Monday, February 8, 2010

VITAMBULISHO VYA KITAIFA KUGHARIMU BILIONI 200/-


Serikali imetenga sh bilioni 200 kwa ajili ya mradi wa utambuzi na usajili wa raia wake ambapo wakimbizi na wageni wataingia kwenye orodha hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Dickson Maimu, alisema fedha hizo zitatumika kwa miaka mitano.

Alisema fedha hizo zitahudumia miradi midogo midogo 14 ikiwemo kuanzisha ofisi kwa kila wilaya nchini kabla ya kuanza rasmi kwa kazi ya utambuzi na usajili ikishirikiana na wadau mbalimbali.

Mkurugenzi huyo alisema pia mradi utawaandikisha watu wote waliopo Tanzania bila kujali uraia wao na kwamba wakimbizi wataingia kwenye mradi huo.

“Hizi pesa ni nyingi kuzitaja, lakini ukweli ni kwamba zitatumika kwa miaka minne kutekeleza miradi midogo midogo ikiwemo ujenzi wa ofisi kila wilaya, ili kuwafikia wananchi wote.

“...Vitambulisho vya utaifa ni kwa ajiri ya usalama, wapo wanaofikiri sisi tunachapisha vitambulisho. Hapana! tunafanya utambuzi na kusajili watu walioko nchini kwa usalama wa nchi.

“Hivi vitasaidia kujua nani ni nani, anafanya nini na anamiliki nini. Hii itatusaidia hata kwa wageni. Mfano mzuri ni maafa ya Mbagala pale kusingekuwa na usumbufu kama mradi huu ungekuwepo watu wangetambuliwa,” alisisitiza Maimu na kubainisha kwamba watakaotambuliwa na kusajiliwa ni watu wenye miaka 18 na zaidi.

Alisema awali yalijitokeza makampuni 104 kutaka kupewa zabuni ya kufanya kazi hii kutokana na kushindwa kuelewa ugumu wa kazi na kwamba katika mchujo wa pili wa kumpata mkandarasi yamebaki makampuni matano yote kutoka nje ya nchi.

Kuundwa kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ni kutokana na uwezo alionao rais chini ya Ibara ya 36 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kwamba hicho ni chombo cha Muungano.

“Mpaka sasa mshauri mwelekezi amepatikana nayo ni kampuni ya Gotham iliyoshiriki katika upembuzi yakinifu ili kumpata mkandarasi atakayemudu kazi hii..,” alisema mkurugenzi huyo aliyeanza kazi Desemba mwaka jana.

No comments:

Post a Comment