Monday, March 15, 2010

ASHTON ZIARANI MASHARIKI YA KATI


Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, leo anaanza ziara yake ya Mashariki ya Kati, ikiwa ni ziara ya kwanza kuifanya katika eneo hilo tangu ateuliwe kushika wadhifa huo mwezi Desemba, mwaka uliopita. Bibi Ashton aliwasili nchini Misri jana jioni kabla ya kuelekea katika mataifa mengine matano ya eneo hilo.

Mkuu huyo wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema ziara yake hiyo katika eneo la Mashariki ya Kati ina ujumbe mahsusi wa kuzihimiza pande zote kushiriki katika mazungumzo ambayo yatalifanya eneo hilo kuwa na amani. Asubuhi ya leo Bibi Ashton anakutana na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Misri, Ahmed Abul-Gheit, na mkuu wa usalama, Omar Suleiman, ambaye ameongoza jitihada za Misri katika mazungumzo ya upatanishi ya Palestina na kuachiwa huru Gilad Shalit, mwanajeshi wa Israel aliyekamatwa na kundi la Hamas mwaka 2006 karibu na mpaka wa Gaza.

Ashton kukutana pia na Amr Moussa:

Bibi Ashton pia anatarajiwa kukutana na Mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu-Arab League, Amr Moussa, ambapo pia ataihutubia jumuiya hiyo. Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya amewasili katika eneo hilo wakati ambao juhudi za kimataifa za kuanzisha tena majadiliano yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na Palestina zikiwa katika hali ya hatari.

Wiki iliyopita, maafisa wa ngazi za juu wa Marekani na Palestina walitoa matamashi makali kufuatia hatua ya Israel kutangaza mpango wake wa kujenga makaazi mapya 1,600 ya walowezi huko Jerusalem Mashariki. Tangazo hilo lilitolewa wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, nchini Israel, muda mchache baada ya kiongozi wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, kukubali kuanza mazungumzo ya amani yasiyo ya moja kwa moja.

Akizungumzia hali ya kuongezeka kwa hali tete katika eneo la Mashariki ya Kati, Bibi Ashton alisema ana wasiwasi kufuatia mpango huo wa Israel na kumtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Benjamin Netanyahu, kuonyesha uongozi wake. Kauli hiyo aliitoa siku ya Jumamosi alipokuwa akizungumza na waandishi habari kando ya mkutano wa mawaziri sita wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya nchini Finland.

Baada ya Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton, kusema mpango huo wa Israel ni sawa na kuitusi Marekani, Netanyahu alisema ataanzisha uchunguzi na amelitaka baraza lake la mawaziri kuwa na utulivu kufuatia shutuma kali za Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Uhusiano kati ya Marekani na Israel:

Bibi Clinton pia aliionya Israel kuwa hatua hiyo inatoa ishara ya kuharibika kwa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili. Aidha, mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya waliungana na Bibi Ashton kabla ya ziara yake hiyo, baada ya miezi kadhaa ya kukosolewa. Bibi Ashton sasa anahitaji kuungwa mkono ikiwa anajaribu kuiinua sura ya Umoja wa Ulaya kama mpatanishi wa mpango wa amani katika Mashariki ya Kati. Ziara hiyo ya Bibi Ashton itazihusisha pia nchi za Israel, Palestina, Lebanon, Syria na Jordan.


.

No comments:

Post a Comment