Tuesday, February 23, 2010

SABABU YA MAUAJI YA WATU 17 MUSOMA


Mauaji ya kikatili ya watu 17 wa familia tatu yaliyotokea mwanzoni mwa wiki iliyopita katika Kata ya Buhare, nje kidogo ya Mji wa Musoma mkoani Mara, yameibua mambo mengine mazito yaliyofichika.

Uchunguzi wa umebaini kwamba, katika tukio hilo majeruhi watatu waliopelekwa katika hospitali ya Mkoa wa Mara, siku mbili baadaye mmoja alifariki dunia na kuacha ndugu wawili wakiendelea kuuguza majeraha

Ilibainika kwamba, chanzo cha mauaji hayo ya watu wa ukoo mmoja ni kutaka kulipiza kisasi cha muda wa miaka minne iliyopita kutokana na ukoo huo kudaiwa kuuwa watu fulani kwa tuhuma za wizi wa ng’ombe.

Uchunguzi huo unakwenda mbele zaidi kuwa, watu hao walitenda ukatili huo kwa kukusudia kutokana na ahadi ya nyuma waliyoitoa kuwa ndugu zao waliouawa mwaka 2005, hivyo ilikuwa ni lazima walipe kisasi.

Ilibainika kwamba, pamoja na kuwa na nguvu kubwa lakini nyumba za wanaukoo huo ziko mbalimbali hivyo kurahisha zoezi la mauaji kwani ingekuwa ngumu mno kukusanyika ili kukabiliana na maadui zao.

Ilifahamika pia kwamba, lengo la wauaji hao ilikuwa ni kumaliza ukoo mzima ili kupoteza ushahidi.

Akisimulia mkasa mzima, mtoto mdogo aliyenusurika aliyejitambulisha kwa jina la Kurwa Kawawa alisema kuwa alisikia milio ya mapanga na kelele za ndugu zake wakiomba msamaha kwa wauaji hivyo akaingia kwenye damu ambapo wauaji walidhani kuwa amefariki kumbe alikuwa hai.

Mwingine ambaye hakuweza kutaja jina lake kufuatia hofu kubwa aliyokuwa nayo, alisema alisikia wauaji wakimlazimisha kaka yake kutoa pesa ambapo aliingia uvunguni na ndipo alipoweza kuwashuhudia jamaa hao wakiwakata ndugu zake kwa mapanga na baadae walimvamia ng’ombe na kumcharanga mapanga.

Ilifichuka kwamba, wauaji hao walikuwa ni watu wenye hasira kufuatia kuwepo kwa madai kuwa waliouawa ni ukoo wenye tabia ya wizi wa mifugo, huku chuki ikitawala zaidi.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mstaafu Enos Mfuru ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa aliliagiza Jeshi la Polisi kufanya kila linalowezekana kuwakamata wote waliohusika.

Katika tukio hilo watu kumi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauji hayo.

No comments:

Post a Comment