Tuesday, February 23, 2010

WATANO WA FAMILIA MOJA WAFARIKI KWA AJALI YA GARI PWANI

Ajali za barabarani zimeendelea kutisha katika mkoa wa Pwani baada ya watu watano wa familia moja kufariki dunia papo hapo na wawili kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha magari mawili waliyokuwa wakisafiria kugongana katika eneo la Ruvu - Nafco wilayani Bagamoyo.

Ofisa Upelelezi mkoani Pwani, Nsato Marijani aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo liilitokea katika barabara ya Dar es Salam - Morogoro na ilihusisha magari mawili ambayo yaligongana uso kwa uso na kusababisha vifo hivyo pamoja na majeruhi.

Alisema gari lenye namba za usajili T 707 EEF aina ya Fuso lililokuwa likiendeshwa na Abdul Hassan (30) mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Morogoro liligongana na gari ndogo aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 529 AED lililokuwa likiendeshwa na mtu aliyetambulika kwa jina moja la Mohamed.

Marijani alisema baada ya ajali hiyo, watu watano waliokuwa wamepanda gari dogo lililokuwa likitokea Morogoro, akiwemo dereva walifariki dunia na maiti zote zimehifadhiwa katika Hospatali Teule ya Tumbi wilayani Kibaha.

Aliwataja waliofariki kuwa ni mtoto wa miaka minne ambaye hakutambulika jina, Mwasiti Hamisi (23), Mwalami Salumu (21), Fatuma Salum (23) na dereva wa gari hilo aliyetambulika kwa jina moja la Mohamed wote wakazi wa Dar es Salaam.

Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Mohamed Salum (30) na Yasira Mohamed (2) wote wakazi wa Dar es Salaam ambao wamelazwa katika Hosptali ya Tumbi kwa matibabu.

No comments:

Post a Comment