu.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdallah Omar na Profesa Issa Shivji, pia waliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari wakihoji umuhimu wa kupiga kura ya maoni.

Wazo la kupiga kura hiyo lilitolewa Januari mwaka huu na Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abubakari Khamis Bakari na kupitishwa na Baraza ili kuwapa nafasi Wanzibari kuamua kuwa na Serikali ya mseto au la.

Muswada huo wa Sheria ya Kura za Maoni wa mwaka 2010 unatarajiwa kuwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi,
Hamza Hassan Juma, ili wajumbe wa Baraza waujadili na ikiwezekana upitishwe na kuanza kutumika mara Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, atakapousaini.

Aidha, Muswada huo utaipa uwezo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kusimamia upigaji kura hizo ikiwa ni pamoja na kupanga tarehe na kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki.

Kwa mujibu wa muswada huo, ni Wanzibari waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura tu, ndio watakaopiga kura ya kuulizwa ana kujibu ndio au hapana na gharama za shughuli hiyo zitabebwa na Wizara ya Fedha.

“ZEC ndio watakaotangaza matokeo na kama kutatokea shaka katika matokeo hayo, haitatiliwa maanani na kama ikitokea matokeo hayo yakafungana,
Tume itatangaza tarehe nyingine katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya matokeo hayo, kwa ajili ya upigaji kura mwingine,” Muswada huo unaeleza.

Hata hivyo, Mzanzibari aliyepiga kura anaruhusiwa kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar. “Uamuzi wa mahakama hiyo ndio utakuwa wa mwisho na hakuna rufani itakayokubaliwa katika Mahakama ya Rufani,”

Lakini kabla ya mtu kukata rufaa dhidi ya matokeo ya upigaji kura huo, atatakiwa kwanza kuwa na wapiga kura 10 kutoka kila mkoa visiwani hapa, wanaomuunga mkono na kulipa Sh milioni tano kwa ajili ya kufungulia kesi siku 30 baada ya matokeo kutangazwa.

Muswada huo ambao unasubiriwa kwa hamu pia unaeleza kuwa itakuwa ni kosa kwa mtu au taasisi kutangaza matokeo ya kura hizo kabla ya ZEC na unapendekeza faini ya kati ya Sh milioni moja hadi 10 au kifungo cha miaka mitatu jela au adhabu zote kwa pamoja.

Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee, alisema jana kuwa katika mkutano huo, kutawasilishwa pia miswada mingine minne ukiwamo wa Haki na Wajibu wa Mwanasheria Mkuu na Wanasheria wote wa Serikali ambao unatarajiwa kujadiliwa kwa siku mbili.

Pia alisema jumla ya maswali 104 yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa katika kikao hicho. Miswada mingine ni pamoja na wa Sheria ya Uvuvi, wa Sheria ya kuanzisha Baraza la Taifa la Michezo na wa Kuanzisha Mamlaka ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe.

***Habari Leo


.

No comments:

Post a Comment