Tuesday, March 2, 2010

MAPOROMOKO YAUA ZAIDI YA 100 UGANDA


Zaidi ya watu 100 wamekufa baada ya kutokea maporomoko ya ardhi eneo la milimani mashariki mwa mkoa wa Bududa nchini Uganda.

Waziri anyeshughulikia majanga nchini humo Musa Ecweru ameelekea eneo hilo kutathmini misaada inayohitajiwa.

Waokoaji wanafukua kwenye matope wakitumia zana hafifu za mkononi wakijafribu kutafuta walionusurika na miili ya watu waliokufa.

Zaidi ya watoto 60 hawajulikani walipo. Walikuwa wamejificha katika kituo cha afya ambacho nacho kilisombwa na maporomoko hayo.

Bw Ecweru amesema yeye mwenyewe amehesabu miili ya watu 58 lakini maafisa walimwambia takriban watu 106 wamekufa.

Amesema serikali yake imetoa majeneza 100.

Zaidi ya watu 300 inaarifiwa hawajulikani walipo baada ya nyumba zao kufukiwa na udongo katika eneo hilo baada ya mvua kubwa kunyesha hivi karibuni.

Waandishi wa habari wanasema mara kwa mara eneo hilo hukumbwa na maporomoko ya ardhi lakini idadi kubwa ya vifo ni jambo lisilo la kawaida.


No comments:

Post a Comment