Sunday, February 28, 2010

ZAIDI YA RAIA 300 WAFARIKI BAADA YA TETEMEKO LA ARDHI NCHINI CHILE

Maafisa wa serikali nchini Chile wanasema kwamba kiasi cha watu 300 wamefariki kufuatia tetemeko la ardhi la 8.8 kwenye kipimo cha Ritcher lililopiga kwenye mwambao wa nchi hiyo mapema jana asubuhi.

Idadi ya watu waliofariki inatarajiwa kuongezeka. Rais wa Chile Michelle Bachelet amesema mkasa huo ni janga la kitaifa. Uharibifu mkubwa umeripotiwa katika mji wa Concepcion kilomita 100 kutoka eneo lilikoanzia tetemeko hilo ikiwa pia ni kilomita 300 kutoka mji mkuu Santiago.

Tetemeko hilo la ardhi limesababisha Tsunami katika bahari ya Pacific huku nchi kadhaa katika eneo hilo zikiwa katika hali ya tahadhari kukabiliana na kishindo cha Tsunami.Kituo kinachohusika na utoaji onyo la kutokea kwa Tsunami,kimethibitisha kwamba mawimbi ya Tsunami yamepiga kwa muda mfupi eneo la Hawaii.Aidha maeneo ya Polynesia, Ufaransa, kisiwa cha Chadham mashariki mwa NewZealand na miji ya pwani ya Chile pia yameshuhudia mawimbi hayo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametuma rambirambi zake kwa waathiriwa na amesema kundi la waokoaji limetumwa nchini Chile. Rais wa Marekani Barack Obama ametuma rambirambi zake kwa raia wa Chile waliopoteza jamma zao na ametoa onyo kwa wakaazi ufuoni ikiwemo Hawaii wawe chonjo.

Jumuiya ya Ulaya imeahidi kutoa euro millioni tatu kwa ajili ya kusimamia msaada wa dharura.

Rais Bachelet amesema zaidi ya makaazi milioni mbili yamaeathiriwa na laki tano yameharibiwa vibaya.

No comments:

Post a Comment